Uganda ilivyoisafishia njia Stars Afcon 2019

Rai - - MAKALA JASMEPITIEMBA - NA AYOUB HINJO

TAYARI timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ imeshacheza michezo miwili ya kutafuta tiketi ya kushiriki michuano ya Mataifa Afrika hapo mwakani (Afcon 2019) ambayo itafanyika nchini Cameroon.

Juni 10, mwaka jana, kikosi hicho kinachonolewa na mwanasoka wa zamani wa Nigeria, Emmanuel Amunike, baada ya kocha mzawa, Salum Mayanga, kutoongezewa mkabata, kilicheza mchezo wake wa kwanza wa Kundi L dhidi ya Lesotho.

Katika mtanange huo uliochezwa katika Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Stars waliambulia sare ya bao 1-1, matokeo ambayo hayakuwavutia mashabiki wa kandanda nchini, wengi wakiitabiria kuishia njiani katika safari ya kuisaka nafasi ya kwenda Cameroon.

Huku straika tegemeo wa kikosi cha Tanzania, Mbwana Samatta, akifanikiwa kufunga bao katika dakika ya 28 kwa mkwaju wa faulo, mshambuliaji wa Lesotho, Thapelo Tale, naye alijibu mapigo kwa kuisawazisha timu yake dakika saba baadaye.

Mchezo wa pili wa Stars ulipigwa mwishoni mwa wiki iliyopita katika Uwanja wa Mandela, Uganda, dhidi ya wenyeji wao ‘The Cranes’. Dakika 90 za mtanange huo uliokuwa na upinzani mkali zilimalizika kwa timu hizo kutofungana.

Hata hivyo, tofauti na ilivyokuwa dhidi ya Lesotho, licha ya kwamba Stars iliambulia pointi moja, kiwango ilichokionesha ugenini kiliwavutia mashabiki wengi wa soka la Tanzania, wakiamini timu yao imeimarika.

Kwa matokeo hayo sasa, Amunike na vijana wake wana pointi mbili ambazo wamezipata katika mechi hizo mbili, mchezo wa tatu ukitarajiwa kuchezwa Oktoba 10, mwaka huu, dhidi ya Cape Verde.

Hivyo, bado suluhu dhidi ya Uganda inaipa nafasi Stars katika mbio za kuisaka tiketi ya kwenda Cameroon mwakani, hasa endapo itakusanya pointi tatu dhidi ya wapinzani wao hao, Cape Verde.

Matumani makubwa waliyonayo mashabiki wa kabumbu nchini ni kikosi cha sasa cha Stars, ambacho si tu kiina kocha wa kiwango cha juu, Amunike, bali pia kinaundwa na mastaa wengi wanaocheza soka la kulipwa nje ya mipaka ya Tanzania.

Wakati huo huo, Stars ina nafasi ya kufanya vizuri kwa sababu hata wapinzani wao hakuna mwenye pointi nyingi zaidi ya Uganda iliyofikisha pointi nne.

Jambo kubwa pekee kwa timu ya Stars ni kutumia michezo itakayopigwa uwanja wao wa nyumbani kwa faida zaidi ya kupata pointi tatu kinyume na hapo inaweza kuwa tatizo kwao.

Yaani katika mchezo ule wa kwanza dhidi ya Lesotho ilibidi washinde ili wajiweke katika nafasi nzuri zaidi ya kuwa moja ya timu yenye uhakika wa kusonga mbele.

Lakini hata hali ilivyo ndani ya kundi hilo bado nafasi ni kubwa sababu bado ana michezo minne ya kucheza ambayo anatakiwa kupata ushindi.

Kwa upande wangu, kubwa zaidi ni jinsi ambavyo wachezaji walivyoweza kuonyesha uwezo mkubwa dhidi ya Uganda katika mchezo uliopigwa Uwanja wa Mandela.

Ulikuwa mchezo wa kwanza wa kocha wa Taifa Stars, Emmanuel Amunike ambaye amechukua nafasi ya Salum Mayanga, hakika ulikuwa mtihani ambao wengi walisubiri kuona ni kipi raia huyo wa Nigeria atakifanya.

Moja, jinsi alivyopanga kikosi chake huku akitumia mfumo wa 3-4-3 kwa kupanga mabeki wa tatu wa kati (Aggrey Morris, David Mwantika na Abdi Banda) ambao walionyesha uwezo mkubwa wa kuzuia.

Kisha viungo wanne ambao wawili walikuwa ni wa asili

(Mudathir Yahya na Frank Domayo) na wengi walikuwa wakitokea pembeni wakipandisha na kuzuia mashambulizi kitaalamu wanaitwa wing-back (Hassan Kessy na Gadiel Michael)

Eneo la mwisho la uwanja walisimama washambuliaji watatu (Simon Msuva, Thomas Ulimwengu na Samatta) ambao kazi yao kubwa ilikuwa kukwamisha mpira wavuni kwa wapinzani.

Kipindi cha kwanza kilikuwa kigumu kwa Taifa Stars sababu msingi wa mfumo ambao Amunike aliutumia unategemea zaidi ufanisi kazi wa ‘wing-backs’ ambao walikuwa ni Kessy na Gadiel.

Kuelemewa kwa kiungo cha Taifa Stars kulitokana na Uganda kuwa na watu wengi zaidi katika eneo hilo ambalo walisimama wawili (Mudathir na Domayo) dhidi ya watatu ambao ambao waliweza kutawala kwa kiasi kikubwa.

Nilitegemea kipindi cha pili kuwe na mabadiliko kwa Tanzania iwe kwa kuingiza kiungo mwingine wa kati au kubadilika mfumo ili kuendana na kasi ya wapinzani.

Hilo la pili lilitokea kwa kocha kubadili mfumo kwa kucheza 4-4-2 huku akimtoa Gadiel na kumpa nafasi Farid Mussa ambaye alienda kucheza winga wa kushoto.

Kwa kiasi kikubwa timu ilionekana kuwa na uhai na kuwadhibiti Uganda ambao walikuwa na nguvu kubwa pembeni ambako waliwasimamisha Nicolas Wadada na Godfrey Walusimbi.

Mabeki hao wa pembeni wa Uganda hawakuwa na nguvu kubwa kama kipindi cha kwanza na hatimaye Stars walicheza kwa kutengeneza nafasi ambazo hata hivyo walishindwa kuzitumia vizuri kupata mabao.

Bado kundi hilo lipo wazi huku kila timu ikiwa na nafasi ya kusonga mbele kama watafanikiwa kuzichanga karata zao vizuri lakini kwa Tanzania naamini uwezo ni mkubwa kutokana na wachezaji waliopo lakini pia kila mmoja anaonyesha kuwa na njaa ya mafanikio.

Kikosi cha Taifa Stars kikifanya mazoezi

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.