YAWEZA KUWA MKASA NDANI YA NEEMA

Rai - - MBELE - MUDHIHIR MUDHIHIR

Shari inaweza ikawa mkasa unaokumba mtu ikamtia hofu, huzuni, maumivu na machungu. Mtu anaweza akaatilika kwa shari ambayo kwa hiari yake ameitafuta na kuifuata iliko, na watu wakasema mwenye kujipiga kofi hapaswi kulia. Na shari inaweza ikawa ni ajali inayomfuata mtu na wenye utu wakamfariji kuwa ajali haina kinga. Lakini kwa ujumla wake shari haina heri japo tunasema kuwa tumbo la shari huzaa heri.

Kwa watu wenye ubinadamu ndani ya nafsi zao daima huwaombea wenzao heri. Huwa tunasikia watu wakisema kuwa adui yako muombee njaa bali laiti tungeleta mazingatio kwamba mwenye njaa hana ubinadamu wala muhali, tusingemuombea njaa yeyote. Adui mwenye shibe ni afadhali kuliko adui mwenye njaa. Nyakati nyingine hata ndugu wa damu na rafiki wenye njaa huwa ni mtihani mgumu kuliko mtihani wa adui.

Kwa kila mwanadamu mwenye mazingatio anapaswa kufanya kila awezalo kujiepushia shari yeye mwenyewe na kumwepushia mja mwenzake. Ama shari ya kuikusudia humwachia mtu majuto. Kuna shari inayomfika mtu kwa uzembe na ndipo wahenga wanapotuzindua kuwa asiye nadhari ng’ombe. Na wapo watu ambao kwao shari ni hulka, hawa nao ni watu. Kwani hujapata kuwasikia watu wakisema kuwa kuna watu na viatu!

Wapo wasiojua kusema na nafasi zao wanapokwaruzwa hata na jambo dogo tu. Hawa ndio akina “sikubali, kwa nini, leo atanitambua, na atatia akili iwapo maharage ni mboga au futari.” Hawa ni wale wenye kuamini kuwa dawa ya moto ni moto na kwamba eti amani haipatikani ila kwa ncha ya upanga. Ikiwa ipo hasara basi ni mtu kushindwa kutabiri hatima ya neno au tendo lake.

Kilichomo ndani ya miliki yako kinaweza kuwa ni fursa ya kukuletea manufaa au ngao ya kukulinda dhidi ya shari, au sumu ya kukutumbukiza kwenye dimbwi la shari yenye kukuangamiza. Utaangukia wapi baina ya utatu huu kutategemea nadhari ya kupima matokeo ya utalolikusudia kulinena au kulitenda. Mtu huvuna anachopanda.

Husemwa kuwa unachokimiliki ndio rasilimali yako na ndio neema yako. Matumizi ya neema hiyo ndio yatakayokuletea tamu au chungu. Unaweza kutumia pumzi zako kupuliza na kuni zikashika moto. Unaweza kupuliza ukauzima moto wa mshumaa na kibatari. Na unaweza kupuliza ili kuyapoza maumivu. Naam! Kumbe kupuliza kunaweza kuwasha na kuzima moto, na kunaweza kupoza maumivu.

Miongoni mwa neema tulizokirimiwa wanadamu ni milango mitano ya ufahamu ambayo ni macho, pua, kinywa, masikio na ngozi. Neema hii inatuwezesha kuona, kunusa, kuzungumza, kusikia na kuhisi ubaridi na ujoto. Lakini kijicho, umbeya na usengenyi ni shari zinazotokana na neema hizi tulizokirimiwa na Mwenyezi Mungu. Wapo waliokirimiwa utajiri ambao badala ya kuwashika mkono wasiojiweza huitumia neema hiyo kufisidi ndoa za jirani zao. Wapo waliokirimiwa kuwaongoza wenzao lakini badala ya kuwasaidia waliopo chini yao, wanawanywa jasho, damu na kuwakanyaga mabegani. Na wapo waliokirimiwa elimu ambayo imewaondosha kwenye kiwi ya ujinga na kuwatumbukiza kwenye dimbwi la upumbavu.

Tumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujaalia fahamu ambayo ni chungio la kuchuja nuru na giza, heri na shari, na utu na unyama. Fahamu ni kama ardhi yenye rutuba tele inayoweza kustawisha mazao na magugu. Hiari na mukhtari wa mbegu gani ya kupandwa ni kwa mwenye fahamu yake. Ukipanda heri utavuna raha na amani, na ukipanda shari utavuna karaha na majuto.

Kalamu ya muungwana inatukumbusha tu kuwa ndani ya neema zimo shari. Tukimshukuru Mwenyezi Mungu na kusubiri, neema zetu ni heri kwetu. Na tukitakabali kwa vipato vyetu, neema zetu ni shari kwetu.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.