CCM yaikuna TALA

Rai - - HABARI - NA MWANDISHI WETU

MWENENDO wa Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Bashiru Ally kuzungumzia umuhimu wa Serikali kupunguza migogoro ya ardhi, umelikuna taasisi ya Tanzania Land Alliance (TALA), ambalo ni jumuiko la wadau wa ardhi nchini.

Hilo limebainika katika mafunzo maalum ya kuwajengea uwezo wadau wa Ardhi kutoka asasi za kiraia yaliyotolewa na TALA, kwa kushirikiana na Serikali.

Mmoja wa watoa mada kwenye mafunzo hayo, Godfrey Massay kutoka Landesa, alisema angalau CCM kupitia Katibu Mkuu wake imeuona umuhimu wa kuondoa migogoro ya ardhi nchini.

TALA ilitoa mafunzo hayo ili wadau wa ardhi kujua hadhi na umuhimu wa kumsaidia mwananchi kumiliki ardhi kupitia program ya Land Tenure Support (LTSP) pamoja na kujua majukumu na ushiriki wa TALA na wadau wengine wa ardhi (MSG) katika kuhakikisha sera bora zinapatikana.

Katika ziara zake za hivi karibuni Dk. Bashiru alipata kusema kuwa katika uongozi wake hayuko tayari kuona kikundi cha watu wachache wenye fedha wanajilimbikizia ardhi huku wananchi wenye kipato cha chini wakiendelea kupigana na wafugaji kwa sababu ya ufinyu wa ardhi.

Kutokana na hali hiyo, alisema ataiagiza Serikali kuyapoka maeneo hayo kutoka kwa watu hao na kuwapa wananchi ili kumaliza migogoro ya ardhi inayosababisha wananchi wengi kupoteza maisha na kupata vilema vya kudumu.

Alisema Morogoro ni moja ya mkoa wenye migogoro mingi ya ardhi kati ya wakulima na wafugaji huku baadhi ya watu wakimiliki maeneo mengi bila kuyaendeleza.

“Siko tayari kuona familia nyingi za kimasikini zikiendelea kunyanyasika na matukio ya aina hiyo,” alisema

Katika hatua nyingine, alisema wananchi wengi wamekuwa wakinyanyasika katika kudai haki zao za msingi kutokana na kukithiri kwa matukio ya rushwa kwa watumishi serikalini.

Alisema CCM mpya inataka viongozi bora na si bora viongozi hivyo ni jukumu lao kuhakikisha matukio yote yenye lengo la kudhulumu haki za wananchi yanakwisha.

Pia alisema viongozi, watumishi ndani ya chama hicho na serikalini watakaoshindwa kuhudumia wananchi wajiondoe mara moja ili kuwapisha wenye kufuata na kutekeleza ilani ya CCM.

Kwa upande wake mratibu wa mafunzo hayo Bernard Baha, aliwataka wadau wa ardhi kuunganisha nguvu ya pamoja katika ushiriki wa kutoa maoni yao juu ya sera mpya ya Ardhi ambayo mchakato wake umeanza tangu mwaka 2016.

Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi imekuwa ikikusanya maoni na kuipitia upya Sera ya Taifa ya Ardhi ya 1995 ili kuiboresha. Zoezi hilo lilianza mwaka 2016 kwa kushirikisha kanda nane za Ardhi ambazo ni Kanda ya Dar es salaam, Kanda ya Mashariki, Kanda ya Kusini, Kanda ya Nyanda za Juu Kusini Magharibi, Kanda ya Magharibi, Kanda ya Kati, Kanda ya Ziwa na Kanda ya Kaskazini.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.