Messi hakustahili kinyanganyiro Mchezaji Bora Fifa 2018?

Rai - - MBELE -

BADO kuna mjadala mzito juu ya nyota Lionel Messi kutoingia ‘top three’ ya wanasoka wanaoiwania tuzo ya Mchezaji Bora wa Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa) kwa mwaka huu.

BADO kuna mjadala mzito juu ya nyota Lionel Messi kutoingia ‘top three’

ya wanasoka wanaoiwania tuzo ya Mchezaji Bora wa Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa) kwa mwaka huu.

Kwa mujibu wa Fifa, ni Cristiano Ronaldo, Luka Modric na Mohamed ‘Moh’ Salah pekee waliobaki kusubiri hafla ya utoaji tuzo hiyo itakayofanyika Septemba 24, mwaka huu.

Ifahamike kuwa hii inakuwa mara ya kwanza kwa Messi, raia wa Argentina mwenye umri wa miaka 31, kuikosa tatu bora ya kinyang’anyiro hicho tangu mwaka 2007.

Hivyo, kukosekana kwake kumezua taharuki kubwa si tu kwa mashabiki wa kandanda, bali hata baadhi ya wachezaji, makocha, na wachambuzi wa kandanda barani Ulaya.

Madai yao ni kwamba takwimu za Messi msimu uliopita zilitosha kabisa kumpa nafasi ya kuingia tatu bora na hata kuibeba tuzo hiyo mbele ya mchezaji yeyote ambaye angeshindana naye.

Kama kigezo ni fainali za Kombe la Dunia, ni kweli Messi alivurunda. Akiwa ndiye nahodha, Argentina yake iliishia hatua ya mtoano (16 bora).

Lakini je, mbona Salah ameingia tatu bora wakati Misri yake haikuwa na maajabu yoyote kule Urusi? Mafarao, wawakilishi wa Afrika waliokuwa wakipewa nafasi kubwa, waliishia 32 bora (hatua ya makundi).

Tofauti ya Salah na Messi katika mashindano hayo ni kwamba, ‘Mwarabu’ huyo alifunga mabao mawili hadi timu yake ilipokuwa timu ya kwanza kuiacha ardhi ya Urusi. Lakini sasa, tuzo kama

hii hutokana na mchango wa mchezaji kwa timu yake. Kwa maana nyingine, si tu kiwango cha mchezaji, bali kiliiwezesha vipi timu yake kufikia mafanikio fulani?

Hapo ndipo unapobaini kuwa Misri haikufaidika chochote kutokanana mabao mawili ya Salah? Kwamba, hakuwa na tofauti na Messi, yaani wote walikwenda kutembea.

Ikumbukwe kwamba Hristo Stoichkov aliponyakua Ballon d’Or mwaka 1994, ilitokana na mabao yake kuiwezesha Bulgaria kushika nafasi ya tatu Kombe la Dunia.

Ukiacha hilo, Messi aliumaliza msimu uliopita akiwa amefunga mabao 34 ya Ligi Kuu ya Hispania ‘La Liga’, akiwa ndiye mchezaji aliyeziona nyavu mara nyingi katika ligi zote kubwa tano barani Ulaya (England, La Liga, Bundesliga, Serie A na Ligue 1).

Mbele ya Ronaldo na Salah waliobaki top three ya Fifa, jamaa akaibeba tuzo ya Mfungaji Bora wa Ulaya, tena ikiwa nimara yake ya tano. Labda Modric hausiki katika hili kwa kuwa kazi yake kubwa uwanjani ni kutengeneza nafasi za wengine kufunga.

Hata hivyo, bado Messi alimzidi hata Modric katika huduma ya pasi za mabao ‘asisti’. Februari, mwaka huu, katika mchezo wa Barcelona yake dhidi ya CD Huesca, aliweka rekodi ya kuwa mchezaji wa kwanza La Liga kufikisha asisti 150 katika karne hii ya 21.

Akamgaragaza pia katika kutengeneza nafasi za mabao, kazi ambayo Modric alitakiwa kuwa ndiye kinara. Messi alikuwa amefanya hivyo mara 121, akimzidi Modric aliyekuwa na 60.

Wakati akimaliza msimu akiwa na asisti 18 (mechi za michuano yote), Modric alikwamia nane, sawa na Ronaldo, huku Salah akiwa na 14. Ukitazama takwimu zingine mbali ya hizo za mabao ya kufunga, kutengeneza nafasi, na kutoa asisti, pia msimu uliopita ulikuwa mzuri kwa Messi. Inashangaza kuona akishindwa kuingia katika kinyang’anyiro hicho cha Mchezaji Bora wa Fifa.

Mtandao wa OmniSport ambao ni maarufu kwa ukusanyaji takwimu, umeonesha kuwa aliumaliza msimu uliopita akiwa amepiga mashuti 192 na ndiye aliyekuwa kinara wa kukokota mpira (174) katika ligi zote tano kubwa barani Ulaya.

Mchango wake huo uliiwezesha Barca kuchukua taji lake la 25 la Liga na ilikaribia kuweka rekodi ya kuwa mabingwa bila kufungwa lakini Levante wakatibua katika mechi ya 37, mchezo ambao hata hivyo Messi hakucheza.

Je, kwa takwimu hizo Messi hakustahili kuwamo katika orodha hiyo ya wachezaji watatu waliobaki kuiwania tuzo ya Mchezaji Bora wa Fifa?

Messi

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.