NI MWANA MALEVYA

Rai - - MBELE -

Usingizi ni aina ya mapumziko kwa kiumbe aliyechoka mwili na akili. Wengine husema kuwa usingizi ni mwana malevya kwa binadamu mwenye shibe yake. Na wapo wasemao kuwa usingizi ni mwana wa uvivu na uzembe katika mwanadamu kujitambua na kuleta mazingatio.

Kwa mnasaba wa tafsiri hizi; usingizi unaweza kuwa mavune ya mwili yanayotokana na shuluba, au ulevi kwa akili unaotokana na shibe; na au uvivu na uzembe wa kuleta mazingatio.

Usingizi kwa aina yoyote iwayo, ni nusu ya kufa. Aliye usingizini hayaoni yapitayo duniani wala hasikii yasemwayo na walio macho. Kuona anayoyaona na kusikia anayoyasikia ni katika ulimwengu wa ndoto.

Naam! Ndani ya ndoto mwanadamu hucheka, hulia, hufurahi na kuhuzunika. Ndani akaiona ndoto mtu huvuna kipato, akajiona yu juu anaelea mawinguni. Na ndani ya ndoto mtu huyabeba matatizo ya dunia mabegani akatamani kufa. Sahibu yangu alipata kuniambia kuwa kuelemewa na usingizi mzito ni nafuu kuliko kuelemewa na usingizi wa kupitiliza.

Maadamu tumeona kuwa usingizi huambatana na ndoto, pengine ni muhimu pia tukaitazama na ndoto. Ndoto au njozi, zipo za kufirika tuwapo usingizini, na nyingine ni matamanio yetu ya baadaye ambayo ni njozi ndani ya fikra tukiwa macho. Hatuna budi kutambua kuwa iwe ndoto ya usingizini au dhamira, namna ya kuiendea tafsiri ya ndoto ni ile ile.

Mosi, mtu lazima aamke kwanza ndipo atanabahi kuwa alipokuwa usingizini aliota ndoto. Pili ili ndoto itimie ni lazima iwekwe katika vitendo.

Waswahili wanao msemo kuwa “usimwamshe aliyelala”. Ukiwauliza kwa nini, wanakuambia utalala wewe. Kwani usingizi unaambukiza? Ah! Maneno ya Waswahili yanazungumzisha mno ubongo. Ila jambo moja sinayo chembe ya ubishi nalo. Jambo gani hilo?

Kumwamsha aliyelala usingizi wa kwelikweli, ni kazi nyepesi kuliko kumwamsha anayejisingizia kulala usingizi. Huyu kila ukimwamsha ndipo anapoongeza kasi na sauti ya kukoroma. Utamtingisha na kumpigia kelele kazi bure. Aliye macho haamshwi.

Unamkuta kijana barobaro mwenye akili timamu na kajaaliwa kiwiliwili kisicho na dosari ya kumzuia kukamata kwa mikono yake na kusimama kwa miguu yake, lakini ndani ya kichwa chake ameusheheni usingizi fofofo. Anatazama kwa macho yake, lakini haoni. Anasikia kwa masikio yake, lakini hazinduki, na akiteleza basi ni ulimi sio mguu.

Amelala usingizi wa pono na hali yu macho. Huyu hata ukimwasha kwa ngoma na njuga, kwake ni wimbo wa kuupepea usingizi mnono.

Ikiwa usingizi huu ni wa mwanao utammwagia maji baridi. Ikiwa usingizi huu ni wa mtu baki, utamwachilia mbali adhalilike na hulka yake. Mtihani unaohitaji ufumbuzi ni pale usingizi huu unapokuwa ni wa mtu aliyebeba dhamana ya ustawi na mustakabali wa wanadamu wenzake.

Kwa mfano, tumuache nahodha analala hadi anaigongesha mashua mwambani, mbao za maliki na mkuku vitawanyike? Hata kidogo! Asiyejua la muhali usiwe na muhali naye.

Waliokubali kwa hiari zao kubeba dhamana ya kuwaongoza wanadamu wenzao, hawana hiari ila kuinua uso, kutazama na kuyaona yanayonyooshewa vidole. Tena hawana hiari, ila kusikiliza na kuzingatia yanayopigiwa kelele.

Namna bora ya kuondosha msuguano baina ya pande mbili ni kuzungumza na kuafikiana. Mkubwa usiringie pembe zako, kwani hapatikani mkubwa pasipokuwepo mdogo. Kalamu ya muungwana inaongeza kuwa hata msuguano baina yako na familia yako, au na wenzako, unahitaji subira na mazungumzo. Ukiamshwa amka.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.