Mke wa Rais abeba dhambi ya kusingizia

Rai - - MAKALA - KIZITO MPANGALA

Ilisemwa na itazidi kusemwa kwamba ya kale ni dhahabu! Naam, ni dhahabu haswa kama unapekua na kupata mafunzo mbalimbali kwayo. Mambo mengi ya sasa yana misingi yake katika mambo ya kale. Kwa mfano kaptura, suruali, gauni, kofia, kiatu, meli, boti, kalai, chepe, simu, siasa, michezo na kadhalika.

Mbunge wa zamani katika Bunge la Dola la kale la Kirumi (Ancient Roma Empire) Mzee Lucius Annaeus Seneca aikumbana na mambo mawili katika ubunge wake ambayo yalikuwa na misingi ya kisiasa tu. Siasa za zamani hazikuwa na mchezo mchezo! Uwongo ulipikwa kwa kuwekwa viungo vingi ili uwe ukweli na ukweli nao ulikaangwa barabara ili uwe uwongo.

Lucius Annaeus Seneca alizaliwamwaka4KK(kabla ya kuzaliwa Yesu Kristo “mbunge” wa zamani wa jimbo la Nazareti, Iesus Nazarenum Rex Iudeus, ‘INRI’) katika kitongoji cha Cordoba (sasa ni sehemu ya Hispania) katika mji wa Baetica. Alichukuliwa na mama yake mkubwa kwenda mjini Roma. Huko Roma alifundishwa fasihi na falsafa ikiwa kama ni elimu ya msingi kwa watoto Warumi wakati ule.

Kutokana na matatizo ya kiafya katika ujana wake ikiwemo Pumu, Seneca alipelekwa kwa mama yake mkubwa nchini Misri aishi huko. Mume wa mama yake mkubwa alikuwa mjuzi wa dawa, alimshughulikia Seneca kwa miaka 10 na kasha lirudi tena Roma. Mwaka 31 BK (baada ya kuzaliwa Yesu Kristo, “mbunge” wa zamani wa jimbo la Nazareti, INRI) aliporudi Roma kwa kushawishiwa na mama yake mkubwa, Seneca alichaguliwa kuwa mbunge.

Miaka ya mwanzo wa ubunge wake alikuwa mtu mwenye mafanikio kisiasa na aliheshimiwa sana kwa utulivu wa akili yake. Lakini kiongozi mkuu wa Dola la kale la Roma wakati ule, Gaius Kaizari maarufu kama Caligula, alimchukia Seneca na alihisi kama ni mkosaji, hivyo alimuamuru ajinyonge yeye mwenyewe. Lakini Seneca hakujinyonga kwa kuwa alikuwa mgonjwa mno wakati amri ya kujinyonga inatolewa. Katika maandiko yake Seneca anamwelezea Gaius Kaizari (Caligula) kama ni mtu katili asiye na huruma.

Alipota ahueni alikumbana na kisa kingine ambacho nafsi yake ilikataa. Wakati Claudius Kaizari anachukua madaka ya kuwa kiongozi wa Dola la kale la Warumi, Seneca alisingiziwa kwamba amembaka Julia Livilla, dada yake Gaius Kaizari (Caligula), aliyetoa madai hayo ni Valeria Messalina, mke wa Claudius Kaizari. Yote hayo yalikuwa ni malengo ya manufaa ya kisiasa kwa “first lady” Valeria Messalina. Seneca laihukumiwa kifo lakini baadaye alikwenda uhamishoni. Kazi zake mbili ambazo zinapatikana ni CONSOLATION TO HELVIAnaCONSOLATION TO POLYBIUS.

