Bunge lifanye mabadiliko ya Katiba

Rai - - MAONI/KATUNI -

Wazo lililotolewa na Jukwaa la Katiba la kupendekeza mabadiliko katika Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya 1977 na Katiba ya Serikali ya Zanzibar (1984), ni jema kwa kuwa ni njia bora ya kujenga demokrasia na kuhakikisha kuendelezwa kwa amani na utulivu.

Hii imetokana na ukweli kwamba Bunge la Katiba ambalo lilihitimisha kazi yake mwaka 2014, lilishindwa kufuata mapendekezo ya msingi yaliyokuwa yamependekezwa na Tume ya Jaji Joseph Sinde Warioba iliyopewa majukumu ya kutafuta maoni ya wananchi kuhusu katiba waitakayo.

Mvutano wa wajumbe wa Bunge la Katiba ulisababisha mfarakano mkubwa na kuundwa kwa Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) ambao uliviunganisha vyama vikuu vya upinzani na hatimaye ikabidi Uchaguzi Mkuu wa mwaka uliofuata (2015) ufanyike kwa kutumia Katiba ya zamani.

Lakini hatuwezi kufanya mabadiliko katika Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pekee, bila kuigusa Katiba ya Zanzibar kwa kuwa kuna vifungu ambavyo vinapingana.

Kwa hiyo, kama mabadiliko hayo yatapelekwa mbele ya Bunge, itabidi pia mapendekezo yapelekwe kwenye Baraza la Wawakishi la Zanzibar.

Mambo kadhaa makubwa pia yamependekezwa —ikiwa ni pamoja na vifungu vya sheria na baadhi ya maeneo ya kanuni kuhusiana na mfumo, usimamizi na uratibu wa uchaguzi.

Jambo lililo muhimu zaidi ni kuundwa kwa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, ambayo itakuwa na muundo tofauti na hii ya sasa.

Inapendekezwa kwamba iwepo Kamisheni itakayoiongoza Tume katika utendaji kazi wake na kwamba patakuwapo na Sekretarieti ya Tume ambayo Mkurugenzi wa Tume ndiye atakuwa mtendaji mkuu.

Pia ni muhimu kuangalia hoja ya kumpunguzia madaraka Rais katika uteuzi wa Makamishna wa Tume. Uteuzi wao ufanywe kwa njia ya usaili na baada ya mchujo, majina yapelekwe Bungeni kujadiliwa na Kamati ya Sheria na Katiba na kisha kupigiwa kura na Bunge.

Vilevile, Mkurugenzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi atokane na majina yaliyopelekwa kwa Rais baada ya Tume ya Uajiri wa Umma kupendekeza majina.

Eneo jingune ambalo inabidi litazamwe upya, ni la mgombea huru katika ngazi zote za uchaguzi, pamoja na nafasi ya urais.

Kimsingi, suala hili lilikwisha tolewa uamuzi katika hatua mbali mbali za Mahakama, ikiwa ni pamoja na Mahakama ya Afrika ambayo iliitaka Tanzania kufanya mabadiliko katika Katiba yake.

Aidha mabadiliko hayo yaweke wazi kwamba vyama vya siasa viruhusiwe kuwa na fungamano (alliances) na kusimamisha mgombea mmoja katika nafasi ya urais, bila kuathiri usajili wa vyama vyao.

Ili damokrasia ionekane kuwapo, tunakubaliana pia na pendekezo la vyama, au vikundi vya watu, kururuhusiwa kuhoji mahakamani matokeo ya kura za urais kama ilivyo katika matokeo udiwani na ubunge.

Aidha, chaguzi zote — za Serikali za Mitaa, Madiwani, Wabunge na Rais, zisimamiwe na taasisi huru — yaani Tume ya Taifa ya Uchaguzi, badala ya Ofisi ya Rais.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.