Wajanja ‘wapiga’ fedha za serikali

Rai - - MBELE - NA IBRAHIM YASSIN, SONGWE

Serikali inawapenda watu wake ndiyo maana inatoa fedha kwa ajili ya ujenzi wa miradi, lakini viongozi ngazi ya wilaya wanakuwa wazembe kiasi cha kusababisha madudu katika halmashauri, mmekuwa mkiendeleza migogoro na wenyeviti na wakurugenzi mnatafutiana fitna.

MKOA mpya wa Songwe, uliogawanywa kutoka jiji la Mbeya, unatajwa kugeuzwa kichaka cha ulaji na baadhi ya watendaji wake. RAI linaripoti.

Ukweli wa hilo umedhibitishwa na uongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) mkoa wa Songwe, baada ya kutembelea baadhi ya miradi ya maendeleo mkoani humo.

Uongozi wa chama hicho tawala mkoa umebaini uwapo wa baadhi ya miradi kukwama tangu mwaka 2013 licha ya serikali kutoa kiasi kikubwa cha fedha za utekelezaji.

Miradi iliyokwama ni ujenzi wa tenki la maji lenye urefu wa mita 48, lililogharimu takribani milioni 400, likiwa na uwezo wa kutunza lita 153,000 za maji.

Mradi huo wa maji ulitarajiwa kunufaisha wakazi 4,754 na ulitakiwa kukamilika ndani ya miezi sita, tangu ulipoanza kutekelezwa katika mwaka wa fedha 2013/14, lakini hadi sasa haujakamilika na mkandarasi tayari ameshaondoka kwenye eneo la kazi licha ya kupewa robo tatu ya fedha za malipo ya mradi huo.

Aidha, ujenzi wa kituo cha afya Mbuyuni ambacho serikali kupitia Wizara ya Afya ilitoa Sh milioni 400 nao umekwama.

Akizungumza katika ziara za utekelezaji wa ilani ya CCM, Meneja wa maji wilayani humo, Mhandisi Needson Ngailo alisema mradi huo ulikwama kwa kuwa ulikuwa unasimamiwa na wilaya ya Chunya.

Alisema Mkandarasi wa mradi huo, aliingia mkataba na wilaya ya Chunya - Mbeya wakati Songwe ikiwa ndani ya Mbeya na baada ya Songwe kujitegemea waliomba wapatiwe mikataba hiyo, lakini walikataliwa na hadi sasa baadhi ya watumishi wapo chini ya Chunya na kwamba kampuni ya Muka Techno limited ya Dar es salaam ndiyo iliyopewa kazi hiyo.

Mkuu wa wilaya Songwe, Samwel Jeremiah alisema mkandarasi huyo alilipwa Sh milioni 330 na zilibaki Sh milioni 53.

“Tuliwahi kumkamata na kumweka rumande kutokana na ubabaishaji wa utekelezaji wa ujenzi huo. Pia nitawasiliana na Mkuu wa Wilaya ya Chunya ili miradi yote ya Songwe isimamiwe na Songwe,” alisema.

Mwenyekiti wa CCM mkoani humo, Eliniko Mkola alisema kutelekezwa kwa mradi huo kunatokana na baadhi ya watendaji wa Serikali kutumia vibaya fedha za serikali.

“Namshauri Mkuu wa Mkoa wa Songwe azungumze na Mkuu wa Mkoa wa Mbeya ili watafute ufumbuzi wa suala hilo, ikiwa ni pamoja na kuhakikisha mkandarasi huyo anakamatwa.

“Haiwezekani serikali itoe fedha nyingi kiasi hicho, halafu viongozi wa ngazi za wilaya waharibu pasipokuchukuliwa hatua, ni lazima waliohusika kuuchakachua mradi huo wachukuliwe hatua kwa sababu tenki lenyewe linavuja, pia halina mfumo wa bomba la nje, chemba hazipo, huu ni wizi,’’ alisisitiza.

