Vijiji vilivyopisha mradi wa maji kupewa kipaumbele

Rai - - MAKALA - NA FERDNANDA MBAMILA

SERIKALI imeahidi kumaliza changamoto zilizopo kwenye vijiji vya Bwira Chini na Kiburumo, Kata ya Serembala, Wilaya ya Morogoro Vijijini.

Hatua hiyo imechukuliwa na Serikali hivi karibuni mara baada ya kuona kuna mkanganyiko baina ya wakazi wa vijiji hivyo na Mamlaka ya Maji Safi na Maji Taka, Dar es Salaam (DAWASA), ambapo mamlaka hiyo ilionyesha kutoeleweka kutokana na mkanganyiko uliojitokeza kati yake na wananchi.

Wakazi hao wanaotakiwa kuhamia eneo la Hungoni ili kupisha mradi mkubwa wa bwawa la Kidunda unaotekelezwa na Mamlaka hiyo kwa ajiili ya kuongeza uwezo wa mitambo ya Ruvu Juu na Ruvu Chini ili kufanya kazi ipasavyo.

RAI, lilipata wasaa wa kufika katika eneo hilo na kukutana na wakazi wa vijiji hivyo viwili vilivyo ungana, kwa ajili ya kuzugumza nao na kujua kero zao. Baadhi ya viongozi, wazawa na wahanga wa eneo hilo walilizungumia suala hilo kwa kina zaidi.

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Morogoro, Sudi Npili, anasema kuwa kwa sasa wameshapokea jumla ya shilingi 280 milioni zitakazotumika kurekebisha dosari ndogondogo zilizojitokeza wakati wa zoezi la ulipaji fidia kwa wakazi wa vijiji hivyo.

Anasema kuwa fedha waliyopokea itatumika katika ujenzi wa shule, zahanati pamoja na kuondoa dosari nyinginezo zilizojitokeza wakati wa zoezi la ulipaji wa fidia.

“Serikali inaendelea na utaratibu wa ujenzi wa zahanati na shule ya msingi na tayari tumeshapokea shilingi milioni 280, ikiwemo 56 mililoni kwa ajili ya ujenzi wa shule,”anasema Npili.

Mkazi wa kijiji Bwira Chini, Msafiri Gila anasema kuwa, wao kama wakazi wa eneo hilo, wameridhia kuhama, ila yapo mambo wanayotegemea, Serikali kuwakamilishia kama vile huduma mbali mbali za kijamii ikiwemo miundombinu ya maji.

Aidha, Gila anaongeza kuwa maji ndio kila kitu katika maisha ya mwanadamu, na hata wenyewe wanajua, hivyo kilio chao kitaisha endapo watatimiziwa kile kinachostahili katika kijiji chao.

“Sisi kama wakazi wa huku, tumeridhia wenyewe kuhama, ila tunaomba Serikali itusaidie kukamilisha mambo yaliyobaki ikiwemo ujenzi wa shule, zahanati, na miundombinu ya maji,” anasema Msafiri.

Kwa upande wake, Msemaji wa DAWASA ambaye hakutaka jina lake liandikwe, aliliambia RAI kuwa, mradi huo utakapoanza utawanufaisha wakazi wa vijiji hivyo, ikiwa ni pamoja na upatikanaji wa ajira, ujenzi wa barabara na miundombinu mingine.

“Mradi huu wa bwawa la Kidunda utakapokamilika utawanufaisha wakazi wa vijiji hivyo, ikiwa ni pamoja na kuzalisha umeme wa 20 MGW, upatikanaji wa ajira pamoja na miundombinu mingine,” anasema.

Anaongeza kuwa katika makazi mapya walihohamishiwa, DAWASA wana mradi wa kuchimba visima vya muda hadi mradi utakapokamilika. Tayari kisima kimoja kimekamilika na zoezi linaendelea.

Saidi Jimbo kutoka Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, naye pia alilizungumzia suala hilo kwa kinaga ubaga kuwa, zoezi la uhakiki lilifanyika kwa umakini na kila mtu alilipwa kufuatana na uhakiki ulivyofanyika, hivyo zoezi lililo baki ni uhamishaji wa makaburi pekee.

Anasema zoezi la uhakiki wa makaburi limeanza hivi karibuni na litakapokamilika, uhamishwaji utafanyika, ili kupisha ujenzi wa bwawa hilo.

Ujenzi wa bwawa la Kidunda utakapokamilika, utaondoa tatizo la maji katika Mkoa wa Pwani na Dar es salaam kwa kuongezea nguvu katika mitambo ya Ruvu Juu na Ruvu Chini.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.