Mfumo dume kikwazo cha maendeleo ya mwanamke

Rai - - MAKALA - NA JOHANES RESPICHIUS

IMEKUWA kawaida kusikia watu mbalimbali hasa wanaharakati wakizungumzia neno ‘Mfumo dume’ pindi wanapotoa elimu kuhusu masuala ya kijinsia.

Kwa maana rahisi, Mfumo dume ni matokeo ya dhana za kurithi, imani za kidini, mila na tamaduni ambazo zinamkandamiza mwanamke na mtoto wa kike.

Mfumo huu umekuwa ukiwanyima haki wanawake na watoto wa kike katika Nyanja mbalimbali kama vile elimu, maamuzi, kutoa mawazo, afya na masuala mengine mengi.

Hali hii ndiyo iliyoweka msukumo mkubwa kwa watu mbalimbali kujikusanya kwa lengo la kuweka agenda moja ya kuhakikisha mwanamke na mtoto wa kike anakuwa na sauti kwenye jamii ikiwa ni pamoja na kupata haki sawa na mwanaume.

Hapo ndipo yalianzishwa mashirika kama Mtandao wa Kijinsia Tanzania (TGNP)likiwa na lengo la kuwezesha harakati za uhamasishaji wa kike ambao huathiri na kuchangia katika ufanisi wa kijinsia wa kuandaa sera na utekelezaji katika maeneo ya Kilimo, Maji, Afya, Elimu na Viwanda, kwa mgawanyo sawa wa rasilimali na maisha endelevu.

Katika kuhakikisha hilo linafanikiwa TGNP imekuwa ikitumia njia tofauti za kufanya harakati zake za kumkomboa mwanamke ikiwamo ya kutumia Kilinge cha Simulizi ambacho utoa fursa kwa baadhi ya makundi ya watu kusikiliza simulizi kutoka kwa watu waliofanikiwa katika harakati zao.

Agosti 31, mwaka huu, TGNP uliwakutanisha Ma-Profesa wawili kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Ruth Meena na Marjorie Mbilinyi ambao walitoa simulizi za maisha yao kwa washiriki wa Kilinge cha Simulizi kilichowahusisha wanafunzi wa kike wa vyuo vikuu.

Wote katika simulizi zao wanaonyesha jinsi gani walivyoweza kupambana na mfumo dume ambavyo ulikuwa umekithiri katika miaka ambayo walikuwa wasichana wadogo.

Profesa Mbilinyi akatumia simulizi ya maisha yake kuwataka vijana walioshiriki Kilinge hicho kutokata tamaa katika kuhakikisha kile wanachokipambania kinafanikiwa bila kujali vikwazo ambavyo vinawaandama.

Anasema tofauti na baadhi ya watu nchini Tanzania kudhani kuwa mfumo dume haupo katika nchi zilizoendele si kweli kwani katika familia yao vitendo vya unyanyasaji wa jinsia na mfumo dume vilisababisha mamayake mzazi kujiua.

Anasema kuwa amezaliwa katika moja ya familia za kipato cha kati nchi za ulaya kwamba pamoja nakuzaliwa ulaya vitendo vya ukatili wa kijinsia na mfumo dume vilikithiri katika familia yao, ambavyo viligharimu uhai wa mama yake mzazi.

“Mfumo dume katika nchi zilizoendelea ulikuwa kwa kiasi kikubwa kwani pamoja na kwamba mama yangu alikuwa amesoma na kufanya kazi baada ya kuolewa na baba yangu aliachishwa kazi ili akawe mama wa nyumbani na kazi yake iwe ni kumtegemea baba na kuangalia familia jambo ambalo lilimfanya anyanyasike kwa kuwa mtegemezi.

“Kwa bahati nzuri nilianza kujitegemea tangu nikiwa mdogo na sijawahi kuishi kwa kumtegemea mtu hata mama yangu alipofariki niliweza kupambana na changamnoto nyingi ambazo zilikuwa mbele yangu.

