Je, zama za Rais Yoweri Museveni zimefika tamati Uganda?

Rai - - MAKALA - NDAHANI MWENDA ndahanimwenda66@gmail.com

Rais wa Uganda, Yoweri Museveni ni moja ya watawala wa Afrika ambao wapo madarakani kwa muda mrefu sasa. Yupo Ikulu ya Kampala tangu mwaka 1986 alipoingia kwa kumpindua Rais wa 8 wa nchi hiyo, Dk. Milton Obote.

Hadi sasa Rais Museveni amedumu madarakani kwa miaka 32. Na katika kipindi cha mwanzo cha utawala wake Yoweri Museveni alikuwa ni mmoja ya watawala wa Afrika waliokuwa wakikosoa uvunjwaji wa katiba hasa kwa watawala waliomtangulia. Alikemea watawala wa Afrika waliong’ang’ania kusalia madarakani.

Mataifa ya Magharibi yalimwagia sifa kedekede kwa kuwa Kiongozi anayependa demokrasia, licha ya hivyo Uganda ilipata misaada ya kifedha kutoka mashirika ya Kimataifa kama IMF na WB kutokana na sera zake za hapo awali wakati anaingia madarakani. Uchumi wa Uganda ulichupa kama mshale kwa wakati huo.

Lakini kadri siku zilivyokwenda madaraka yalimnogea Yoweri Museveni na kuanza kuvunja katiba ya nchi hiyo. Kwa sasa Rais Yoweri Museveni anatawala Uganda kwa mihula mitano. Katika uchaguzi wa mwaka 2001 aliahidi kuwa awamu hiyo ingekuwa ndiyo ya mwisho lakini alikuja kuigeuka ahadi hiyo baada ya kuoondoa ukomo wa Rais kukaa madarakani mwaka 2005.

Pia hakuishia hapo mwaka 2017 tumeshuhudia akiondoa ukomo wa umri wa mtu kugombea urais, kabla ya hapo umri wa mwisho ulikuwa ni miaka 70, lakini Rais Yoweri Museveni baada ya kuona amevuka aliamua kutumia Wabunge wa chama chake kuondoa ukomo wa umri.

Kwa uovu aliofanya Rais Yoweri Museveni ni dhahiri sasa anaogopa kuachia madaraka kwa kuhofia kuwajibishwa pindi mtawala mpya atakaposhika hatamu.

Kwasasa hakuna demokrasia Uganda, uchumi unadidimia, Uhuru wa habari hakuna. Vyama vya kijamii na wenye mawazo mbadala wanakandamizwa na kuumizwa.

Agosti 13, 2018 Katika uchaguzi mdogo wa Jimbo la Arua ambapo Rais Museveni alikwenda kumnadi mgombea wa chama chake, chama tawala NRM kiligalagazwa na mgombea binafsi aliyekuwa anaungwa mkono na wabunge wengine wa upinzani hasa Mbunge wa Jimbo la Kyadodo Mashariki, Robert Kyangylanyi Ssentamu (Bobi Wine), Rais Museveni na chama chake walipoona wameshindwa waliamua kuwapa kesi wabunge wa upinzani walioshiriki uchaguzi ule.

Tangu Agosti 13, 2018- Bobi Wine alikuwa anashikiliwa katika kambi ya Kijeshi huku akiteswa mpaka ulimwengu ulipopiga kelele ndipo alipoachiwa mara baada ya mawakili 24 kumtetea kupinga Bobi Wine kufunguliwa mashitaka katika Mahakama ya Kijeshi ili hali yeye si mwanajeshi. Mara baada ya kuachiwa alikamatwa tena na Jeshi la Polisi na kufunguliwa mashitaka katika mahakama ya kiraia kwa kosa linalodaiwa la uhaini. Serikali ya Museveni inadai Bobi Wine na wafuasi wake walilishambulia gari la Rais kwa mawe na hivyo kufanya wawe kutenda kosa la uhaini.

