WAKO KATIKA NJIA SAHIHI

Rai - - MBELE - JIMMY CHARLES

UKIYASIKILIZA maelezo na malalamiko ya baadhi ya Watanzania wanaotumia visimbuzi vya kulipia (content by subscription), juu ya hatua ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kuzitaka baadhi ya kampuni kutorusha matangazo ya chaneli za ndani kwa kile kinachotajwa kuwa ni ukiukwaji wa leseni zao, unaweza kuamini bila chembe ya shaka kuwa mamlaka hayo yana nia ovu na wananchi ambao ndio inawatumikia.

Sakata hilo ambalo msingi wake ni utekelezaji wa matakwa ya sheria, limekuwa likichukua sura mpya kila uchwao.

Miongoni mwa sura hizo ni kuwapo kwa tishio la baadhi ya kampuni eti, kuziondoa chaneli zinazopaswa kuoneshwa bure kwa hoja kuwa hawalipi.

Umoja wa wamiliki wa visimbuzi ndio ulitio tishio hilo kwa kutoa siku 30, wakisema kuwa endapo wamiliki wa chaneli hizo hawataanza kulipia gharama kwa ajili ya kurusha matangazo kupitia mitambo yao, wataziondoa.

Kauli hiyo ilitolewa wakati wamiliki wa vituo vya televisheni za ndani wakitafuta njia mbadala ya kurusha matangazo yao.

Umoja huo unaoundwa na visimbuzi vya Startimes, Ting na Continental ulisema umefikia uamuzi huo baada ya kutolipwa kwa zaidi ya miaka minane na chaneli 34 zilizosajiliwa kutumia mitambo yao.

Mwenyekiti wa wamiliki hao, Dk Vernon Fernandis alisema baada ya kushinda zabuni, sheria iliwataka kujenga mitambo ili wamiliki wa chaneli waitumie kurusha matangazo na kuwawekea kiwango elekezi cha gharama za kuwatoza kwa mwezi. “Kila kituo kinachotumia mitambo yetu kinatakiwa kulipa Sh2.4 milioni kwa mwezi kwa kila mkoa ambao matangazo yao yatafika, lakini hatujalipwa tangu mwaka 2010 jambo ambalo linatupa hasara kubwa,” alisema Dk Fernandis.

Alisema walitumia zaidi ya Dola300 milioni za Marekani kuwekeza katika ujenzi wa minara 47 wakitarajia faida kutokana na malipo kutoka kwa wamiliki hao, lakini imekuwa kinyume cha matarajio yao.

Chaneli zinazobebwa na Ting, Startimes na Continental zinapaswa kulipa huduma ya kubebwa kwao, hilo halina ubishi na niwaombe hawa waungwana wasisake visingizio kwenye hili.

Haya na mengine mengi yametoa msukuma wa baadhi ya wananchi kujenga imani haba na TCRA, jambo ambalo si jema. Kwenye eneo hili mamlaka haipaswi kulaumiwa.

Hata hivyo kwa fikra zangu naamini imani hiyo inachagizwa na namna ya walalamikaji walio wengi kutokuwa na ufahamu wa kutosha juu ya uamuzi huo wa TCRA,.

Binafsi sikupata kuwa miongoni mwa walalamikaji wala waathirika wa uamuzi huo kwa sababu kadha wa kadha, ambazo itachukua kurasa kadhaa kuzieleza kwenye safu hii. Lakini pia kwa sasa si wakati sahihi wa kufanya hivyo.

Hata hivyo kwa kuwa ninao ndugu, jamaa na marafiki walioathirika kwa namna moja ama nyingine sikujiweka nyuma ya sakata hili ambalo wengi wa walalamikaji wanainyooshea kidole TCRA. Huenda walikuwa sahihi kwa sababu hawakujua dhamira njema iliyonayo mamlaka hayo.

Kwa kuwa uamuzi umeshachukuliwa na hatua kadha wa kadha zimeshaanza kutekelezwa, kamwe siioni haja ya kufanya rejea ya sakata hili, badala yake nimewiwa nigawane na wenzangu ufahamu nilioupata juu ya uamuzi huu wa TCRA, ambao kwangu niliouna na bado nauona ni sahihi.

Kwanini sahihi? Ni sahihi kwa sababu unabeba maslahi mapana ya nchi, lakini pia unayo dhamira kuu ya kumlinda mlaji (mtumiaji) bila kujali kipato chake.