“Kutokana na msimamo wangu ilifika hatua nikata kufutwa kwenye familia na bibi yangu, nilikuwa nasoma lakini baada ya mama kufa na baba kuoa mke mwingine, mama wa kambo alininyima nafasi ya kujiendeleza jambo ambalo lilinipa msukumo mkubwa wa kumpigania mwanamke na kumkwamua kwenye mfumo dume,” anasema Profesa Mbilinyi.

Anawashauri vijana wa kike walio katika elimu ya juu kupambana kikamilifu na kusimamia malengo waliojewekea bila kujali changamoto zilizopo na kwamba wanapaswa kujiwekea malengo kama aliyojiwekea kwamba ‘Hawezi Kuishi bila Kuleta Mabadiliko na Ukombozi kwa Mwanamke’.

Kwa upande wake, Profesa. Ruth Meena naye anaanza kwa kuwashauri washiriki hao ambao wengi wao walikuwa vijana wa kike kutoka vyuo vikuu mbalimbali nchini kuhakikisha wanasimamia ndoto zao.

Anasema kuwa wasikubali kuvunjwa moyo kwa kukatiushwa tamaa bali wanapaswa kupambana na vikwazo vilivyopo kwani wao pia walikumbana navyo, lakini ujasiri wao ndio siri ya mafanikio yanayoonekana wakati huu.

“Nilisoma kwa shida, nilianza kupinga vitendo vya unyanyasaji tangu nikiwa shuleni na wakati mwingine ujasiri wangu uliwaponza wenzangu…kinachotakiwa ni kupambana kufikia malengo ama ndoto za kila mmoja bila kujali vikwazo.

“Niliolewa nikiwa na miaka 23 wakati nasoma chuo kutokana na mfumo dume mume wangu alinibadilisha jina na kuacha kutumia jina la baba yangu nikaanza kutumia jina lake jambo ambalo lilimuumiza sana mama yangu wakati wa mahafali baada ya kutosikia nikiitwa kwa jina la Baba.

“Alikasilika sana akidhani sikufaulu mtihani ndio maana hakusikia jina langu anal9lifahamu likiitwa, akaambiwa nimeitwa kwa jina la mume wangu... alimfuata Mume wangu na kumuuliza ananibadilisha jina yeye ndiye alinisomesha mpaka kufika hapo nilipokuwa... hiyo inaonyesha ni kiasi gani alikuwa anachukiwa mfumo dume,” anasema Profesa Meena.

Aanaasema mfumo dume haukuishia hapa kwamba hadi anafikia hatua ya kuwa Profesa amepetia milima na mabunde mengi ambayo yalikuwa yanawekwa na baadhi ya watu ili asiweze kufikia ndoto yake lakini kutokana na kutokata tamaaa ameweza walau kifikia kile alichokiwa aakitamani siku mojaa akifikie.

Kuhusu ukatili wa kingono anasema umeanza kitambo hicho kwani wakiwa jeshini yeye na wenzake watano waliwahi kuandikiwa barua inayofanana ya kimapenzi na mmoja wa askari kambini walikokuwa.

Anasema kutokana na ushirikiano waliokuwa nao waliweza kushirikiana kwa pamoja na kusababisha askari akafikishwa kwenye ngazi husika akachukuliwa hatua ya kuswekwa jela miezi sita.

Aidha mwanaharakati ambaye ni mwanachama wa Mtandao wa Kijinsia Tanzania (TGNP ) Profesa Meena amesisitiza kuwa ni muda muafaka kwa wanawake wote kwa pamoja kuungana kwa pamoja ili kupinga vikali mfumo huo ambao unawakandamiza naa kuwanyonya na kwamba wasimame imara kupigania maendeleo na kutimiza ndoto zao.

Kwamba wanatakiwa kuwa mstari wa mbele kuukataa na kupiga vita ukatili wa kijinsia, utabaka pamoja na ubeberu uliokithiri hasa kwa zile familia ambazo bado zinadhana potofu ya kumdidimiza mwanamke katika kupata elimu na uongozi.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.