Pia Bobi Wine alipata dhamana na kuachiwa huku akiwa hawezi kutembea pekee yake baada ya mateso makali aliyokuwa akipata wakati anashikiliwa na Jeshi.

Baada ya tukio hilo, taasisi na watu mbalimbali walilaani kitendo cha vyombo vya dola kutumia nguvu pasipo lazima wakati wa kuwatawanya waandamanaji waliokuwa wakipinga Bobi Wine kushikiliwa.

Mmoja ya waliolaani kitendo cha Jeshi la wananchi wa Uganda na Polisi kuwapiga waandamanaji ni Mufti wa Uganda, Ramadhan Mubajje. Mufti Mubajje alilaani kitendo hicho alipokuwa akihutubia maelfu ya waumini wa Dini ya Kiislamu katika maadhimisho ya sikukuu ya Idd Al-Riadha tarehe 21 Agosti 2018 Jijini Kampala.

Pia katika kuhakikisha kuwa nchi inatawaliwa kwa sheria, Spika wa Bunge la Uganda, Rebecca Kadaga alimwandikia barua Rais Museveni akitaka kuwawajibisha wanajeshi waliowapiga wabunge wa upinzani katika sakata la uchaguzi wa Arua. Spika anadai kuwa kufanya hivyo ni kuvunja Katiba ya nchi hiyo Ibara ya 21 (a) na (b) inayozuia mtu kutezwa, hivyo itakuwa ni vigumu kwa yeye kuendesha shughuli za Bunge kama wanajeshi hao hawatachukuliwa hatua.

Kwasasa hali ya kisiasa nchini Uganda si shwari sana, makundi mbalimbali hata ndani ya chama tawala yameanza kumpinga Museveni waziwazi hasa vijana.

Rais Museveni anatuhumiwa kuiendesha nchi kama familia maana amewajaza madarakani ndugu zake, kuanzia mwanae mkubwa, Dada yake na mkewe.

Kumekuwa na sintofahamu katika nchi ya Uganda hasa kwa siku za hivi karibuni. Museveni kwa kujibu mapigo ya wanaompinga siku za karibuni amemjibu Spika Kadaga kuwa anaweza (yeye Museveni) kuvunja Bunge maana hata katika kipindi cha mwaka 19711979 hakukuwa na Bunge hivyo asijione yupo ‘peponi’

Rais Museveni si yule wa miaka 1970 hadi miaka ya 1980 aliyepigana msituni kuikomboa Uganda kutoka mikononi mwa Dk. Milton Obote, Museveni wa sasa hajali tena haki, hajali uhuru wa habari, hajali uhuru wa kujieleza. Kwasasa amekuwa Mungu mtu

ndani ya Uganda, hasikilizi mtu yoyote isipokuwa wanaomuunga mkono tu.

Ikumbukwe kuwa Spika Rebecca Kadaga ni Makamu Mwenyekiti wa Chama tawala (NRM) lakini hamwogopi bosi wake (Rais Museveni) anapokiuka sheria, na hii inaashiria kuwa huenda zama za Rais Museveni zinahesabika.

Wimbi la watawala waliokaa madarakani lilianza kutikisa huko Kaskazini mwa Afrika, Hosni Mubaraki (Misri) Muamar Gaddafi (Libya) na baada ya hapo akaja Laurent Gbagbo (Ivory Coast), Yahya Jammeh (Gambia) na mwaka jana tukashuhudia Robert Mugabe (Zimbabwe) aking’olewa madarakani pamoja na José Eduardo Dos Santos (Angola) ambaye aliyeondoka mwaka jana bila kupinduliwa.

Siku za Rais Yoweri Museveni naziona zinasogea kwani hata Julius Kaisari (Mtawala wa Rumi ya Kale) hakudumu milele kwenye utawala wake. Aliuawa kizembe kwa ulevi wake wa madaraka na kukiuka miiko ya Warumi.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.