Utabiri unaosubiriwa makundi 3 Uefa

Rai - - MICHEZO KIMATAIFA - HASSAN DAUDI NA MITANDAO

BARANI Ulaya mambo ni moto na hiyo ni baada ya droo ya hatua ya makundi ya msimu huu wa Ligi ya Mabingwa kuchezeshwa Alhamisi ya wiki iliyopita mjini Monaco, Ufaransa.

Kwa mujibu wa waandaji ambao ni Shirikisho la Soka la Ulaya (Uefa), mechi za raundi ya kwanza zitaanza kuchezwa Septemba 18 na 19. Unakosaje kwa mfano?

Katika makundi nane yaliyopangwa, kila moja liliwekewa timu nne na ni mbili pekee zitakazokuwa na nafasi ya kwenda hatua inayofuata ambayo ni ya mtoano (16 bora). Patamu hapo!

Wakati, Manchester United wakiangukia Kundi H ambalo linazihusisha Juventus, Valencia na BSC Young Boys, mahasimu wao wakubwa katika soka la England, Manchester City, wapo Kundi F, hivyo wataumana na Olympique Lyon, Shakhtar Donetsk na 1899 Hoffenheim.

Mabingwa watetezi, Real Madrid, wameangukia Kundi G linalowakutanisha na AS Roma, CSKA Moscow na FC Viktoria Plzen, huku Bayern Munich wakiwa Kundi E lenye Ajax, Benfica na AEK Athens.

Kundi D nalo si gumu kwa timu zote, hasa Porto na Schalke ambazo zina uhakika wa kwenda hatua ya mtoano mbele ya Galatasaray ya Uturuki na Lokomotiv Moscow kutoka Urusi.

Hata hivyo, wachambuzi wa soka barani Ulaya wameyapuuza makundi hayo, wakidai ni mepesi kwani vigogo wana nafasi kubwa ya kusonga mbele.

Hivyo, walichokifanya ni kutabiri kitakachojiri katika makundi mengine matatu yaliyobaki (A, B na C), ambayo kwa mujibu wao, ndiyo yanayopaswa kutolewa macho zaidi.

Kundi A (Atletico, Dortmund, Monaco, Club Brugge)

Kwa mashabiki wa kandanda, hilo ni ‘kundi la kifo’. Atletico Madrid ni tishio, wakiuanza msimu huu wa 2018/19, kwa kuwafunga Real Madrid na kuchukua ubingwa wa Super Cup.

Msimu uliopita, vijana hao wa kocha Diego Simeone walivurunda Ligi ya Mabingwa Ulaya lakini walipotua Ligi ya Europa wakawa mabingwa.

Katika kundi hili, wanakutana na Borussia Dortmund, moja kati ya timu ngumu si tu Bundesliga, bali hata barani Ulaya. Msimu uliopita, walimaliza wakiwa mabingwa wa Kombe la Ligi, tena kwa kuitandika Bayern Munich.

Licha ya Monaco, mabingwa wa Ligue 1 msimu wa 201617, kusifika kwa soka lake la kushambulia, kuna uwezekano mkubwa wa kushindwa kufua dafu mbele ya vigogo hao, ikizingatiwa kuwa ni timu mbili pekee zinazotakiwa kusonga mbele.

Wachambuzi wanatabiri kuwa Atletico wataongoza kundi, wakifuatiwa na Dortmund, Monaco na Club Brugge.

Kundi B (Barca, Tottenham, Inter, PSV)

Barca ambao ni mabingwa mara tano wa michuano hii, watakuwa na kibarua cha kumaliza hatua ya makundi wakiwa kileleni, jambo ambalo wamelifanya kwa misimu yote 11 iliyopita.

Watavaana na Tottenham ambayo licha ya kutosajili wakati wa kiangazi, hivi karibuni walithibitisha makali yao kwa kuitandika Man United mabao 3-0.

Huku PSV ikionekana kutokuwa na nafasi ya kusonga mbele, Inter nayo si ya kubeza kwani kwa sasa ni tishio kwa Juventus wanaojaribu kulitetea taji lao la Ligi Kuu msimu huu.

Utabiri wa wachambuzi ni kwamba Barca watamaliza hatua ya makundi wakiwa juu, na nafasi ya pili itashikwa na Tottenham, yaani Inter na PSV zitarejea nyumbani mapema tu.

Kundi C (Liverpool, PSG, Napoli, Crvena Zvezda)

Hili nalo ni kundi la kifo. Kwanza, linazikutanisha timu bora kwa sasa. Pili, ni klabu zenye kiu kubwa ya taji hilo, hasa PSG , Liverpoolna Napoli.

Msimu uliopita ulikuwa wa mafanikio kwa timu hizo. PSG walitwaa ubingwa wa Ligue 1, Napoli wakashika nafasi ya pili Serie A, na Liver walicheza fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Jambo zuri kwa mashabiki wa Napoli ni kuajiriwa kwa kocha Ancelotti, ambaye ana uzoefu mkubwa katika michuano hii.

Liver wao wanacheka tu, hasa baada ya kikosi chao kuongezewa makali na ujio wa kipa Alisson, na mastaa Fabinho, Naby Keita na Xherdan Shaqiri.

Msimamo wa mwisho katika kundi hili unatabiriwa kuiona Liver ikiongoza na PSG ikifuata, kwa maana kwamba Napoli sna Crvena Zvezda hazitaingia 16 bora.

Kikosi cha Tottenham

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.