Madagascar walivyoweka rekodi kufuzu Afcon 2019

Rai - - MAKALA JAMOIKITOBA -

KWA mashabiki wa soka barani Afrika, uhondo ni mikimiki ya kuwania tiketi ya kushiriki fainali za Afcon 2019 ambazo zitafanyika nchini Cameroon. Michuano hiyo inatarajiwa kuanza kutimua vumbi Juni 15 na kufikia tamati Julai 13 na kwa mara ya kwanza itashirikisha timu 24 na si 16 kama ilivyokuwa hapo awali.

Wiki iliyopita, viwanja mbalimbali viliwaka moto kwa mechi za kufuzu lakini gumzo kubwa lilikuwa ni Madagascar, moja kati ya mataifa madogo kwenye uso wa dunia, likiwa na watu wasiozidi 500,000.

Kwa mara ya kwanza katika historia ya soka la nchi hiyo, Madagascar ilikata tiketi ya kucheza mashindano hayo ya Shirikisho la Soka barani humu (CAF).

Madagascar, ambao pia hawajawahi kushiriki fainali za Kombe la Dunia, waliiandika historia hiyo Jumanne, tena ikiwa ni timu ya kwanza kufuzu ukiacha Cameroon iliyopenya moja kwa moja kwa kigezo cha wenyeji.

Kujihakikisha kwenda Afcon 2019, waliichapa Guinea ya Ikweta bao 1-0, mfungaji wao katika mchezo huo akiwa ni Nijiva Rakotoharimalala anayeishi Thailand.

Wakati huo ukiwa ni mtanange wa marudiano, ule wa kwanza ambao Madagascar walikuwa ugenini, walishinda kwa matokeo kama hayo, mfungaji wao siku hiyo akiwa ni Faneva Ima Andriatsima.

Matokeo ya wiki iliyopita yaliiwezesha Madagascar kufikisha pointi 10 na kufuzu licha ya kubakiza mechi mbili za Kundi A zitakazochezwa Novemba, mwaka huu, na Machi, mwakani.

Katika safari yake, kikosi hicho cha kocha wa kimataifa wa Ufaransa, Nicola Dupuis, kilizichapa Sudan, Guinea ya Ikweta, kabla ya kulazimisha sare walipokutana na vigogo Senegal.

Dupuis raia wa Ufaransa, alikabidhiwa mikoba ya kuliongoza benchi la ufundi la timu hiyo mwaka jana, akichukua nafasi ya Auguste Raux aliyetimuliwa.

Hata hivyo, haikuwa rahisi kwa Madagascar kuitia mkononi tiketi ya kushiriki michuano ya Afcon kwani tangu mwaka 1970 imejaribu mara 18 bila mafanikio.

Kwa kiasi kikubwa, mafanikio yake yametokana na mchango wa wachezaji wake wanaocheza soka la kulipwa nje ya nchi hiyo, ambapo kikosi cha kwanza cha kocha Dupuis kinaundwa na nyota wanne wanaokipiga Ufaransa.

Pia, sita wanacheza katika mataifa ya Algeria, Ubelgiji, Misri, Reunion, Saudi Arabia na Thailand, na ni mmoja pekee anayesakata kabumbu pale Madagascar.

Katika hatua nyingine, wawakilishi wa Ukanda wa Afrika Mashariki, hasa Uganda, Kenya na Tanzania, nao wameonekana kuwa kwenye nafasi nzuri ya kwenda Afcon mwakani.

Uganda wanaoongoza Kundi L wakiwa na pointi 10, watafuzu endapo wataepuka kichapo katika mchezo wao ujao dhidi ya Cape Verde.

Matokeo hayo yatakuwa na faida pia kwa wenzao wa Tanzania kwani hapo watatakiwa kuifunga Lesotho tu ili kuzisogelea fainali hizo.

Aidha, endapo adhabu ya Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa) kwa Sierra Leone itafikia hatua ya kuiondoa Kundi F, basi itakuwa ni habari njema kwa Kenya watakaokuwa wamefuzu moja kwa moja kwa pointi saba walizonazo.

Kilichoiponza Sierra Leone ni kitendo cha serikali ya nchi hiyo kuingilia masuala ya soka, jambo ambalo linapingwa vikali na sheria za Fifa.

Huku Tanzania ikiwa haijazigusa fainali za Afcon tangu mwaka 1980, wenzao wa Kenya wamekuwa wakizitazama kupitia televisheni kwa miaka 15 sasa.

Wakati huo huo, Misri, Tunisia na Senegal zilizovurunda katika fainali za Kombe la Dunia za mwaka huu, zimeshafuzu fainali za Afcon 2019, licha ya kwamba kila moja imebakiza mechi mbili.

Nigeria wao wanahitaji pointi moja, kwa maana ya sare, katika michezo miwili iliyobaki katika Kundi E ili kujihakikishia safari ya Cameroon.

Vigogo wengine, Morocco, ambao mchezo wa wiki iliyopita uliwashuhudia wakilazimishwa sare ya mabao 2-2 na ‘vibonde’ Comoro, wanahitaji ushindi wa mechi moja kati ya mbili zilizobaki ili kwenda Afcon 2019.

Bahati mbaya kwa mashabiki wa kandanda wa Rwanda, Sudan na Sudan Kusini ni kwamba timu zao zimeshaondoshwa katika kinyang’anyiro.

UnaiNEicmoelaryDupuis

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.