Elimu inahitajika kwa wanaushirika

Rai - - MAKALA - NA MWANDISHI WETU

KATIKA siku za hivi karibuni kumekuwa na mwendelezo wa kuwakamata baadhi ya viongozi wabadhirifu wa vyama mbalimbali vya ushirika nchini.

Kwa miaka mingi vyama vyua ushirika vimegeuzwa shamba la bibi kutokana na kukithiri kwa ubadhirifu, ulaji na ufisadi uliokuwa ukifanywa na viongozi wake, ambao wengi wao walijigeuza miungu watu.

Viongozi wengi wa ushirika wao ndio wamekuwa wakulima, wasafirishaji na wakati huo huo wamejigeuza wanununuzi.

Hatua hiyo ilikuwa ikiwafanya watu hao wachache kuogopwa na wakulima ambao ndio waendeshaji wakuu wa vyama vikuu vya ushirika.

Haikuwa rahisi kwa mkulima mdogo ama wakulima kutoka kwenye vyama vya msingi kuwahoji viongozi wa chama vyama vikuu vya ushirika.

Mkulima aliyethubutu kufanya hivyo cha moto alikiona, alielekezea shutuma, hujuma na hila kadha wa kadha ili kumdhoofisha na wakati mwingine kuelezwa wazi kuwa zao lake halina kiwango kwenye soko, hali inayomlazimu kubaki nalo shambani hadi kumwozea.

Dhahama hili limewakumba sana wakulima wengi wa Kahawa wa Kagera, wapo walioambiwa Kahawa zao si nzuri hali iliyotajwa kuwasukuma kupeleka kahawa zao nchini Uganda, hatua iliyopingwa na Serikali.

Mara kwa mara kumekuwa kukiripotiwa kuwa ndani ya vyama vikuu vya ushirika kuna uonevu na ufujaji wa mali, matokeo yake yalikuwa ni kushughulikiwa kwa baadhi ya watu kwa madai kuwa wanavujisha taarifa hizo.

Jambo la kushukuru ni hatua na nia njema inayochukuliwa na Serikali ya awamu ya Tano, tayari vigogo wa sasa na hata wa zamani wa baadhi ya vyama vikuu vya ushirika mkoani Kagera, Mwanza na Kilimanjaro wameshaanza kufikishwa mahakamani.

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alipata kuonya kuwa Serikali haitamsamehe mtu yeyote atakayejihusisha na ubadhirifu wa mali na fedha za Ushirika nchini.

Majaliwa alitoa kauli hiyo katika Maadhimisho ya Siku ya Ushirika Duniani yaliyofanyika mkoani Dodoma, ambapo pamoja na mambo mengine alisema Serikali haitasita kuwachukulia hatua kali ikiwemo kuwapeleka katika vyombo vya dola wezi wa mali na fedha za ushirika kwani wamekuwa wakirudisha nyuma maendeleo ya vyama hivyo.

Hatua hiyo ni njema, lakini itakuwa njema zaidi kama kutakuwa na utaratibu wa kutoa elimu kwa wakulima wadogo kutambua haki na nguvu kubwa waliyonayo kwenye vyama vikuu vya ushirika.

Vyama vya msingi vyenyewe ndivyo nguzo kuu ya vyama vikuu vya Ushirika, pasipo na vyama vya msingi ni wazi hakuna chama kikuu.

Wakulima hawapaswi tena kuendelea kuwa watumishi wa viongozi wa vyama vikuu vya Ushirika, badala yake wanapaswa kuwa mabosi wa viongozi hao.

Wasiwaogope, wasiwaonee haya, wanapaswa kuwasema na kuwakosoa bila hiyana pale wanapoona kuna makosa ama mkengeuko wa aina yoyote ile.

Ni jukumu la vyama vya msingi vinavyoundwa na wakulima kuvilinda vyama vikuu vya Ushirika, si uhaini wala uhalifu kusimamia vyama vyao vikuu vya Ushirika.

Wakulima wakifanya hivyo ni wazi wizi, ubadhifu na uonevu utakwisha kwenye vyama vikuu vya Ushirika na ili suala hili lifanikiwe ni vema Serikali ikaviagiza vyama vikuu vya ushirika kuwapa elimu wakulima wadogo, lakini pia ni vema viongozi wa vyama vya msingi wakaepuka kununuliwa kwa namna yoyote ile hasa kwenye mikutano muhimu.

Inaelezwa kuwa halikuwa jambo la ajabu kwa viongozi wa vyama vya Ushirika kuwarubuni kwa fedha na zawadi mbalimbali viongozi wa vyama vya msingi ambao wanashiriki kwenye mikutano mbalimbali ya chama kikuu ili wapitishe matakwa yao.

IIfike mahali vyama vya msingi view na utayari wa kuwalipa posho, nauli na mahitaji mengine watu wanaoteuliwa kwenye kushiriki mikutano ya vyama vikuu vya Ushirika ili kuepuka kununuliwahatua inayoweza kumnyima mtu nguvu ya kupinga ama kukosoa.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.