Waziri wa Sheria apigilia msumari

Rai - - MBELE - NA GABRIEL MUSHI SAKATA LILIVYOANZA

KAULI hiyo ya Rais Magufuli ambayo kimsingi ndiyo iliyozua mjadala mkubwa na hata baadhi kuanza kubashiri kuhusu hatma ya Ukuu wa Mkoa wa Makonda, imeendelea kuwasha moto baada ya Prof. Kabudi kuelezea wazi kuwa hata yeye hana gari la kutembelea kwa sababu baadhi ya magari ya wizara hiyo yamekwama bandarini hadi yatakapolipiwa kodi.

KAULI ya Waziri wa Sheria na Katiba, Profesa Palamagamba Kabudi kuwa mtu yeyote kutoka mbinguni au duniani lazima alipe kodi, imeendelea kupigilia msumari sakata la makontena 20 yanayodaiwa kuwa ni ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda ambayo yameibua mjadala baada ya Mamlaka ya Mapato Nchini (TRA) kutaka yalipiwe kodi. RAI linachambua.

Msingi wa sakata hilo ni uwapo wa taarifa kuwa Makonda ameomba msamaha wa kodi.

Makontena hayo yanayotajwa kuingizwa nchini kwa jina la Paul Makonda yakiwa na samani mbalimbali zinazodaiwa ni kwa ajili ya shule za mkoa anaouongoza, yamezua gumzo baada ya kupigwa mnada mara mbili bila mafanikio.

Kauli hiyo ya Prof. Kabudi imeshabihiana na kauli ya Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango pamoja na Rais John Magufuli ambaye wiki iliyopita alihoji sababu za Makonda kutolipa kodi kwa sababu katika sheria za nchi ni mtu mmoja tu aliyepewa dhamana kwa mujibu wa sheria ya fedha, sheria ya madeni, sheria ya dhamana na misaada.

“Nafikiri kupitia sheria namba 30 ya mwaka 1974 kifungu cha 3, 6, 13 na 15, ndiye amepewa dhamana ya kupokea misaada kwa ajili ya nchi, hakuna mtu mwingine, hayupo.

“Sasa ukichukua makontena kule umezungumza na watu wengine au na wafanyabiashara, unasema una makontena yako, halafu unasema ya walimu wala hata shule hazitajwi.

“Hii maana yake nini? Si unataka utumie walimu ulete haya makontena, utapeleka shule mbili, tatu, ndizo zitapewa mengine utakwenda kuyauza kwenye ‘shopping mall’, lakini walimu walikwambia wanahitaji masofa? Wafanyakazi wasitumike kwa masilahi ya watu fulani,” alisema Rais Magufuli.

Kauli hiyo ya Rais Magufuli ambayo kimsingi ndiyo iliyozua mjadala mkubwa na hata baadhi kuanza kubashiri kuhusu hatma ya Ukuu wa Mkoa wa Makonda, imeendelea kuwasha moto baada ya Prof. Kabudi kuelezea wazi kuwa hata yeye hana gari la kutembelea kwa sababu baadhi ya magari ya wizara hiyo yamekwama bandarini hadi yatakapolipiwa kodi.

Akizungumza na Watanzania waishio nchini Marekani mwishoni mwa wiki iliyopita, Prof. Kabudi alisema nchi ikishaanza kuchezea misamaha ya kodi imekwisha kwa sababu kila mtu atatafuta mwanya wa kusamehewa kodi.

“Sasa tunakusanya pesa… tunasimamia kodi ndio maana kwenye hilo hakuna exception, kwenye sheria ya kodi hakuna exception, mpaka serikali tunalipa kodi, mimi wizara yangu sina gari la waziri, tumeagiza magari yapo bandarini. Yanasubiri kodi, mengine yamekaa miezi saba yanasubiri pesa tulipe kodi.

“Unajua mkishaanza kuchezea kodi kwa misamaha mmekwisha, kila mtu atatafuta mwanya. Kwa hiyo chini ya serikali hii, serikali yenyewe na yeyote yule. Atoke mbinguni, atoke duniani atalipa kodi. Atalipa kodi lazima… hilo ni muhimu tunalijua,” alisema Prof Kabudi wakati akifafanua baadhi ya majukumu aliyokabidhiwa wizara kwake.

Mbali na hayo Prof. Kabudi alisema mojawapo ya jukumu kubwa alilokabidhiwa na Rais Magufuli ni kuwatumikia Watanzania kwa kusimamia utekelezaji dhabiti wa sheria zilizopitishwa kusimamia rasilimali za nchi.

