NGO’s zinaweza kusaidia kupambana na ujinga, maradhi

Rai - - MAKALA - VICTOR MAKINDA

Ujinga, Maradhi na Umaskini ni maadui watatu wakuu wanaotukabili watanzania. Yupo adui wa nne, huyu anaitwa rushwa au maarufu kwa jina la Ufisadi.

Maadui hawa kwa ujumla wake tangu tupate uhuru mwaka 1961 tumekuwa tukipambana nao. Kwa kiasi fulani na kwa baadhi tu ya maeneo maadui hawa tumewapunguza nguvu. Yapo maeneo maadui hawa wamekuwa na nguvu kubwa hata kutushinda au kuonesha wazi kuwa nguvu tunayoitumia kupambana nao haitoshi na tuna kila sababu ya kuongeza dhamira, nguvu, mbinu na maarifa ya kupigana na maadui hawa.

Umaskini ni mama wa ujinga. Ujinga na maradhi ni marafiki wa kudumu. Palipo na umaskini, watu huwa wajinga. Palipo na ujinga maradhi hutamalaki. Hivyo kupambana na ujinga au moja kati ya maadui hawa ni kupambana na adui mwingine kwa wakati.

Awali nimeeleza kuwa maadui hawa kuna baadhi ya maeneo tumeonesha dalili za kuwapunguza nguvu. Lakini kuna maeneo ushindi wetu ni muhali. Hapa tuna swali la kujiuliza maeneo hayo ni yepi ambayo maadui hawa wamekuwa na nguvu kutushinda na maeneo yepi tumejitahidi kuwapunguza nguvu?. Je ushiriki wetu kama jamii ukoje katika kupambana na maadui hawa?

Ukweli Ulivyo maeneo ya majiji na miji kwa kiasi fulani maadui hawa ujinga, maradhi na umaskini tumefanikiwa kuwapunguza nguvu. Lakini maeneo ya vijijini maadui hawa wangali wana nguvu na wamesimama imara kutuangamiza. Tatizo letu kubwa, nguvu zetu nyingi tumezielekeza kupambana na maadui hawa mijini huku tukiwa tumevisahau vijiji ambako ndiko wanakoishi maelfu ya waTanzania wanaokabiliwa kwa nguvu na maadui hawa. Ndiyo, vijijini ujinga umetamalaki, maradhi hali kadhariki, lakini pia umaskini umetawalaki.

Serikali kwa upande wake inajitaidi na inaendelea kujitahidi kupambana na maadui hawa. Ukweli ulivyo serikali peke yake haiwezi kuundosha ujinga, maradhi na umaskini, miongoni mwa waTanzania pamoja na juhudi kubwa na nzuri za serikali hasa hii ya awamu ya tano ambayo imejidhatiti kupambana na maadui hawa kufa na kupona.

Kwa kuwa serikali ni watu na watu ndio sisi, hapa tunaona kuwa kuna ulazima wa watu binafsi na taasisi zisizo za kiserikali kuhakikisha kuwa kwa pamoja tunapambana kuuondoa umaskini wa kipato wa Watanzania walio wengi hususani watanzania waishio vijijini.

Zipo taasisi nyingi ambazo zinaisaida serikali kupambana na umaskini na maadui ujinga, maradhi na umaskini. Taasisi ya Tanganyika Christian Refugeeice Service (TCRS) ni miongoni mwa taasisi isiyo ya kiserikali na isiyolenga kupata faida, iliyojidhatiti kikamilifu kuisaidia serikali kuondoa umaskini kwa watanzania hususani waishio vijijini.

Taasisi ya TCRS ilianzishwa mwaka 1964 kwa lengo la kutoa misaada kwa wakimbizi. Miaka ya 1980 TCRS ilipanua wigo wa huduma zake na kuanza kufadhili miradi ya maendeleo vijijini. Mradi uliyojulikana kama Distric Intergrated Rural Develoment Project (IRDPs) ni kielelezo. Lengo la mradi huo ilikuwa ni kupanua njia za kisekta katika usambzaji wa maji safi na salama, huduma za afya, miundombinu, miradi ya elimu, utunzaji wa mazingira, kuboresha kilimo na mifugo sambamba na shughuli nyingine zenye mchango wa moja kwa moja kwa mwananchi kwa ajili ya kuiongezea kipato. Miradi hiyo ilitekelezwa katika mikoa ya Kigoma, Singida na Kagera katika wilaya za Ngara na Karagwe.

Awali TCRS ilikuwa ikitekeleza miradi yake kama msaada kwa wanachi katika maeneo yaliyoonekana kwa mujibu wa tafiti kuwa yanakabiliwa na umaskini mkubwa wa kipato na miundombinu ya elimu, afya na maji.

Mwaka 1999 TCRS ilibadili mbinu juu ya miradi yake ya kuwaondolea umaskini wananchi kutoka ile mbinu ya awali ya kutoa misaada na sasa ikaanza kutumia mbinu ya kuwajengea uwezo wananaachi. Kubadili mbinu huku kulifuatiwa na tafiti za kutosha juu ya miradi ambayo TCRS walikuwa wakiifadhili kwa wananchi na namna ilivyopokelewa na kutunzwa na kuleta tija kwa jamii.