Mwaka 49 BK, Seneca aliitwa tena Roma kutoka uhamishoni. Kaizari Claudius alishinikizwa na mke wake wan ne, Agrippina, ambaye alikuwa na undugu na Seneca. Hivyo, Claudius huenda angekosa penzi kama angepuza shinikizo lile la kumrudisha Seneca. Seneca aliporudi Roma aliteuliwa kuwa mwalimu wa mwana wa Claudius. Mwana huyo huyo baadaye akawa kiongozi wa Dola hilo na aliitwa NERO CLAUDIUS KAIZARI, kiongozi katili zaidi katika historia ya Dola la kale la Warumi (Ancient Roma Empire), na Seneca aliteuliwa kuwa mshauri wa Nero Kaizari akisaidiana na mlinzi mkuu bwana Sextus Aficanus Burrus.

Seneca anasifika kwa uandishi wa hotuba nzuri alizokuwa akimuandalia Nero Kaizari akisaidiana na Sextus Africanus Burrus. Pia aliandika wasifu mzuri wa Claudius Kaizari (baba yake Nero) ambao ulisomwa na Nero wakati wa mazishi ya Claudius. Mwaka 58 BK, Publius Suillius Rufus alimvamia Seneca ili amuue lakini alishindwa. Publius alimtuhumu Seneca kwamba alilala na Agrippina, mjane wa Claudius Kaizari.

Baada ya kiufariki Publius, Seneca alitangaza mara mbili kujiuzulu lakini alikataliwa na mkuu wake, Nero. Seneca akaamua kuishi maisha ya ukimya kwani hakuonekana mara kwa mara kazini mahakamani. Aliishi katika ukimya huo huku kila mmoja akijihoji kuna nini anakifanya. Muda mfupi baadae alitangaza vitabu vyake viwili ambavyo ni NATURALES QUAESTIONES na LETTERS TO LUCILIUS ambacho aliandika mawazo yake ya kifalsafa. Alihusika katika kikundi kilichopanga njama za kumuua Nero. Nero alipopata taarifa alimuamuru Seneca ajiue yeye mwenyewe.

Seneca anaheshimika hata sasa kuwa ni miongoni mwa wanafalsafa muhimu wa kale katika Dola la kale la Warumi. Alikuwa pia mwandishi wa tamthilya ambapo aliandika tamthilya 8 ikiwemo tamthiliya maarufu ya kisiasa inayoitwa OEDIPUS THE KING. Pia, aliandika insha mbalimbali ambazo ni chanzo kimojawapo cha maarifa mjini Roma.

Pamoja na kuzingiziwa kubaka na changamoto zingine, Seneca anatupa mafunzo kwamba kutatishwa tama na watu kwa maneno ya uwongo hakuondoi morali ya kufanya mambo mengine muhimu. Pia, Seneca anatuonyesha wazi kwamba kujisomea maandiko mbalimbali ni suala la muhimu na anatoa rai kwa wanasiasa kujibiidisha katika maarifa ili waboreke katika malumbano ya hoja na siyo kulumbana kwa hisia tu.

Moja ya kazi zake ambazo zimetafsiriwa kwa lugha ya Kiingereza ni HARDSHIP AND HAPPINESS nyingine ni ANGER, MERCY AND REVANGE ambazo zinaeleza mawazo yake katika ugumu wa maisha, furaha, huruma, hasira na kisasi. Seneca hakulipa kisasi kwa yeyote aliyemtendea vibaya, iwe kwa manufaa ya kisiasa anu si kisiasa, hivyo anatoa somo kwamba kisasi muhimu ni kutunza ukimya. Mwalimu wangu fulani Seminarini alikuwa akituhimiza kwa kusema “vijana mjifunze kunyamaza, tunzeni ukimya,” basi tulikuwa Waseminari haswa!

Seneca anatunda mengi katika maisha, hakuwa na digrii ya yoyote lakini morali yake ilimpaisha. Kila mmoja ana morali na juhudi katika kuliendea jambo, hivyo tuzitumie. Hata kuhabarishana namna hii kunatokana na morali. Kwa hiyo wanasiasa wakipenda wanaweza kufuata mifano ya maisha ya Lucius Annaeus Seneca.

Lucius Annaeus Seneca

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.