“Sheria ya kwanza ni ya mamlaka ya nchi kuhusu umiliki maliasili Namba 5 ya mwaka 2017 ambayo inatekeleza kwa vitendo ibara ya tisa na 27 ya Katiba ya Jamhuri ya Tanzania na sheria ya pili ni ile ya mapitio na majadiliano kuhusu masharti hasi kutokana na mikataba ya maliasili za nchi – Namba 6 ya mwaka 2017 ambayo tumekuwa tunaitumia kusimamia majadiliano na makampuni ya madini nchini kwetu,” alisema.

Aidha, kauli hiyo ya Prof. Kabudi kuhusu umuhimu wa kulipa kodi imekuja pia siku chache baada ya Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango kuibuka na kumjibu Makonda kuwa makontena hayo yatapigwa mnada tena na tena.

Mazingira ya Dk. Mpango kutoa kauli hiyo yalitokana Makonda kutoa kauli ya kuwatisha watu watakaonunua makontena hayo ya samani akisema atalaaniwa yeye na vizazi vyake.

Mijadala kuhusu makontena hayo awali ilianza Machi mwaka huu na kutulia kwa muda hadi ilipoibuka tena wiki mbili zilizopita baada ya Mamlaka ya Mapato (TRA), Idara ya Forodha kutangaza kupiga mnada.

Makontena hayo ambayo yanapigwa mnada na kampuni ya udalali ya Yono Auction Mart kwa idhini ya TRA yamenadiwa Jumamosi iliyopita bila mafanikio katika ghala la Dar es Salaam Inland Container Deport (DICD) eneo la bandari Kurasini.

Awamu ya kwanza makontena hayo yalishindwa kupata wateja, sababu kubwa iliyotolewa awamu ya pili na wateja ni kwamba makadirio ya bei yana walakini ukilinganisha na samani zilizoko kwenye makontena hayo.

Kwamba samani hizo hazikupangwa kwa mpangilio na kwamba kama jambo hilo lingetekelezwa vizuri zingetosha kwenye makontena matano tu na si 20.

Agosti 25 mwaka huu Mamlaka ya Mapato (TRA) ilitisha mnada wa makontena kutokana na mmiliki ambaye ni Makonda kushindwa kuyalipia kodi.

Mnada huo haukufikia lengo kutokana na wateja kushindwa kikidhi bei zilizokuwa zimepangwa na TRA, hivyo ikapangwa siku nyingine ya kufanya mnada ambayo ilikuwa Septemba mosi.

Siku moja baada ya kufanyika kwa mnada wa kwanza Makonda akiwa kanisani Wilayani Ngara, alizungumzia suala hilo la mnada wa makontena yake kwa kuwatisha wanunuzi wa samani hizo ambapo alisema mtu atakayenunua atalaaniwa yeye na vizazi vyake.

Hata hivyo kauli hiyo ya Makonda haikuwa ya kwanza kwani Mei mwaka huu alisema TRA na Wizara ya Fedha wanauhujumu Mkoa wa Dar es Salaam, kwamba wakiendelea kuyazuia makontena hayo atawashtaki kwa Rais.

Alisema TRA wanakusanya kodi ambayo inakwenda kujenga shule na samani zikiwemo mbao za kufundishia.

“Sasa umepata mtu wa kukupa mbao za kufundishia zinazotumia umeme, walimu wetu wanateseka na chaki zinaingia puani, mtu analeta madawati, meza za walimu na vifaa vya kufundishia vya zaidi ya Sh bilioni mbili, wewe leo unakuja unamlipisha kodi.

“Hutakiwi kuwa na akili ya darasa la tatu kujua kwamba huu msaada ni kwa walimu waliowafundisha wao na wanaofundisha watoto wao.

“Unatoza kodi inaenda kununua tena meza za walimu na vifaa vya kufundishia. Hayo ni mahesabu gani? Wakiendelea ntaenda kuwashitaki kwa Rais,” alikaririwa Makonda akisema.

Jumatatu wiki iliyopita Waziri Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango alifanya ziara ya kushitukiza katika Bandari ya Dar es Salaam na kutembelea mahali yalikohifadhiwa makontena hayo ya Makonda ambapo alimjibu Makonda kwa kusema makontena hayo yatapigwa mnada hadi mteja atakapopatikana.

“Niliapa kutekeleza sheria za nchi na sheria za kodi. Katika usimamizi wa sheria hizi, Kamishna zisimamie bila kuyumba. Piga mnada mara ya kwanza, ya pili na ya tatu kadiri sheria inavyokuruhusu”.

Hata hivyo, wafuatiliaji wa mambo wanasema huenda Waziri huyo wa Fedha aliamua kuchukua msimamo huo ili mbele ya safari asije kushitakiwa kwa matumizi mabaya ya madaraka kama ilivyowakumba mawaziri wa fedha wa zamani, Basil Mramba na Daniel Yona.

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda

Waziri wa Sheria na Katiba, Profesa Palamagamba Kabudi

Waziri wa Sheria na Katiba, Profesa Palamagamba Kabudi

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.