Ukweli ni kwamba kila biashara inazo sheria, kanuni na taratibu zake na ukikiuka ni lazima ushughulikiwe, hivyo ndivyo ilivyo kwenye biashara hii ya urushaji wa matangazo.

Tunaweza kudhani na hata kujiaminisha kuwa TCRA wamechelewa ama wamekurupuka kuchukua uamuzi huu. La hasha!

Ukweli ni huu, Mkurugenzi Mkuu wa TCRA, Mhandisi James Kilaba, ameweka wazi kuwa kabla ya kufikia uamuzi huu wa sasa, muda mfupi baada ya kujiondoa analogi na kuhamia digitali, zipo kampuni zenye leseni ya kutangaza kwa kulipia zilichukua chaneli zinazopaswa kuoneshwa bure.

Baada ya kufanya hivyo mamlaka iliziandikia barua kampuni zinazomiliki visimbuzi vya kulipia na kuzitaka iziondoe chaneli hizo, ama ibadilishe leseni zake kutoka za kulipia na kuwa za bure (free to air). Yote haya yamefanyika kwa utaratibu stahiki na wahusika hawakuyatekeleza kwa kipindi chote hicho. Watanzania tunapaswa kujua kuwa kwenye maudhui ya utangazaji wa Luninga yapo mambo mawili muhimu.

Mosinimaudhuiyanayotazamwa bila kulipiwa (free to air)na pili ni maudhui yanayotazamwa baada ya kulipia (content by subscription).

Maeneo yote mawili haya yanalindwa na leseni tofauti, kwa maana kila maudhui kati ya hayo mawili yana leseni na sifa zake na haziingiliani hata kidogo na mwombaji halazimishwi achukue leseni ipi kati ya hizo mbili ni hiyari yake.

Maudhui ya FTA yanabeba sifa ya kumhabarisha mwananchi matukio yanayohusu jamii inayomzunguka ikiwamo taarifa za habari, vipindi vya watoto, mijadala inayohusisha wananchi ikibeba mada za maendeleo, taarifa na maelekezo mbalimbali kutokja kwa viongozi.

Hali ni tofauti kwa visimbuzi vya kulipia, huku maudhui yake yamelenga kufanya biashara zaidi kwa njia ya malipo kutoka kwa mtazamaji.

Eneo hili hubeba tamthilia ambazo ni mpya sokoni, filamu mpya sokoni kwa ajili ya watu wazima, vipindi vyenye hatimiliki na michezo mbalimbali ya kitaifa na kimataifa.

Pamoja na utofauti wa leseni, lakini pia yapo maeneo muhimu na nyeti ambayo Watanzania wote tunapaswa kukubaliana na uamuzi wa TCRA. Endapo TCRA itaendelea kuacha chaneli za ndani kurushwa kwenye visimbuzi vya kulipia ni wazi haki ya kupata taarifa kwa Watanzania walio wengi itapotea pale tu atakapokosa uwezo wa kulipia tozo ya mwezi (subscription fee).

Wigo na mtandao wa ufikishaji wa huduma za utangazaji kwenye maeneo mengi nchini utapungua, uwezekano wa matangazo ya biashara kutowafikia wananchi wengi ni mkubwa, lakini kubwa zaidi ni miundombinu ya visimbuzi vya kulipia imejengwa nje ya nchi, hali inayozalisha ugumu katika kuidhibiti, tofauti na ile ya FTA.

Kwa fikra zangu naamini TCRA wako katika njia sahihi, tukiliacha suala la urushaji wa matangazo ya chaneli za ndani kuhodhiwa kiholela, upo uwezekano mkubwa wa huko tuendako kikundi kidogo cha watu kikawaondolewa watu wasio na uwezo wa kulipia ving’amuzi haki ya kupata habari zinazohusu nchi yao.

Pamoja na utofauti wa leseni, lakini pia yapo maeneo muhimu na nyeti ambayo Watanzania wote tunapaswa kukubaliana na uamuzi wa TCRA. Endapo TCRA itaendelea kuacha chaneli za ndani kurushwa kwenye visimbuzi vya kulipia ni wazi haki ya kupata taarifa kwa Watanzania walio wengi itapotea pale tu atakapokosa uwezo wa kulipia tozo ya mwezi (subscription fee).

Mkurugenzi Mkuu wa TCRA, Mhandisi James Kilaba

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.