CCM isidumu kufanya mageuzi irudi kwenye msingi wake

Rai - - MAONI/KATUNI - NA GERARD CHUCHUBA

Katika makala moja wiki moja nyuma nilieleza jinsi madhehebu ya ukristo yalivyozuka baada ya kuzaliwa Kanisa Katoliki la Roma licha ya kuyazuia kwa ukali na ukatili, nikaeleza jinsi Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere alivyoshinikiza vyama vingine vya siasa viruhusiwe ili tutoke kwenye siasa za chama kimoja.

Nilieleza kwamba Mwalimu alifanya hivyo baada ya kuona kuwa CCM ilikuwa imetoka kwenye msingi wake wa kujenga Tanzania ya Ujamaa na kujitegemea yenye siasa isiyoegemea upande wowote magharibi wala mashariki.

Kwa kulizika Azimio la Arusha, CCM ilitudhihirishia kwamba imekuwa madhehebu. Zaidi ya asilimia 80 ya Watanzania tulichelewa kuliona hilo na hivyo tukalikataa pendekezo la kuruhusu uwepo wa vyama wanavyoviita vya upinzani. Ukimwita mtoto jina baya, shetani atalifuatilia liwe kweli, vyama vilivyotakiwa viisimamie na kuikosoa pale Bunge linapopwaya, vikawa vya upinzani kwelikweli vikipinga mema na mabaya ya Serikali!

CCM kwa kuwa madhehebu imesababisha maendeleo ya nchi yawe ya polepole sana. Kwa vipi? Tumepuuza usemi wa wahenga kwamba “Umoja ni nguvu na utengano ni udhaifu”

Baada ya siasa hizo, za wagawe uwatawale, zilizoasisiwa na Warumi “Imperialists” wa kwanza walioitawala uingereza kwa miaka 40 walitumia siasa ya “Divide et impera” waingereza nao wakainakili na waliitumia enzi hizo mpaka enzi tulizonazo.

Tanzania, wote tumeona kwamba imekatwa mapande kadhaa, ushahidi ni usemi kuwa eneo Fulani ni ngome ya Chama Fulani. Watanzania tumegawanyika hivyo mpaka Bungeni! Migawanyiko hii imetupunguzia kasi ya maendeleo! Tunaendelea mbele kwa mambo mengi ni kweli lakini kwa kasi ndogo na kwa nguvu ya ziada sana.

Migawanyiko hii imesababisha ufisadi. Siasa za migawanyiko zinafanyisha wenye madaraka wasiwe na hakika ya kesho yao na hivyo wakawa wanachukua chao mapema! Kwa tabia hiyo fedha ya miradi ya maendeleo ikawa haikamiliki kwa wakati na mingine inakwama kabisa. Watu wamechukua chao mapema!

Kwa kupotoshwa kwa makusudi tukaendelea kutoa elimu ya kulenga kuajiriwa. Mtu akimaliza kidato cha nne akakosa kwa kwenda, watu wanamshangaa amekosa hata Ualimu! Hawasemi hata upolisi!

Mwalimu akaonekana ni mtu asiye na nguvu katika taifa hili. Bahati mbaya sana, mwalimu naye akajiona yu hivyo jamii inavyomwona.

Baba wa Taifa aliuona upungufu huu na akaukemea,

Akihutubia katika tukio fulani hapo tulipozoea kupaita Kingulunyembe Chuo Cha Ualimu 27 Agosti, 1966 baada ya kuzungumza kwa kifupi juu ya shughuli husika, alisema “let me now turn to a different subject. For what I really want to talk about today is the power which teachers have…..”

Kwa tafsiri yangu “sasa nitazungumzia suala tofauti hivi leo. Nalo ni nguvu ambayo walimu wanayo”

Aliendelea, akakemea makosa yaliyokuwa yanafanyika na nionavyo yanafanyika hata leo mwaka 2018 ya kumwona mwalimu si mtu wa muhimu na wa kutiliwa maanani sana.

Mwalimu Nyerere akihitimisha kwa kusema “for teachers can make or ruin our society’! kwa maana walimu wanaweza kuijenga au kuiharibu jamii yetu’! hivi ndivyo tulivyofanywa na tunaendelea kufanya. Eti walimu wanawapa mimba wanafunzi wao! (Freedom and Socialism uk.223).

