Siasa safi na maendeleo huharibiwa na uongozi mbovu

Rai - - MAONI/KATUNI - HILAL K. SUED

Miaka nane iliyopita, akitoa hotuba baada ya kutangazwa kwa matokeo ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2010 katika Ukumbi wa Karimjee, Rais mteule (wakati huo) Jakaya Kikwete alionyesha kustushwa na ushindi mdogo alioupata – wa asilimia 62.8

Miaka nane iliyopita, akitoa hotuba baada ya kutangazwa kwa matokeo ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2010 katika Ukumbi wa Karimjee, Rais mteule (wakati huo) Jakaya Kikwete alionyesha kustushwa na ushindi mdogo alioupata – wa asilimia 62.8 – ukilinganisha na ushindi wake wa miaka mitano iliyotangulia (2005) wa asilimia 84.

Alisema: “Kuna changamoto (matatizo) yaliyojitokeza ambayo yataifanya CCM kukaa chini na kutafakari ili kutafuta ufumbuzi wake… kutafuta nguvu mpya katika chaguzi zijazo...” Kauli kama hiyo aliirudia katika hotuba yake baada ya kuapishwa siku tano baadaye.

Pamoja na ujasiri wake aliounyesha katika kujaribu kusema ukweli kuhusu matokeo, Kikwete alishindwa kukiri kinagaubaga kitu kimoja – kwamba vyama vya upinzani alivyowahi kuviita “vyama vya msimu” navyo vilikuwa na uwezo wa kutoa dhoruba kali kwa chama kilichokuwa madarakani kwa miaka 50.

Kwa upande wa CCM – kukosekana – katika uchaguzi ule (na ule uliofuatia wa 2015) – kile ambacho hupendelewa kuitwa “ushindi wa kishindo” kuliibua, kwa mara ya kwanza, kigugumizi kikubwa miongoni mwa makada na viongozi wa juu wa chama hicho katika kutamka “Ushindi wa kishindo.”

Lakini uwe wa halali, mnono, wa mizengwe, wsa goli lka mkono au wa kupora, ushindi ni ushindi. Haya ni maneno ya kishabiki tu, na mashabiki wa vilabu vya mpira wanalifahamu hilo vizuri, kwani baada ya mechi watauzungumzia sana ushindi katika vijiwe vyao, lakini hatimaye husahau yote -- hata iwapo kulikuwapo mabao ya mkono ya wazi.

Katika chaguzi za siasa za kidemokrasia, ushindi wa aina nyingine yoyote mbali na ule wa halali na wa haki una athari zake kwa amani na utulivu wa nchi husika – na hasa hali ikiwa inarudiwa rudiwa miaka nenda miaka rudi. Hakuna haja ya kutoa mifano – iko tele katika Bara letu la Afrika.

Kama nilivyogusia hapo juu katika uchaguzi wa 2015 ushindi wa CCM ulikumbwa na dhoruba kali ingine, tena zaidi, hali iliyoonyesha kwenda tofauti na kauli ya Kikwete ya 2015, chama chake kamwe hakikukaa chini na kutafakari kile alichokiita “kutafuta ufumbuzi wake… kutafuta nguvu mpya katika chaguzi zijazo….” Katika uchaguzi huo mgombea wa chama chake, John Magufuli alipata asililia 58.4 ya kura zote, ikiwa chini ya ile asilimia 62.8 aliyopata Kikwete mwaka 2010.

Hii inaonyesha kitu kimoja tu – kwamba chama hicho kimekuwa kinatatizwa na suala la uongozi na si kitu kingine kama vile sera au ilani zake. Na hali ya namna hiyo imekuwa ikijiingiza katika safu za juu za serikali yake pia.

Na ndiyo maana hadi leo hii Rais Magufuli amekuwa akilia na viongozi wa serikali katika ngazi mbali mbali – kama vile mawaziri, wakuu wa mikoa, wakuu wa wilaya, wakurugenzi wa halmashauri n.k. na kila mara amekuwa akiwabadilisha kutokana na utendaji kazi wao usioridhisha.

