UJAUZITO WAMSABABISHIA MWANAMKE KIPARA

Rai - - MBELE - NA HASSSAN DAUDI

NIKWAMBIE tu kwamba changamoto ni sehemu ya maisha. Ni kama wasemavyo Waswahili, maisha ni safari yenye milima na mabonde.

Hivyo basi, usiamini wewe ndiye mwenye matatizo zaidi ya wengine na ikafikia hatua ya kukufuru (kufanya kinyume cha matakwa ya Mungu) kwa kuhisi hakutendei haki.

Je, ni utafiti gani ulioufanya ukakuonesha kuwa tatizo linalokubabili sasa ni kubwa zaidi ya waliyonayo wengine? Kumbuka, kwako kukifuka moshi, kwa mwenzako kunateketea kwa moto.

Mfano mzuri katika hilo, hebu tiririka na kisa hiki cha bibiye Emma Holmes, mkazi wa North Yorkshire, Uingereza, mwenye umri wa miaka 40.

Simulizi inaanzia akiwa na umri wa miaka 16, ambapo mimba yake iliharibika, na mbaya zaidi alijikujikuta akipoteza uwezo wa kupata ujauzito.

Kuanzia kipindi hicho, Emma aliyewahi kuwa mwalimu, akaamini ataondoka katika ulimwengu huu akiwa hana mtoto, na anasema alithibitishiwa hivyo na madaktari.

Katika hali ya kushangaza, mwaka 2009, vipimo vya madaktari vilithibitisha kuwa alikuwaa na ujauzito, jambo ambalo lilimwacha hoi, japo alilifurahia mno.

Lakini sasa, ghafla mrembo huyo alianza kutokwa na damu mara kwa mara na alipokwenda hospitali, aliambiwa mimba imetungwa nje ya mfuko wa uzazi.

Kwa mara nyingine, Emma alijikuta akimpoteza mtoto mwingine, safari hii ikitokana na upasuaji aliofanyiwa.

Hata hivyo, wakati akiwa katika kipindi hicho kigumu, likaibuka balaa jipya. Mama yake mzazi alibaini kuwa nywele za mwanawe huyo zilikuwa zikiisha kichwani, tena kwa kasi ya ajabu.

Mbaya zaidi, haikuishia katika kupoteza nywele za kichwani. “Siku moja mama alinitazama na kugundua kuwa nywele zilianza kuniota mabegani, hali ambayo sikuwa nayo hapo awali,” anasimulia mwanamke huyo.

Katika mahojiano yake na gazeti la Metro la Uingereza, hapa Emma anasimulia ilivyokuwa. “Nywele zilipoanza kuondoka kichwani, nilijikuta nikishindwa kutoka nje kwa wiki kadhaa (kwa sababu ya aibu),” anasema Emma kuwaambia waandishi wa Metro.

“Unajua mwanzoni familia yangu iliona ni jambo la ajabu lakini binafsi nililichukulia poa tu. Sikuwa nikilifikiria sana.

“Siku moja nikiwa naoga, nikagundua kuwa kulikuwa na tatizo. Ilinikera mno. Kila nilipojishika kichwani, nywele zilikuwa zikibaki mikononi, sikuweza kuzizuia.”

Aidha, mlimbwende huyo anaendelea kusimulia kuwa hata madaktari walipochukua vipimo kwa ajili ya uchunguzi wa kitaalamu, hawakuweza kubaini chanzo cha tatizo lake hilo. “Sikuweza kupata jibu,” anasema.

Baada ya muda mfupi, tayari sehemu kubwa ya kichwa chake haikuwa na nywele kabisa na kuanzia kipindi hicho usingeweza kumuona Emma akiwa bila ‘wigi’ kichwani, lengo likiwa ni kuficha kipara chake.

Kwa mujibu wake, kipindi hicho alilazimika kusitisha kujumuhika na marafiki zake, ikifikia hata hatua kuacha kazi ya ualimu. Alipotoka nyumbani, ni pale tu alipokwenda hospitali kumuona daktari.

Tofauti na tatizo lilipoanza mwaka 2009, baada ya kuishi na hali hiyo kwa takribani miaka tisa, hivi sasa Emma ameshaizoea ingawa si rahisi kusema anafurahia kuendelea kuishi nayo kwa miaka mingi ijayo.

Huenda ukawa unajiuliza alivyoweza kuyazoea majanga hayo, kiasi kwamba sasa anayaona ni kawaida. “Mbali ya kula mboga za majani kwa wingi, pia nimekuwa nikichoma sindano zinazoelezwa kusaidia uoteshaji wa nywele, tiba ambayo nakiri kuwa inanisaidia,” anasimulia.

Wakati huo huo, kwa kutambua kuwa tatizo hilo linaweza kuwa si la peke yake, ameanzisha kituo cha kuwasaidia wanawake wengine nchini Uingereza na ulimwenguni kote.

Akiwa ameshawahudumia maelfu ya wanawake, hapa Emma anaelezea ushauri anaowapatia kabla, wakati na baada ya matibabu. “Huwa nawaambia wataishinda hali hii.”

Tukutane wiki ijayo kwa kisa kingine. Duniani kuna mambo bwana!

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.