Ubabe wa Trump wahamia kwa majaji ICC

»Atishia kuwafungulia mashitaka

Rai - - MAONI/KATUNI - NA HILAL K SUED

Utawala wa Marekani chini ya Rais Donald Trump umeibua vita ya maneno dhidi ya Mahakama ya Kimataifa ya Makosa ya Jinai (International Criminal Court -ICC) na umetishia kuwawekea vikwazo majaji wake, na hata kuwafungulia mshitaka nchini humo iwapo wataendelea na uchunguzi wao dhidi ya m akosa ya kivita yanayodaiwa kufanywa na askari wa Marekani nchini Afghanistan.

John Bolton, Mshauri Mkuu wa masuala ya usalama wa Donald Trump ametoa vitisho hivyo katika hotuba yake mapema wiki hii mjini Washington kwa kikundi cha wanasiasa mahafidhani (Federalist Society.

Alisewma: “Leo, mkesha wa Septemba 11 napenda kutoa ujumbe wa wazi na wa bila kutafuna maneno kwa niaba ya Rais (Trump). Marekani itatumia njia zote n dani ya uwezo wake kuwalinda raia wetu na wale wa washiriki wetu kutoka kwa mashitaka ya uonevu unaofanywa na mahakama hii isiyo halali.

“Hatutashirikiana na ICC. Hatutatoa msaada wowote kwa ICC… tutaiachia ICC ife yenyewe. Hata hivyo, kwetu sisi na kwa hali yoyote ile Mahakama ya ICC ni kama ilisha kufa kitambo.”

Mwaka 2016 Mahakama hiyo yenye makao yake The Hague, Uholanzi ilisema askari wa majeshi ya Marekani na maafisa wa Shirika la Kijasusi la Marekani (Central Intelligence Agency –CIA) huenda walitenda uhalifu wa kivita kwa kuwatesa wananchi wa Afghanistan waliokuwa kizuizini na mamlaka za majeshi hayo.

Bolton amesema iwapo uchunguzi utaendelea kufanywa na ICC dhidi ya raia wake, utawala wa Trump utafikiria kuwapiga marufuku Majaji wa Mahakama hiyo kuingia Marekani, kuweka vikwazo fedha zote za Mahakama hiyo zilizopo katika mabenki na/au taasisi za fedha nchini Marekani na hata kuwafungulia mashitaka katika mahakama za Marekani.

Amesema Marekani inapingana na mawazo kwamba ICC inaweza kuwa na mamlaka makubwa zaidi ya Katiba ya Marekani, na kuongeza kwamba Marekani haiwezi kuruhusu raia wake washitakiwe na mamlaka za kutoka nje. MAREKANI ILIJITOA ICC MWAKA 2001 Mahakama ya ICC ilianzishwa mwaka 2002 kutokana na Mkataba wa Roma (Rome Statute) ambao mchakato wake, ulioanzia mwishoni mwa miaka ya 90 Marekani ilishiriki kikamilifu chini ya utawala wa Rais Bill Clinton.

Lakini mwaka 2001 chini ya Rais George W Bush Marekani ilijitoa, pamoja na nchi nyingine kama vile Urusi, China, Israel na nyinginezo. Akitangaza uamuzi wa kuitoa nchi yake kutoka ICC, Bush alizionya nchi zote duniani ambazo zitathubutu kuwakamata na kuwapeleka raia wa nchi yake kwenye mahakama ya ICC. Hata hivyo zaidi ya nchi 120 duniani kote na wanachama wa Mahakama hiyo.

Ni mahakama ya kwanza ya kudumu ya kimataifa iliyolenga kuwashitaki wahalifu wa makosa ya kivita, makosa dhidi ya ubinadamu na makosa ya mauaji ya kimbari.

Chimbuko kuu la kuanzishwa kwa ICC ni ile Mhakama ya kimataifa iliyoundwa baada ya Vita Kuu ya Pili, mwaka 1945 kuwashitaki wahalifu wa utawala wa Kinazi wa Adolf Hitler.

Baada ya hapo kulikuwa hakuna mahakama nyingine ya namna hiyo iliyoundwa na baada ya vita vya Cambodia, Yugoslavia na sierra Leione ambako kulitokea uhalifu mkubwa wa makosa ya kivita, jumuiya ya kimataifa iliamua kuunda mahakama maalum kushughulikia wahalifu waliotokana na vita hivyo.

Hata hivyo mbali na Marekani ICC imekuwa inashambuliwa na baadhi ya nchi nyingine kadha duniani, hususan zile za Barani Afrika kwa kile kinachoonekana undumila-kuwili kwake. UPENDELEO WA ICC NA UONEVU DHIDI YA AFRIKA Kwa mfano Kifungu Na. 8(a) (i-viii) cha mkataba wa ICC kinaorodhesha makosa ya kivita (war crimes) – ikiwa ni pamoja na kuuwa raia kwa makusudi, kutesa au kudhalilisha binadamu, kumpa maumivu makubwa hadi kuharibu afya au viungo vyake vya mwili; uharibifu mkubwa usio wa lazima kwa mali na miundominu, kuwakamata watu na kuwahamisha kwa nguvu na baadaye kuwaweka kizuizini bila kufuata sheria.

Kile ambacho Marekani ilikifanya nchini Iraq hakiwezi kwenda tofauti na makosa haya. Karibu vitendo vyote vya jinai vilivyofanywa na Marekani nchini Iraq baada ya uvamizi wa 2003, viko chini ya vifungu hivyo.

