Misaada ya maendeleo haisaidii kuleta usawa duniani

Rai - - KIMATAIFA / KATUNI -

Nchi tano masikini zaidi duniani kwa kipimo cha mgawanyo wa pato la taifa (GDP per capita) ni Jamhuri ya Congo, Msujmbiji, Uganda, Tajikistan and Haiti.

Hivyo mtu anaweza akadhani kwamba nchi hizi ni miongoni mwa nchi zinazopokea misaada mingi kutoka Uingereza. Si kweli. Nchi zinazopokea misaada mingi kutoka Uingereza ni Pakistan, Syria, Ethiopia, Nigeria na Afghanistan.

Na hakuna miongoni mwa nchi zile tano masikini zaidi duniani zimo katika kundi la nchi kumi za juu zinazopokea misaada kutoka Uingereza.

Wiki iliyopita, wakati wa ziara yake katika baadhi nchi za Afrika, waziri Mkuu wa Uingereza Bi Theresa May alisema kwamba katika kipindi cha baada ya nchi yake kujiondoa kutoka Umoja wa Ulaya (EU), bajeti yake ya fedha kwa ajili ya misaada itatumika kukukza biashara na masilahi yake ya kisiasa.

Hata hivyo, ndivyo hasa misaada kutoka nchi hiyo ilivyokuwa inatumika. Nchi ambazo hupokea misaada mingi zaidi kutoka Uingereza ni ama masoko makubwa kama vile Nigeria (iliyotembelewa na Theresa May wiki iliyopita), au zile nchi zilizopo katika maeneo muhimu hasa katika ‘mapambano dhidi ya ugaidi’ kama vile Pakistan, Afghanistan na Syria.

Hali kama hii iko pia kuhusu misaada kutoka Marekani. Hakuna nchi yoyote miongoni mwa nchi masikini zaidi duniani zimo katika kundi la nchi zinazopokea misaada mingi kutoka Marekani.

Badala yake misaada mikubwa mikubwa ya Marekani hupelekwa katika nchi za Israel, Misri, Jordan, Afghanistan na Kenya, vile vile kutokana na sababu za biashara na kisiasa.

Hali hii ni halisi pia kuhusu ile misaada inayopitia mashirika ya fedha ya kimataifa kama vile Benki Kuu ya Dunia (WB) na Shirika la Fedha Duniani (IMF). Hakuna nchi zilizo masikini zaidi duniani ambazo zimo katika miongoni mwa wapokeaji wakubwa kumi wa misaada kutoka taasisi hizo za fedha za kimataifa.

Ndani ya nchi zinazotoa misaada, watu wengi wa mrengo wa kulia hupinga sana misaada kwa nchi za nje, wakati wale wa mrengo wa kushoto huiunga mkono kama ni njia moja ya kugawana utajiri wa dunia. Lakini misaada hutolewa si kwa ajili ya hisani, inaunganishwa kama silaha ya kukuza uchumi na kufukuzia malengo mengine ya kisiasa.

Nchi nyingi tajiri huvuna fedha nyingi zaidi kutokana na malipo ya riba kutoka nchi zinazipokea misaada kuliko zile fedha wanazozitoa kama misaada.

Karibu nusu ya misaada yote inayotolewa kwa ajili ya maendeleo ‘hufungwa’, yaani nchi zinazopokea lazima zitumie misaada hiyo kununulia bidhaa na huduma nyingine kutoka nchi inayotoa misaada.

Tovuti ya shirika la misaada la serikali ya Marekani (USAid), kupitia kifungu chake kimoja ilikuwa inajigamba kwamba: “Mlengwa mkuu wa programu ya misaada ya nje ya Marekani siku zote imekuwa Marekani yenyewe. Karibu asilimia 80 ya mikataba ya USAid na misaada mingine huenda moja kwa moja kwa makampuni makubwa ya Marekani.

“Misaada imetengeneza masoko mapya kwa bidhaa za viwandani za Marekani na kuhakikisha malaki ya ajira kwa Wamarekani.”

Kifungu hicho hatimaye kiliondolewa mwaka 2006 baada ya kuona kilikuwa kinaiumbua Marekani. Hivyo hata kabla ya Donald Trump kuingia Ikulu ya Marekani misaada ya USAid ilikuwa inaiweka “Marekani Kwanza.”

Sehemu kubwa ya misaada ya nje huwa ni mikopo, ambayo huziumiza sana nchi zinazoendelea kutokana namalimbikizo ya madeni. Nchi nyingi tajiri hupokea zaidi kupitia riba.

Na kuanzia mtikisiko wa kifedha duniani wa mwaka 2008 serikali za nchi za magharibi zimeweza kuzidisha uwezo wao kukopa fedha kwa riba ndogo kwa kuanzisha programu za misaada kwa ajili ya kuzikopesha nchi masikini kwa riba kubwa, hivyo kutengeneza faida kubwa kupitia migongo ya watu wa nchi masikini. Wachunguzi wa mambo wanasema aina hii ya misaada ni kashfa tupu.

Kihistoria, Uingereza imekuwa ikitoa misaada yake kupitia fedha moja kwa moja (grants) kuliko mikopo. Lakini mwaka 2014 kamati moja maalum ya Bunge inayosimamia misaada ya maendeleo ya kimataifa ilipendekeza kutoa mikopo zaidi.

Aidha misaada ya nje si tu inakuza chumi za nchi tajiri, lakini pia inakuza sera zao kwa nchi za nje. Kutokana na Ripoti ya mwaka 2014 ya utafiti uliofanywa na Bunge la Marekani, “misaada inaweza kuwa kama karoti na fimbo, na ni nyenzo muhimu ya kushawishi mambo, kutatua migogoro fulani fulani na kudumisha hadhi ya Marekani.”

Katika kipindi cha Vita Baridi, nchi za magharibi zilikuwa zinatumia misaada kuzisaidia serikali zilizokuwa zikipinga ukomunisti. Na tangu Mashambulizi ya Septemba 11/2001, misaada imekuwa nyenzo muhimu ya vita dhidi ya ugaidi.

Na suala la sasa hivi linalohusishwa na misaada ni suala la uhamiaji. Nchi za Umoja wa Ulaya (EU) kwa mfano, zimezidisha kuifanya misaada kuwa na masharti kwa nchi za Kiafrika kuzuia uhamiaji wa watu wao kwenda Ulaya.

Na si nchi za magharibi pekee ambazo hufanya hivi, China pia sasa hivi ambayo ni nchi kubwa yenye kutoa misaada, pia huiona misaada kama nyenzo ya kuwania masilahi ya kisiasa. Nayo pia huifunga misaada yake na masharti ya ununuzi wa bidhaa na huduma kutoka China.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.