Klopp presha tupu, rekodi zinapeleka kilio Anfield

Rai - - MAKALA JASMEPITIEMBA -

NI mwishoni mwa wiki hii mbele ya mashabiki 90,000 wanaotarajiwa kuujaza Uwanja wa Wembley, mchezo wa raundi ya tano tangu kuanza kwa msimu huu wa Ligi Kuu ya England (EPL).

Je, dakika 90 za mtanange huo zitamalizika kwa Liver ya kocha Jurgen Klopp kuendeleza wimbi la ushindi baada ya kuzoa pointi 12 katika mechi zote nne zilizopitaItakumbukwa kuwa ushindi wao wa mwisho ni ule wa mabao 4-0 walioupata katika Uwanja wa Anfield dhidi ya West Ham, ambao ulikuja baada ya kuzichapa Crystal Palace (2-0), Brighton (1-0), na Leicester (2-1).

Kwa upande wake, Tottenham ya kocha Mauricio Pochettino, moja kati ya timu ngumu EPL, itarejea uwanjani ikiwa na hasira kwani ilichapwa mabao 2-1 na Watford katika mchezo uliopita.

Aidha, bado kushindwa kuondoka na pointi tatu dhidi ya Watford hakumaanishi kuwa Tottenham ni timu mbovu. Huenda ni kutokana na ugumu wa Ligi Kuu ya England, ambayo mara nyingi ni ngumu kutabiri matokeo, hata timu kubwa inapokutana na ‘kibonde’.

Ikumbukwe kuwa kabla ya kukutana na Watford, walishaishindilia Man United mabao 3-0, tena wakiwa ugenini katika mchezo huo uliochezwa mbele ya mashabiki 74,994.

Ushindi huo mnono uliomweka hatiani kocha mwenye maneno mengi, Jose Mourinho, ulitanguliwa na matokeo mengine mazuri dhidi ya Fulham (3-1) na Newcasle (2-1).

Kabla ya kukumbana na kipigo hicho cha ugenini, tayari kikosi hicho kilishashinda mechi zake tatu, kikizilaza mapema Manchester United (3-0), Fulham (3-1), na Newcastle (2-1).

Ukiacha kiu ya kila upande kuzitaka pointi tatu, uhondo wa mchezo huo wa keshokutwa uko kwenye safu za ushambualiaji wa timu hizo mbili. Wakati Liver wakiwa wametumia mechi nne zilizopita kupachika mabao tisa, iko hivyo pia kwa Tottenham.

Lakini sasa, wanachoweza kutambia mashabiki wa Liver mbele ya wenzao hao wa Kaskazini mwa Londo, ni eneo lao la ulinzi, ambalo hadi hatua hii, ni mpira mmoja pekee uliofanikiwa kuzitikisa nyavu zao.

Tottenham, ambayo haikusajili mchezaji yeyote katika dirisha la usajili la majira ya kiangazi lililofungwa wiki chache zilizopita, wataingia uwanjani wakiwa na wasiwasi mkubwa wa ‘ukuta’ wao.

Katika mechi nne zilizopita, tayari mabeki wake wamesharuhusu mabao matano, sawa na ‘vibonde’ Bournemouth, Leicester City, Wolves na Cardiff City, huku ikizidiwa hata na Watford (3) na Southampton (4), ambazo si sehemu ya timu zinazopewa nafasi kubwa ya kutwaa ubingwa msimu huu.

Hiyo inaonesha wazi kuwa Tottenham itakuwa na kazi ya ziada kuwazuia Liver kupata bao kwa dakika zote 90. Pia, haitashangaz akuona safu ya ulinzi ya Liver ikirusu bao kutokana na ubora wa Tottenham katika eneo la ushambuliaji.

Kuelekea mchezo huo wa Jumamosi, rekodi zinaonesha kuwa timu hizo zimeshakutana mara 52, Liver wakiwa kinara wa ushindi kwa kushinda mechi 23. Hata hivyo, wasiwasi mkubwa wa mashabiki wa Liver ni kwamba katika mechi 14 pekee ambazo Spurs wameambulia ushindi, 12 ni walizokuwa nyumbani.

Kwamba, licha ya Liver kuongoza kwa kuifunga Spurs, hawana rekodi nzuri wanapokutana nao ugenini, yaani nje ya Uwanja wa Anfield, ambao ‘Majogoo’ hao walianza kuutumia 1884.

Kulithibitisha hilo, mchezo wa mwisho ambao Liver walikwenda ugenini katika Uwanja wa Wembley, waliondoshwa kwa kichapo cha mabao 4-1. Matokeo ya mechi iliyofuata, ambayo Liver ilikuwa nyumbani Anfield, hayakuwa mazuri pia, waliambulia sare ya mabao 2-2 mbele ya Tottenham.

HASSAN DAUDI NA MITANDAO

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.