Kwa mfano, hatua ya aliyekuwa Jemadari mkuu wa majeshi ya Marekani, Rais George Bush

kuamrisha vikosi vyake vya anga kudondosha mabomu katika mji wa Fallujah Novemba 2004, hatua ambayo ilisababisha mamia ya watu wasio na hatia wakiwemo watoto na wanawake kupoteza maisha, moja kwa moja ni uhalifu wa kivita.

Lakini hadi sasa, ICC haijasema lolote kuhusu uhalifu huo uliofanywa na Bush na mshirika wake, waziri mkuu wa Uingereza Tony Blair. Badala yake, Marekani imekuwa ikishinikiza kukamatwa kwa viongozi na raia wa Afrika kama vile Rais wa Sudan Hassan Al-Bashir.

Kuhusu mateso juu ya binadamu, askari wa Marekani wanatuhumiwa kutesa na kuwadhalilisha mamia ya wafungwa waliokuwa wakishikiliwa katika magereza ya Abu-Ghraib na Mazar-e-Sharif mwaka 2004 nchini humo.

Na huko Sri Lanka, kwa mujibu wa ripoti ya mashirika ya kimataifa, katika miezi ya mwisho mwisho ya vita ya wenyewe kwa wenyewe vilivymalizika mwaka 2009, majeshi ya serikali yaliua maelfu ya raia wasiokuwa na silaha, wengine wakiwa mahospitalini walikokuwa wakitibiwa au kupata hifadhi.

Umoja wa Nchi za Ulaya (EU) ulipendekeza Umoja wa Mataifa iunde tume ya kuchunguza mauaji hayo, na ikibidi wahusika watinge ICC. Serikali ya Sri Lanka ilikuja juu juu na hapo hapo kuhoji: Mbona Umoja wa Mataifa haukufanya hivyo kwa Marekani kwenye mauaji ya Iraq?

Ikumbukwe kwamba pamoja na Marekani kujitoa katika ICC, bado inayo ushawishi mkubwa kupitia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa katika kuelekeza nani akamatwe na nani asikamatwe kama watuhumiwa wa ICC.

Kutolewa hati za kukamatwa kwa Omar Bashir wa Sudan na Kanali Gadaffi na wenzake ulitokana na ushawishi mkubwa wa Marekani.

SUALA LA AL-BASHIR NA NCHI ZA AFRIKA KUTISHIA KUJITOA

Kwa upande wake, nchi kadha Barani Afrika zimekuwa zikitishia kujitoa kutoka ICC kutoka na kile kinachoonekana kuonewa kwa Bara la Afrika tu. Ukweli ni kwamba tangu Mahakama hiyo ianze kazi na viongozi na/au watu wengine kutoka Bara la Afrika tu ndiyo ama wametina kwenye mahakama hiyo, wake mahabusu huko The hague kungojea kesi zao, au kutolewa hati za kukamatwa kwao.

Miaka miwili iliyopita Mahakama hiyo ilitoa uamuzi kwamba Afrika ya Kusini ilikiuka wajibu wake kimataifa pale iliposhindwa kumkamata Rais wa Sudan Omar Al_Bashir alipotembelea nchi hiyo Juni mwaka 2015.

Mahakama hiyo ilisema kwamba wakati Rais Zuma alipomkaribisha Al-Bashir, alishindwa kumtia mbaroni hivyo kukiuka waziwazi amri ya Mahakama hiyo ambayo ilikuwa imetoa hati ya kumkamata kutokana na makosa ya mauaji ya kimbari na makosa mengiine ya kivita katika jimbo la Darfur nchini mwake.

Aidha Mahakama hiyo ya ICC ilitupilia mbali utetezi dhaifu wa Serikali ya Afrika ya Kusini kwamba isingeweza kumtia mbaroni AlBashir kwa sababu alikuwa na kinga kama kiongozi mkuu wa nchi (head of state) aliyekuwa akihudhuria mkutano wa Umoja wa Afrika (AU).

Wachunguzi wa mambo wanasema tukio hilo limeitia dosari hadhi ya Afrika ya Kusini, nchi ambayo ni miongoni wa waanzilishi wa Mahakama hiyo ya kimataifa.

Hata hivyo uamuzi huo wa ICC ulionekana kutoa ‘ahueni’ ya aina fulani: jopo la majaji waliamua kutolifikisha suala hilo la Afrika ya Kusini kwenye Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwa ajili ya hatua zaidi dhidi ya nchi hiyo – kama vile kuwekewa vikwazo.

Katika uamuzi wake ICC ilisema mahakama ya Afrika ya Kusini yenyewe ilikuwa imetoa uamuzi dhidi ya serikali yake – pale ilipokubali ombi kutoka kwa kikundi kimoja cha wanaharakati la kutoa hati ya kumkamata Al Bashir.

Aidha jitihada za Afrika ya Kusini za kujitoa kutoka Mahakama hiyo ya Kimataifa ziligonga mwamba. Mapema mwezi Machi mwaka 2017 serikali hiyo ililazimika kulifuta tangazo lake la kujitoa baada ya Mahakama Kuu ya Pretoria kusema kwamba serikali ilikuwa imekwenda kinyume na Katiba ya nchi.

Na kwa upande wake Mahakama hiyo ya ICC imewkuwa na malalamiko yake hususan dhidi ya Umoja wa mataifa. Mapema mwaka jana Mwendesha Mashitaka Mkuu wa ICC Fatou Bensouda, alisema Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilishindwa kuwa pamoja na Mahakama hiyo.

Alitoa mfano kwamba Baraza hilo limeshindwa hata kutoa maazimio ya kulaani nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa ambazo katika matukio sita zilishindwa kumkamata Al-Bashir, na ambazo ICC ilitoa taarifa kwa Baraza.

Fatou Bensouda

John Bolton

Mahakama ya ICC katika kikao cha kusikiliza kesi

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.