Meneja wa wa Mpango wa Uwezeshaji wa Jamii wa TCRS Mkoa wa Morogoro, Rehema Samweli, anaeleza kuwaTCRS ililazimika kubadili mbinu kwani wananchi ikiwa wanapelekewa mradi ambao haukuwa kipaumbele chao, wanakosa utayari wa kuutunza na kuuthamini mradi husika. Lakini pia miradi inayofadhiliwa kwa asilimia mia moja, pasipo wananchi kushirikishwa katika utekelezaji wake, wananachi hukosa uchungu nayo hivyo walibaini kuwa ni vema kuwajengea uwezo wananchi, kubaini vipaumbele vyao na kuwashirikisha katika utekelezaji wa mradi kulingana na mahitaji yao.

Akielezea historia ya miradi ya kuwaondolea umaskini wananchi na kuwajengea uwezo wa kujimudu kwa kipato, Rehema Samweli, anasema kuwa Mkoani Morogoro katika Halmashhauri ya wilaya ya Morogoro vijijini, moja kati ya Halmsahauri ambayo wakazi wake wana kipato cha chini, mwaka 2006 walikuja na mradi wa kuwajengea uwezo wananchi kwa lengo la kuwasaidia katika miradi wanayoiibua na kufundisha shughuli za ujasiliamali ikiwa ni pamoja na kufuga na kazi za mikono.

Katika kutimiza azma hiyo, TCRS ilikutana na Madiwani wa kata zote za wilaya ya Morogoro na Wakuu wa Idara ili kuutambulisha mradi na kufanya mchakato wa kupata kata na vijiji ambavyo TCRS ilifanya kazi navyo. Vijiji 12 kutoka katika kata 3 vilichaguiwa kuingia katika mradi huo. Katika vijiji hivyo ambavyo mradi ulitekelezwa viongozi wa vijiji walipatiwa mafunzo juu ya maana ya uongozi, wajibu na majukumu ya vongozi.

TCRS ilifanya tafiti kwenye kaya 4,527 za vijiji vyote 12.Mwezi wa 12, TCRS ilitoa taarifa yake ya utafiti kwa na kubaini kuwa kaya za walengwa 613 , kati ya kaya hizo kaya 326 zinaongozwa na wanaume na kaya 287 zinaongozwa na wanawake ambapo mafunzo ya kilimo na ufugaji yalifanyika kwa vikundi. Katika tafiti hizo ilibainika pia kuna watu wasiojua kusoma wala kuandika ambapo mafunzo kwa wasiojua kusoma na kuandika yalitolewa.

TCRS iliendesha mafunzo ya afya na usafi wa mazingira kwa kamati za mazingira kila kijiji. Pia kampeni kuhusu ukimwi na virusi vya ukimwi ilifanyika. Vikundi vya kuweka akiba na kukopa maarufu kama SACCOS vilianzishwa na kupatiwa mafunzo maalumu.

Katika kuhakikisha wananchi walio maeneo kame wanapata maji TCRS Ilianzisha mradi wa kuvuna maji ya mvua. Mradi huu ulifanyika katika vijiji vya Kiwege na Mlilingwa, Halamshauri ya Morogoro Vijijini. TCRS ilijenga matanki mawili moja likiwa na uwezo wa kuhifadhi lita 36,000 na jingine lita 55,000. Sambamba na kuwajengea uwezo wananchi kwa kuwawezesha kufuga kuku, mbuzi na mizinga ya nyuki,

Ilitoa mafunzo kwa viongozi wa vijiji juu ya wajibu na majukumu ya uongozi, mabadiliko ya tabia ya nchi na katiba.

Huo ni mradi mmoja katika miradi mingi ambayo TCRS inatekeleza katika maeneo ya vijijini husuasani katika kwa lengo la kuisadia serikali kuondoa umaskini, ujinga na maradhi kwa wananchi wake.

Hivi sasa TCRS imekuja na mradi kabambe wa kuwatambua na kuwapa mafunzo maalumu wafanyabiashara wadogo wadogo maarufu kama Machinga wa mjini Morogoro.

Akielezea kuhusu mradi huo Rehema Samweli, anasema kuwa lengo la mradi huo ni kuhakikisha kuwa wafanya biashara ndogo ndogo, kwanza wanatambulika, pili wanafanya biashara katika maeneo na mazingira salama na tatu wawe na sifa za kuweza kukopesheka na taasisi za kifedha, kwani kwa muda mrefu kundi hili la wafanyabisahara wamekosa sifa za kukopesheka kwa kuwa hawana anuani maalumu ya makazi na bisahara zao.

Ukweli Ulivyo mchango wa TCRS na mashirika mengine ya kiraia una tija kubwa katika jamii ya Kitanzania katika kupambana na maadui wakuu ambao ni ujinga, maradhi, umaskini sambamba na ufisadi. Wito kwa serikali ni kutoa ushirikiano wa karibu kwa taasisi hizi ili kwa pamoja tuweze kupambana na maadui hawa na kuwashinda.

Meneja wa mradi wa mpango wa kuiweesha jamii Morogoro (TCRS), Rehema Samweli.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.