Katika mradi wa kituo cha afya Mbuyuni, kamati hiyo imebaini ubadhirifu baada ya baadhi ya kuta za jengo la kituo hicho kupinda huku fremu za milango zikikosa ubora uanolandana na Sh. milioni 400 zilizotumika licha ya kituo hicho kutokamilika.

“Nimefanya kazi za ukandarasi miaka mingi, sijawahi kuona ujenzi wa haina hii, serikali inatoa fedha kwa ajili ya miradi ya maendeleo, lakini kwa jinsi ujenzi huu ulivyo, ni dhahiri kuwa viongozi ngazi ya wilaya mlikuwa likizo, fedha hapa zimetumika vibaya” alisema Mkola.

Hata hivyo, Afisa manunuzi wa wilaya hiyo, Recho Ndimila alisema fedha iliyobaki ni milioni sita pekee na kuongeza kuwa baadhi ya vifaa vingine vipo stoo.

Aidha, Mhandisi wa majengo, Urch Mkombozi alisema ili kurekebisha baadhi ya kuta zilizopinda kutahitajika fedha nyingine zaidi ya Sh milioni 50 kukamilisha ujenzi huo.

Kutokana na utetezi wa Mkombozi, Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Brigedia Jenerali Nicodemas Elias Mwangela alitangaza kuunda kamati maalum ya kuchunguza mradi huo.

Aidha alimuagiza mkurugenzi mtendaji wa halmashauri hiyo kumsimamisha kazi mhandisi huyo na kumtaka afisa manunuzi kuonesha vielelezo vya manunuzi.

Hata hivyo, ilidaiwa kuwa mkuu wa wilaya hiyo ya Songwe ndiye aliyechukua zabuni ya kutengeneza milango na madirisha hayo kwa kupitia kiwanda chake cha kutengeneza samani.

Aidha, ilidaiwa kuwa vifaa vya ujenzi ikiwemo mifuko ya saruji iliyokuwa ikitolewa na wadau mbalimbali kwenye halmashauri hiyo, vilitumika tofauti na matakwa ya mradi.

Hata hivyo, Mkuu huyo wa wilaya alikana kumiliki kiwanda hicho na kudai kuwa hayo ni maneno ya watu wanaotaka kumchafua.

“Ndugu wanahabari, nazungumza mbele ya viongozi hapa, mimi sijahusika na jambo hilo, ni maneno ya watu tu wanataka kunichafua,hata mkienda brela hamtakuta jina langu. Kuhusu vifaa vinavyodaiwa kuuzwa sio kweli, tusisababishe wadau waache kuchangia kwa ajili ya maneno ya watu,’’ alisema Jeremiah.

Mkuu wa mkoa wa Songwe aliahidi kuwasiliana na mkuu wa mkoa wa Mbeya ili kuangalia namna ya kumalizia miradi hiyo kwa kuwa imekaa zaidi ya miaka miwili bila kukamilika.

Brigedia Jenerali Mwangela alisema hatokuwa na huruma kwa kiongozi atakayeonekana ni mzigo katika utendaji wake.

“Serikali inawapenda watu wake na ndiyo maana inatoa fedha kwa ajili ya ujenzi wa miradi, lakini viongozi ngazi ya wilaya wanakuwa wazembe kiasi cha kusababisha madudu katika halmashauri, mmekuwa mkiendeleza migogoro na wenyeviti na wakurugenzi mnatafutiana fitna.

“Wilaya ya Songwe ni miongoni mwa wilaya iliyofanya vibaya katika utekelezaji na usimamizi wa fedha za serikali katika miradi ya maendeleo, ikifuatia na Momba na Ileje, nimeteuliwa na Rais kufanya kazi katika mkoa huu, sitokubali halmashauri kuendekeza madudu, kaeni mjitathimini fanyeni kazi kama timu, halmashauri ya Mbozi na Ileje mnaongoza kwa migogoro’’ alisema Brigedia Jenerali Mwangela

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.