TFF ishushe rungu kwa wanaopuuzia Leseni za klabu

Rai - - MICHEZO - NA MWANDISHI WETU

TAKRIBANI miaka misimu mitano sasa ya Ligi Kuu ya Tanzania Bara kumekuwepo na mkakati wa utekelezaji wa agizo la Shirikisho la Soka barani Afrika (CAF), kuhusiana na mfumo au utaratibu ambao unaozihitaji klabu kuwa na sifa kamili ili kushiriki mashindano mbalimbali.

Kwa kawaida leseni hizi hutolewa na chama kinachosimamia mchezo wa soka katika nchi husika kwa kufuata mfumo uliowekwa na CAF ambapo kwa hapa Tanzania ni TFF.

Toka agizo hilo litangazwe bado utekelezaji wake umekuwa wa kusua sua ambapo klabu nyingi hapa nchini vimeshindwa kwua na mipango thabiti ya kuweza kuvimiliki viwanja vyao binafsi na badala yake kuishia kuchangia matumizi katika viwanja vinavyomilikiwa na Chama cha Mapinduzi au serikali.

Mwenyekiti wa Kamati ya Leseni za klabu Wakili, Lloyd Nchunga, amesema kuwa timu zote ambazo hazitakidhi vigezo vya kupewa leseni hadi kufikia muda wa dirisha dogo la usajili, hazitashiriki michuano ya Ligi Kuu na ikiwezekana timu hizo zitashushwa daraja.

Kuna mambo matano (5) makubwa kwenye Leseni ya klabu ambapo ili klabu iweze kushiriki mashindano ni lazima iwe nayo.

SUALA LA KIMICHEZO

Klabu iwe na mpango wa maendeleo ya soka la vijana na mpango huo uwe umepitishwa na idara ya ufundi ya TFF. Maana yake klabu iwe na timu za vijana zisizopungua mbili, moja iwe ya miaka kati ya 19-21 nyingine kati ya miaka 15-17 na zote ziwe na mabenchi yake ya ufundi yanayojulikana siyo makocha wanashuka chini na kupanda juu.

MIUNDOMBINU

Kila klabu iwe na uwanja wake wa mazoezi ambapo siyo lazima klabu iwe inamiliki uwanja binafsi, inaweza ikakodi lakini ni lazima ipeleke mkataba wa makubaliano hayo. Lazima klabu iwe na uwanja wake wa nyumbani kwa ajili ya mechi za ligi, kama klabu haina uwanja wake basi iwe na mkataba unaoonesha uwanja wake wa kukodi itakaoutumia kama uwanja wa nyumbani.

Viwanja hivyo lazima viwe aina mbili kimoja kitumie nyasi bandia yenye viwango bora na kuthibitishwa na Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA) na CAF, na kingine chenye nyasi za kawaida.

Katika kipengele cha uwanja, lazima kuwepo na chumba ambacho kinamfanya mtu kuona uwanja wote ulivyo na idadi maalumu ya mashabiki wanaoingia uwanjani. Pia uwanja unatakiwa kuwepo na taa pamoja na uzio unaotenganisha sehemu ya wachezaji na mashabiki.

Pia kuwepo na chumba cha huduma ya kwanza na chumba maalumu kwa ajili ya matibabu au kuwepo na gari ya huduma ya kwanza uwanjani. Kwani kuna wachezaji wengi hawatakiwi kupewa huduma ya kwanza bali kukimbizwa hospital moja kwa moja.

Uwanja huo uwe na sehemu ya kukaa wageni (VIP) na sehemu maalumu kwa ajili ya waandishi wa habari. Aidha ipo haja ya uwanja kuwa na sehemu rafiki kwa

walemavu.

UMILIKI WA KLABU

Hii ni sehemu mojawapo muhimu ambapo inatakiwa kujulikana nani ni mmiliki hasa wa klabu husika. Klabu inatakiwa iwe na utawala ambapo shughuli za utendaji zinakuwa chini ya katibu mkuu.

Katika mfumo huu mmiliki wa klabu haruhusiwi kumiliki klabu zaidi ya moja.

WATENDAJI WA KUAJIRIWA

Watendaji wanatakiwa wawe na sifa za kuwa watendaji wenye sifa sahihi kama vile taaluma husika, kama ni afisa habari basi awe na taaluma ya habari, mtu wa fedha lazima awe na taamula ya masuala ya fedha vilevile mtu wa utawala.

MASUALA YA KISHERIA

Klabu iwe na katiba yake inayotambulika na mambo yake yote ya kiutendaji yafate katiba inavyotaka, yaani lisifanyike jambo lolote nje ya katiba.

MASUALA YA FEDHA YATAMBULIKE

Lazima ifahamike vyanzo vya mapato vya klabu husika. Klabu inatoa wapi pesa na inatumia kwa namna gani. Lazima kuwe na ripoti ambayo imekaguliwa na wakaguzi waliosajiliwa kutoka nchi husika. Klabu inatakiwa isiwe na deni lolote linatokana na usajili, klabu isiwe inadaiwa kodi na mamlaka ya kiserikali na mishahara wanayolipwa wachezaji na wafanyakazi wengine kodi iwe inalipwa.

Mpaka sasa klabu nyingi za hapa nchini wamejitahidi kutekeleza suala la viwanja ingawa nyingi wameingia mikataba na wamiliki ambao ni Chama cha Mapinduzi au serikali.

Klabu chache sana zina viwanja vyao vya mechi kama vile Azam (Chamazi), JKT Ruvu (Meja Isamuhyo Mbweni), Ruvu Shooting (Mabatini Pwani), Mtibwa (Manungu).

CAF kw kutambua umuhimu wa suala hilo katika kurahisisha maendeleo ya mpira, ilimteua Rais wa zamani wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Leodegar Tenga, kuwa Rais wa Kamati ya Usimamizi wa Mfumo wa Leseni ya Klabu (Management of Club Licensing system) akisaidiwa na Rais wa Shirikisho la Soka Afrika Kusini, Danny Jordan.

Wakati sual;a hili linaonekana kutiliwa mkazo hivi sasa na CAF je nini hatima ya klabu nyingi za Tanzania ambazo bado ziko nyuma sana katika utekelezaji wa suala hilo la leseni za klabu?

Hata hivyo inaweza kuwa ‘mtihani’ mkubwa kwa Tenga ambaye amekabidhiwa idara hiyo nyeti inayoshikilia hatima ya soka kuchezeka huku nchi anayotoka ikiwa na changamoto kubwa ya kutimiza vigezo hivyo.

Lakini kwa kuwa tayari Mwenyekiti wa Kamati ya Leseni za klabu Wakili Nchunga, ametoa tahadhari hiyo ni jukumu la klabu husika wanatumia muda mfupi uliobaki ili kukamilisha utaratibu huo kabla ya rungu kutua.

Katika hili TFF wanapaswa kukunjua meno na kuwaadhibu watakaokiuka ili kuzifanya kwenda na kasi ya maendeleo kama ilivyo nchi zingine.

Uwanja wa Taifa Dar es Salaam ukifanyiwa marekebisho mara kwa mara ili kuhimili mechi nyingi za mfululizo

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.