Nini suluhisho vijana Uswahilini kukimbilia ‘Sauzi’?

Rai - - HABARI - NA HASSAN DAUDI

T

UKUBALIANE kuwa ukiacha utumizi wa dawa za kulevya na vitendo vingine vya kihuni, kwenda Afrika Kusini kwa ‘njia za panya’ ni upande mwingine wa maisha ya vijana wa Uswahilini.

Kila uchwao, kundi kubwa la vijana wenye umri wa kuanzia miaka 20 hadi 35, wengi wao wakiwa ni wale wenye elimu ya msingi au kidato cha nne, limekuwa likiondoka nchini kwenda huko wanakokuita ‘Sauzi’, ‘Bondeni’, ‘Ulaya ya Afrika’ au ‘Kwa Madiba’.

Binafsi niseme wazi kuwa inasikitisha kwa sababu hilo ni rika linalotakiwa kuwa aidha vyuoni au katika shughuli zingine za maendeleo ya jamii zao.

Kuliweka hilo sawa, si kwamba napingana na suala la kwenda Afrika Kusini au kwingineko kutafuta maisha ila siridhishwi na namna wanavyosafiri na hata kuyaweka hatarini maisha yao.

Kama nilivyoeleza hapo juu, vijana hao hutumia njia zisizo halali, ambazo huwafanya kusafiri muda mrefu, tena hata usiku na mchana, sababu kubwa ikiwa ni kukwepa gharama na vikwazo vingine.

Kubwa zaidi ya hilo, nimekuwa nikikwazwa na namna vijana hao wanavyoondoka nchini wakiwa hawana maandalizi ya kuridhisha.

Si tu huenda huko wakiwa hawana fedha za kutosha, elimu, wala ujuzi wowote utakaowawezesha kuajiriwa, wengi wao huwa hawana mahala pa kufikia.

Kwa namna moja au nyinginge, changamoto hizo huwafanya wajiingize katika matukio ya kihuni wafikapo huko, ikiwamo kuiba, mapenzi ya jinsia moja, au hata kuuza na hata kutumia dawa za kuevya.

Mfano; tumeshuhudia mara kadhaa baadhi ya vijana waliokwenda huko wakirejea wakiwa ‘mateja’ au wezi, maisha ambayo hawakuwa nayo hapo awali.

Kuongezea katika hilo, ipo mifano mingi ya waliopatwa na matatizo ya afya ya akili kutokana na msongo wa mawazo baada ya kukumbana na hali ngumu ya kimaisha huko ughaibuni.

Pia, hata waliorejea wakiwasawakiakili,hujikuta wakichanganyikiwa wanapowaonna wenzao waliowaacha hapa nchini wamewazidi kimaendeleo baada ya wao kupoteza muda mwingi ughaibuni.

Kwa mazingira hayo basi, naamini jitihada za makusudi zinatakiwa kuchukuliwa kuiokoa nguvu kazi inayoteketea kila iitwayo leo kutokana na safari hizo.

Tofauti na ilivyozoeleka, ambapo Serikali imekuwa ikiachiwa mzigo huo mzito, binafsi naamini tatizo linaanzia katika jamii.

Ukweli ni kwamba wazazi, ndugu, jamaa au marafiki wamekuwa wakishuhudia mwanzo hadi mwisho mipango hiyo ya vijana wao wanaohangaikia njia za mkato kwenda Afrika Kusini.

Aidha, kama si kuwasaidia kwa fedha, watu hao wa karibu wamekuwa wakiishia kulalamika, wakishindwa kushirikiana na jeshi la polisi kudhibiti matukio hayo. Endapo jamii itaanza, basi tatizo hilo halitachukua kitambo kutokomea na kubaki historia.

Nikirejea kwa Serikali, uwekezaji mkubwa unatakiwa katika kuelimisha vijana wa mitaani, nikiamini kuwa huenda wengi wao hukimbilia ‘Sauzi’ kutokana na upotoshaji wa wenzao walioko huko.

Aidha, hilo la elimu linaweza kwenda mbali zaidi, likielekezwa katika kuwajenga kisaikolojia vijana waliokataa tamaa baada ya kukosa ajira, ambao kimsingi ndiyo huvutiwa na safari za ng’ambo kujaribu ‘zali’ (bahati) lao.

Vilevile, hilo la utitiri wa vijana wanaokimbilia nje kusaka maisha linapaswa kuchochea kasi ya mikakati iliyopo ya kukabiliana na changamoto ya uhaba wa ajira nchini.

Nisisitize kwamba si tu jitihada zinatakiwa katika ongezeko la vyuo vya ufundi, bali pia gharama za elimu hiyo zinapaswa kuwa rafiki kwa wazazi wenye kipato duni kwani watoto wao ndiyo wahusika wakubwa wa safari hizo za Afrika Kusini.

Itoshe kwa leo kukuandikia, hadi wiki ijayo.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.