Mawaziri wajiepushe kutoa ahadi kwa wapigakura

Rai - - MAONI/KATUNI -

KUNA kampeni zinaendelea katika majimbo matatu ya uchaguzi — Jimbo la Ukonga katika Mkoa wa Dar es Salaam, Korogwe Vijijini, Mkoa wa Tanga na Monduli Mkoa katika Mloa wa Arusha. Ukiondoa Jimbo la Korogwe ambako Mbunge wake, Stephen Ngonyani alifariki dunia, majimbo mengine mawaili, Wabunge wake waliokuwa chama cha upinzani cha Chadema walijiuzule na kujiunga na Chama cha Mapinduzi (CCM).

Chama tawala kimewarudisha Mwita Waitara kugombea jimbo lilele la Ukonga na Julius Kalanga akarejeshwa kugombea tena Jimbo la Monduli. Kama CCM wameona inafaa kuwarejeshea wapiga kura watu waliowachagua na halafu wakaasi ni vyema, hilo tunawaachia wakazi wa Ukonga na Monduli kuamua katika uchaguzi mdogo wa tarehe 16, mwezi huu.

Lakini katika majimbo ya Monduli na Ukonga, vigogo wa CCM kwa maana ya mawaziri waliotumwa kuwapigia kampeni wagombea wao, wametoa ahadi mbali mbali kwamba Serikali itajikita kwenye kutatua kero za wananchi. Sisi tunajiuliza- hivi Serikali haiwezi kutatua matatizo yanayowakabili wananchi mpaka wawakilishi wao wawe wanachama wa CCM!

CCM kwanza ndicho chama kikongwe nchini — kilikuwapo kabala ya vyama vingine kuanzishwa — na kwa kuwa kilikuwa chama pekee, ndicho kilijenga mustakabali wa nchi — amani na utulivu, umoja na mshikamano, hakikupaswa, na hakipaswi kuwa chama cha kuwagawa wananchi.

Kauli iliyotolewa na Naibu Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Jumaa Aweso, kule Monduli kwamba Serikali itatoa Tsh. 1.2 bilioni kutatua kero ya maji katika mji wa Monduli, na hivyo wananchi wamchague mgombea wa CCM, Julius Kalanga, ina ukakasi — ina maana wasipomchagua hawatapata maji!

Tunajiuliza hivyo kwa sababu inaonekana Serikali hii ya CCM ni ya kibaguzi — inawabagua wananchi wasio na vyama na wale wenye vyama vingine — kwamba hawatapata huduma muhimu kama maji kwa sababu wawakilishi waliowachagua sio wana-CCM. Uko wapi umoja na mshikamano kama watawala wanafanya ubaguzi wa wazi wazi?

Maneno kama hayo yaemesemwa pia na mawaziri kwenye kampeni za Ukonga — kwamba kwa kuwa Waitara sasa amejiunga na CCM, na wakimchagua, atamaliza kero za wana Ukonga! Ni kauli za kuwatega wapiga kura, ni kama wanalazimishwa kumchagua mtu ambaye huenda hawamtaki.

Kwa kuweka kumbukumbu sawa, mwaka 1994 Azim Premji (marehemu) aliyekuwa Mbunge wa Kigoma Mjini kwa tiketi ya CCM, alivuliwa Ubunge na Mahakama Kuu, kwa sababu kwenye kampeni ya kugombea ubunge katika uchaguzi mdogo wa Jibo la Kigoma Mjini mawaziri walitoa ahadi kujenga barabara kiwango cha lami.

Katika uchaguzi mdogo wa Igunga wa mwaka 2011 ambapo CCM ilimsimaisha Dalali Kafumu Waziri wa Ujenzi wakati huo aliahidi kujenga daraja kama mgombea atachaguliwa. Mahakama Kuu ilimvua ubunge kwa kigezo cha kuwa ahadi ya kujenge daraja ni sawa na hongo kwa wapigakura wa Igunga, ingawaje Mahakama ya Rufaa, haikukubaliana na uamuzi na ikamrejeshea ubunge.

Kifupi ni kwamba, viongozi wenye dhamana, wajiepushe na kauli tata ambazo zinaashiria kwamba wananchi wanabaguliwa kwa sababu ya kumkataa mgombea wa CCM. Isitoshe, kama hali hii ya kibaguzi itaendelea, CCM wanajijengea anguko.

Wanachama wa CCM na vyama vingine vya upinzani kwa pamoja, hawawazidi uwingi wananchi ambao hawana vyama. Kwa hiyo, kuwanyima wanachi huduma muhimu kwa sababu za kisiasa, kunajenga chuki mioyoni mwa wapiga kura — wananchi waachwe watimize haki yao ya Kikatiba ya kumchagua kiongozi wanayemtaka.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.