Tulipotoshwa kwamba watoto wanaomaliza Darasa la Saba na kufaulu vizuri somo la Hisabati wapelekwe Shule za Ufundi kama vile Ifunda na wasifundishwe Historian a Elimu viumbe. Tukapokea ushauri huo na kutarajia watakuwa chachu ya kuanzisha viwana. Hiyo ilikuwa ni mwanzoni mwa miaka ya themanini.

Waliotupotosha wanajua mwanafunzi anayeimudu hisabati katika ngazi hiyo ana

akili sana. Hivyo ukimfundisha historia atakuwa mgumu kudanganywa na kupotoshwa kwa kuwa anakujua atokako na hivyo anaweza kujua lipi la kwanza na lipi ni la pili kwake na kwa nchi yake pia.

Ukilibishia hili kamuulize Profesa Paramagamba Kabudi, sasa mheshimiwa waziri aliona umuhimu gani, kuanzisha somo la historia ya sheria na wakubwa wakamfuata. Kwangu mimi historia ni somo muhimu kwa watu wanaotafuta maendeleo yanayolingana na hali waliyo nayo.

Kati ya vitu vinavyochelewesha maendeleo ya watanzania ni pamoja na ushamba wa waliokabidhiwa wadaraka ya kutuongoza. Walikurupukia majumba, magari na maisha ya ufahari wakajitenga na wanaowaongoza wakasahau kuwa kuvuka daraja kabla ya kulifikia huleta ajali.

Kutokusimamia kilimo kwa nguvu zote ili kithibitishe kuwa kiuti wa mgongo wa maendeleo ya nchi kama tulivyo na tunavyokiri kwa kauli bila matendo mwafaka.

Kujali shibe yako kati ya wenye njaa nao ni ushamba na shibe yako ni masimango yako.

CCM ikiacha kung’ang’ana na mageuzi, kuvua gamba itaendelea kuwa madhehebu ya siasa na kuzalisha madhehebu zaidi nchini.

Kama viongozi wa CCM wanaitakia mema Tanzania, wairejeshe misingi kama ilivyowekwa katika Azimio la Arusha! Hili likifanyika nchi itakuwa na umoja na kwa kuwa umoja ni nguvu, sera nzuri tulizonazo zitakwenda zitazaa matunda.

Bunge letu litatumia muda wake kujadili maendeleo ya nchi kwa akili iliyotulia bila kugeukageuka huku kwa kuhofia kujikwaa katika kauli na kuzua zogo bungeni zitakazomlazimisha Spika kuwatoa nje baadhi yao jambo la aibu kwa atolewaye na pia kwa waliomchagua!

Zingatia, CCM ikiurejesha msingi wake sahihi, vyama vinavyoitwa vya upinzani vitadhoofika na vingi vitajifia – watapinga nini kama nchi ina maendeleo na ushamba uletao ufisadi na rushwa vimetoweka?

Kwa wasifu wa Katibu Mkuu wa CCM aliyepo kama ulivyotolewa na ndugu Jimmy Charles katika RAI 28 – Julai 4- 2018, matumaini yanaonekana kwa mbali.

Wasifu wa Dk. Bashiru Ally ukijumuishwa na kazi zinazofanyika Tanzania hivi sasa bila kelele na maazimio, binafsi naona mwanga mbele.

Aidha, nimetiwa moyo na mawaidha yaliyotolewa na kiongozi wa waislamu katika kilele cha Iddi iliyopita ametuonya tusiwe wepesi kukurupuka na kuunga mkono mawazo ya baadhi ya viongozi yanayotolewa huku yakiwa ni mawazo ya mtu ambayo hayawezi kuthibitishwa kwa utafiti yakinifu. Hongera sana mtoa onyo hilo. Tunayasubiri mawaidha kama hayo kutoka kwa viongozi wa dini zingine.

Kwa kuhitimisha,CCM imeyachelewesha maendeleo ya nchi au imeyafanya yaje polepole mno. Imezalisha madhehebu ya siasa zaidi ya ishirini. Aidha elimu potofu, kwa makusudi nayo imetucheleweshea.

Mwisho ni ushamba wa wengi wa viongozi wetu ambao walidhani kujilimbikizia mali kunaleta heshima wakawa mafisadi na wala rushwa. CCM iongoze njia irudi kwenye msingi nchi ipone.

0768-462511

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.