Mwanzoni tu baada ya uhuru wetu, katika hotuba na maandiko yake kuhusu masuala ya maendeleo, baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere alikuwa akisema maendeleo yanahitaji vitu vinne tu vya msingi- ardhi, watu, siasa safi na uongozi bora, na kuongeza kwamba kitu ambacho alikiona kilikuwa kinakosekana ni kile cha mwisho – uongozi bora.

Na ndiyo maana maendeleo ya kweli yamekuwa yakiipiga chenga nchi hii pamoja na kujaliwa ardhi nzuri yenye rutuba; huku chini ya ardhi hiyo na juu yake kuna mali asili kem kem, na mamilioni ya watu kama ‘nguvu-kazi’ iliyosheheni.

Na hata siasa zinazoendesha nchi hii ni safi pia, kama zinavoainishwa katika katiba ya nchi, na za vyama vyote kwani hazina vipengele vya kibaguzi na zote zinataja uzingatiaji wa haki za msingi za raia wake. Lakini yote haya ni katika nadharia tu kwani kiuhalisia viongozi husika wamekuwa wakikiuka misingi ya katiba, sheria na kanuni.

J. P. Morgan, bilionea mkubwa wa Marekani aliyeishi mwishoni mwa karne ya 19 aliwahi kunena: “Kila mtu huwa anazo sababu mbili za kile anachokitenda – sababu nzuri na ile iliyo halisi.” Kwa wanasiasa wengi nukuu hii inawahusu kwa kiwango kikubwa na ndiyo kipimo cha unafiki wa wengi wao na ni kielezo cha ufisadi wao.

Kwa mfano kiongozi katika utawala anaweza kuanzisha mradi kabambe wa maendeleo na kupigiwa debe kuwa ni wa nia njema na kweli kimuonekano ni wa nia njema – lakini utakuta sababu halisi ni kwa wachache kufaidika mabilioni kifisadi. Ipo mifano ya hali hiyo hapa nchini mwetu – mfano mkubwa ni ule wa miradi yote ya ufuaji umeme wa aina ya IPTL.

Aidha takriban nchi nyingi Barani Afrika hutatizwa na suala la uongozi, na si vitu vingine, na ndiyo maana maendeleo yake yamekuwa duni. Miaka 38 ya utawala wa Robert Mugabe nchini Zimbabwe haukuleta tija yoyote kiuchumi kwa wananchi – kwani hata sarafu yake (Zimdollar) iliathirika hadi mwishoni wananchi walikuwa wanaikwepa.

Kuna wanaosema sasa hivi kwamba ni vigumu kwa kiongozi wa sasa Emerson Mnangagwa kubadilisha mambo, hasa ikitiliwa maanani kwamba yeye mwenyewe kwa muda mrefu alihusika katika utawala wa Mugabe katika kuangamiza uchumi wake.

Mugabe alikuwa anaendeshwa kwa kusaka “kiki” aliyoamini kuipata kupitia suala la kuwanyang’anya Wazungu mashamba yao. Mnangagwa atapata tabu sana kubadili mambo kwani itabidi asiwaonee haya wenza wake katika uongozi ambao wengi ni wale wale aliokuwa nao enzi za Mugabe.

Wakati haikuwa chama chake, chama tawala cha ZANU-PF, bali ni nguvu ya jeshi la nchi hiyo ndiyo hatimaye iliyomuondoa Mugabe madarakani, kule Afrika ya Kusini ni chama tawala cha ANC, kupitia mkutano wake mkuu ndicho hatimaye kilimuondoa Jacob Zuma madarakani. Na hiyo ilikuja baada ya mara kadha chama hicho, kupitia wingi wake Bungeni kushindwa kumuondoa kila mara kura ilipoletwa Bungeni na upinzani kufanya hivyo.

Bunge lilishindwa kwa sababu ya ushabiki wa kivyama huku Wabunge wengi wa serikali wakihofu kupoteza masilahi mbali mbali waliokuwa wakifaidika

Na hata siasa zinazoendesha nchi hii ni safi pia, kama zinavoainishwa katika katiba ya nchi, na za vyama vyote kwani hazina vipengele vya kibaguzi na zote zinataja uzingatiaji wa haki za msingi za raia wake.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.