Mashabiki Simba wanavyochagiza ushindi wa timu yao

Rai - - MICHEZO - NA MWANDISHI WETUI

KWANI unadhani wahenga waliposema ‘ukiona vinaelea vimeundwa’ walikosea? La hasha walikuwa na maana wakiamini misemo yao yote kwenda sambamba na maisha ya wanadamu kulingana na mazingira halisi ya wanapoishi kwa wakati husika.

Pengine huo unaweza kuwa mfano mzuri kama si msemo huo kwenda sambamba na matukio mengi lakini moja ni hili la mafanikio yanayoizunguka timu ya Simba hasa katika matokeo ya uwanjani ndani ya dakika 90.

Ukitazama ushindi wa timu ni wazi unatokana na mambo mengi kufanikishwa na uongozi wa klabu hiyo ambao hivi karibuni wameanza kuonja ladha ya mabadiliko kwa kuanza kutumia mfumo mpya.

Simba imeweza kukata kiu ya mashabiki wake kuanzia msimu wa 2016/17 pale walipoukosa ubingwa dakika ya mwisho kabisa kwani waliachwa nyuma na watani zao wa jadi Yanga kwa tofauti ya mabao ya kufunga na kufungwa baada ya kufungana kwa pointi 68.

Kilichowatuliza wanachama na mashabiki wa klabu hiyo ni kupata tiketi ya kushiriki michuano ya kimataifa ambapo walicheza Kombe la Shirikisho baada ya kutwaa ubingwa wa Azam Confederation.

Hata hivyo msimu wa 2017/2018 wakatimiza ndoto yao ya kutwaa ubingwa tena baada ya kuukosa kwa takribani misimu minne hivi. Unajua siri ya mafanikio hayo

Hakuna shaka kwa watu walio karibu na klabu hiyo wanafahamuwazi mchango wa kundi la mtandaoni lijulikanalo kama ‘Simba Hq’ kwa msaada wao wa hali na mali katika kushirikiana na uongozi kuhakikisha wanapata matokeo ikiwemo kutwaa mataji.

Kundi maarufu la ‘Simba Hq’ chini ya uongozi wa Mwenyekiti wao, mfanyabiashara maarufu hapa nchini, Farouq Baghoza ni kundi linaloundwa na mashabiki wa timu hiyo wenye kada tofauti kama vile wabunge, wafanyabiashara, madaktari, walimu na wengineo wapatao 150 kutoka mikoa mbalimbali nchini.

Lilianzishwa kutokana na ubunifu wa Ofisa Habari wa klabu hiyo Haji Manara ambaye licha ya changamoto zilizokuwa zikiwakabili kiasi cha kusababisha hamasa kupungua hali ambayo ni wazi ilikuwa inaelekea kuitikisa timu.

Haji mmoja wa wasemaji wachache sana wenye mvuto wa aina yake pale anapotaka kujenga hoja ya kuitetea klabu yake alifanikiwa kuwakutanisha wanasimba wengi ndani ya kipindi kifupi ambapo katika muunganiko wao wakatengeneza taratibu zao rahisi sana za kuwaongoza hadi leo hii wanatembea wakifurahia mafanikio ya timu yao. Kwa mujibu wa mmoja wa Weka Hazina wa kundi hilo, Richard Malwiba mpaka sasa kundi hilo likiwa na uhai wa miaka miwili tu toka lianzishwe wamefanikiwa kukusanya zaidi ya shilingi milioni 300 na kuwapatia wachezaji kama bonasi.

Sifa za kujiunga kwanza ni lazima ama uwe mwanachama au shabiki wa klabu hiyo lakini pia utayari wa mhusika katika kutekeleza malengo ya kundi ambayo ni michango kila inapohitajika na wakati sahihi kisha kulipa kiingilio cha shilingi laki moja kama usajili wa mwanachama wa kundi.

Ni ubunifu ulioje kuweza kupata kiasi nkikubwa cha fedha kama hicho na kuzitumia kama hamasa kwa wachezaji wao

Utaratibu wa kundi hilo maarufu kwa wanasimba kama Simba Hq ni kutoa kiasi cha fedha sh. Milioni tano kwa kila mechi za Ligi Kuu, Kombe la FA ikiwemo michuano ya kimataifa ndani ya masaa 24 tu toka kupatikana kwa matokeo.

Katika kuthamini jitihada hizo, mwekezaji mkuu wa klabu hiyo, mfanyabiashara kijana, Mohammed Dewji maarufu kama ‘Mo’ aliamua kuwaunga mkono kwa kutoa kiasi cha fedha sawa na wanachotoa na kufanya kiasi wanachopewa wachezaji hao kuwa sh. milioni 10.

Mchanganuo wa zawadi hiyo unamfanya mchezaji wa Simba kuweka kibindoni kiasi cha kati ya sh. 450,000 na 350,000 kwa kila mechi huku ndani ya wiki moja tu wakiwa na uwezo wa kujiingizia kipato cha kati ya sh. 700,000 hadi 900,000 ukiangalia kwa mwezi utabaini wanapata fedha nyingi sana.

Utaratibu wa jinsi ya kugawanya fedha hizo kundi liliwaachia wachezaji wenyewe ambao chini ya usimamizi wa meneja wao Robert walikubaliana mgao uende sambamba na mchango wa kila mmoja katika mechi husika. Kama mtu alicheza anapewa mgao mkubwa, akifuatiwa na aliyekuwepo benchi na wale wasiokuwepo katika programu ya mechi wanapata kidogo.

Kuna baadhi ya nyakati kundi hilo huchangia sh. milioni 10 na wakichanganya na zile za Mo inafanya kiasi kuwa sh. milioni 20 kama kutakuwa na mechi kubwa.

Katika mtazamo wa kawaida wala haimchukui mtu kubaini umuhimu wa kundi hilo katika kuchagiza ushindi kwa timu yao.

Tathimini inaonyesha wazi toka kuanza kwa utaratibu huu umesaidia sana kurejesha hamasa kwa wachezaji katika kupambana na kutafuta ushindi. ‘Penye udhia penyeza rupia ‘ ndivyo inavyoelekea kwani ndani ya timu kumekuwepo hali ya kupambana pamoja na mshikamano miongoni mwa wachezaji.

Kupitia hilo, imesaidia kupunguza ubinafsi kwa badhi ya wachezaji kung’ang’ania kufunga hata kama yuko katika nafasi mbaya ilihali yuko mwingine aliyeko katika nafasi nzuri zaidi.

Kila mtu sasa anatambua iwapo watashinda watapata bonus hivyo wanachofanya ni kutafuta ushindi kwa ushirikiano mkubwa sana bila kujali nani atafunga kwa sasa kwao poini tatu ndiyo muhimu na sio nani kafunga.

Ni wazi suala zima la ushindi linatokana na uongozi kutekekeleza majukumu yao kwa kiwango kikubwa lakini bado michango ya kuchagiza hamasa kujitoa kama kundi hili yamerahisisha kwa kiasi kikubwa mafanikio ya timu yao.

Jonas Mkude (kushoto) akipokea fedha tasilimu shilingi milioni mbili kutoka kwa Mweka Hazina wa kundi la Simba Hq, Richard Malwiba (kulia) baada ya kutwaa tuzo ya mchezaji bora kutoka kwa mashabiki wa klabu hiyo.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.