Arsenal, Chelsea nani kuzoa tril 1.3-Ligi ya Europa?

Rai - - MAKALA JAMSEPITIEMBA -

DROO ya Ligi ya Europa ilichezeshwa mwishoni mwa wiki iliyopita mjini Monaco, Ufaransa, lakini macho na masikio ya mashabiki wa kandanda yalikuwa kwa Arsenal na Chelsea, mahasimu wa jijini London zinakotokea timu hizo.

Wengi walitaka kujua vigogo hao wa Ligi Kuu ya England (EPL) wangekua wapi, yaani wangepangwa na timu zipi katika makundi yao?

Hatimaye, Gunners wakaangukia Kundi E, hivyo kukutanishwa na Sporting Lisbon (Ureno), Qabarag (Azerbaijan) na Vorskla Poltava (Ukraine), huku Chelsea wakitupwa Kundi L lenye PAOK (Ugiriki), BATE Borisov (Belarus) na Videoton (Hungary).

Timu zingine na makundi ni kama ifuatavyo: Kundi A-Bayer Leverkusen, Ludogorets, FC Zurich na AEK Larnaca. Kundi B-Red Bull Salzburg, Celtic, RB Leipzig na Rosenborg.

Kundi C-Zenit, FC Kobenhavn, Bordeaux na Slavia Praha. Kundi D-Anderlecht, Fenerbahce, Dinamo Zagreb na Spartak Trnava.

Kundi F-Olympiacos, AC Milan, Real Betis na F91 Dudelange. Kundi G-Villarreal, Rapid Wien, Spartak Moskva na Rangers.

Kundi H-Lazio, Olympique Marseille, Eintracht Frankfurt na Apollon Limassol. Kundi I- Besiktas, Genk, Malmo FF na Sarpsborg 08.

Kundi J-Sevilla, Krasnodar, Standard Liege na Akhisarspor. Kundi K-Dynamo Kyiv, Astana, Rennes na Jablonec.

Mechi za raundi ya kwanza zitaanza kuchezwa Septemba 20, mwaka huu, na kufikia Desemba 13, zitakuwa zimebaki timu 32 pekee kati ya 62 zilizopo sasa.

Ni vita ya zaidi ya miezi nane (Sept 20Mei 29) na timu itakayoibuka kidedea itajinyakulia kitita cha Pauni milioni 455 (zaidi ya Sh Trl 1.3 za Tanzania).

Licha ya uwepo wa timu ngumu kama Marseille, Sevilla na Milan, Arsenal na Chelsea zinapewa nafasi kubwa ya kutwaa taji hilo, hasa baada ya kuikosa michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Ukiacha kufika nusu fainali msimu uliopita, ambapo Atletico Madrid waliibuka mabingwa, wachambuzi wa soka barani Ulaya wanaamini Arsenal ina cha kujivunia chini ya kocha Unai Emery.

Akiwa na kikosi cha Sevilla ya Ligi Kuu ya Hispania ‘La Liga’, mkufunzi huyo aliyetua Arsenal akitokea PSG, aliinyakua taji hilo mara tatu.

Kwa upande wake, Chelsea yenye maskani yake Magharibi mwa London kama ilivyo West Ham, nayo imeonekana kuwa na mabadiliko makubwa tangu kutua kwa kocha raia wa Italia, Maurizio Sarri.

Pia, ni kweli hawakufanya vizuri msimu uliopita, kiasi cha kushindwa kumaliza ligi wakiwa ‘top four’ lakini mataji mawili ya Ligi Kuu ya England ndani ya miaka minne iliyopita ni habari mbaya kwa wapinzani wao Ligi ya Europa.

Hata hivyo, licha ya kuzitabiria makubwa Arsenal na Chelsea, wachambuzi wanasisitiza kuwa Milan, Marseille na Sevilla ni tishio kubwa kwa wawakilishi hao wa England.

Ni kweli Milan haijaweza kurejea katika ubora wake wa miaka mingi iliyopita, lakini si timu ya kubeza, hasa katika michuano hii. Hapo unaizungumzia timu yenye mataji 14 ya mashindano ya Ulaya.

Chini ya mchezaji wao wa zamani ambaye kwa sasa ndiye kocha, Gennaro Gattuso, Milan inatazamiwa kuwa tatizo kwa Arsenal na Chelsea katika mbio za kuufukuzia ubingwa wa Ligi ya Europa msimu huu.

Faraja kubwa waliyonayo mashabiki wa Milan ni uwepo wa mpachikaji mabao wao mpya aliyepishana mlangoni na staa Cristiano Ronaldo pale Juventus , Gonzalo Higuain.

Ukiitazama Marseille, klabu yenye mashabiki wengi zaidi katika soka la Ufaransa, nayo si ya kupuuzwa. Hakuna ubishi kuwa PSG wanaitawala Ligi Kuu ya Ufaransa ‘Ligue 1’ lakini Marseille wanajivunia kucheza fainali ya Ligi ya Europa msimu uliopita.

Hakika utatarajia kukiona kikosi chenye mastaa kama Dimitri Payet na Kevin Strootman kikiitoa jasho si tu Arsenal au Chelsea, bali timu yoyote barani Ulaya.

Sevilla ni tatizo jingine kwa Arsenal na Chelsea. Kutokana na mafanikio yao katika michuano hiyo, wamepachikwa jina la ‘Wafalme wa Europa’.

Tangu mwaka 2006, wamelibeba mara tano, ikiwamo rekodi yao ya kuvutia ya kulipeleka kabatani mara tatu mfululizo (2013-2016).

Kumbukumbu itakayowafaa mashabiki wa Arsenal na Chelsea ni ile ya msimu uliopita ambapo Sevilla waliing’oa Manchester United katika hatua ya robo fainali ya mashindano haya ya Ligi ya Europa.

HASSAN DAUDI NA MITANDAO

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.