Bunge la 11 mwisho wa wabunge wengi CCM

CHAMA CHA MAPINDUZI ambacho sasa kinajipambanua kama CCM, kinatajwa kuwaweka mashakani wabunge wake wengi hasa wale waliokuwa karibu na chama miaka ya nyuma. RAI linachambua.

Rai - - MBELE - NA MWANDISHI WETU

CHAMA CHA MAPINDUZI ambacho sasa kinajipambanua kama CCM, kinatajwa kuwaweka mashakani wabunge wake wengi hasa wale waliokuwa karibu na chama miaka ya nyuma. RAI linachambua.

Mwenendo wa mambo ndani ya CCM kwa sasa unawatenga kabisa makada wake ambao wananyadhifa za ubunge, lakini walipata kuhudumu kwa karibu ama kwa mbali ndani ya chama.

Wabunge hao ambao baadhi yao wanatajwa kuwa wakosoaji wakubwa wa serikali ya awamu ya Tano, wananafasi ndogo ya kurudi bungeni baada ya Bunge la 11 kufikia tamati kutokana na kuzalishwa kwa mfumo mpya wa uteuzi wa wagombea ubunge, ambao hauhitaji uamuzi wa watu wengi.

Kwa sasa majina ya wagombea ubunge yanateuliwa na Kamati Kuu Maalum ya Halmashauri Kuu ya Taifa.

Tayari mfumo huo umeshaanza kutumika katika chaguzi ndogo za marudio, wabunge wote waliohama kutoka kwenye vyama vyao na kujiunga na CCM, akiwemo James Ole Millya, Dk. Godwin Mollel, Mwita Waitara, Pauline Gekuli, Maulid Mtolea wamerudishiwa majimbo yao na wengine kuteuliwa kuwania tena nafasi hizo kwenye majimbo hayo hayo waliokuwapo awali.

Aidha, CCM mpya inatajwa kujikita katika mfumo wa kuondoa utaratibu wa makada wake kudhani wao ni muhimu zaidi ya w engine na ndio maana sasa inatoa nafasi kwa makada wanaojiunga kupewa nafasi za uongozi wa kuchaguliwa ama wa kuteuliwa.

Anguko la makada hao wa CCM haliishia kuwagusa wabunge waliokuwa karibu na chama katika tawala zilizopita pekee, lakini pia linatawakamata baadhi ya wabunge walioonesha na wanaoonesha kuendelea kuwa na matamanio ya urais au walijiingiza kwenye makundi ya wawania urais.

Uwezekano wa kufanikisha hatua ya kuwabana makada hao unaongezewa nguvu na kasi ya kiutendaji ya Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk. Bashiru Ally ambaye anaonekana dhahiri kuibeba vema agenda ya CCM mpya inayojali utu zaidi ya kitu na inayokemea ufisadi.

Mara kadhaa katika hotuba zake Dk. Bashiru amekuwa akiukemea ufisai na mafisadi na kuweka wazi kuwa kamwe hawatakuwa tayari kuwaacha mafisadi na majizi yatambe.

Mbali na hayo lakini pia hali ya mambo ndani ya chama kwa sasa inaonesha wazi kuwa namna pekee ya kushughulika na wabunge hao pamoja na makada wengine ambao si wabunge, lakini walikuwa na ushawishi ndani ya CCM, ni kuwaondolea nguvu kwa kuuweka hadharani ushiriki wao katika kuzihujumu mali za chama.

Tayari Dk. Bashiru ameshasema kuwa makada wake wote waliohujumu mali za chama kwa maslahi yao binafsi watasafishwa mmoja baada ya mwingine bila kujali majina ama vyeo vyao.

Dk. Bashiru ambaye amenukuliwa mwishoni mwa wiki iliyopita na moja ya magazeti ya chama hicho, alisema CCM imedhamiria kusimama kwenye yake na hivyo haina nafasi ya kuwa na watu majizi.

Ukweli wa hoja ya wabunge wengi wa CCM kuwa na nafasi ndogo ya kurejea bungeni kwenye Bunge la 12, unadhihirishwa na kauli yake ya hivi karibuni kwa moja ya magazeti ya CCM, kuwa mkakati wa kushughulika na makada hao utaanzia kwenye kura za maoni za kusaka nafasi mbalimbali kwenye uchaguzi Mkuu ujao wa mwaka 2020.

Timu ya uchunguzi wa mali za chama hicho inaelezwa kuwa imegundua mambo mengi machafu ikiwemo uchukuaji wa magari, viwanja, shule za jumuiya ya wazazi na majengo ya biashara ya chama hicho.

Katika kuhakikisha makada hao ambao baadhi yao ni wabunge, Dk. Bashiru alisema hawatasalimika pamoja na kuwa na majina makubwa katika ulingo wa siasa nchini.

Mbali na kuwasubiri kwenye harakati za kutafuta nafasi ya kuwania uongozi, lakini pia hawataachwa salama kwani tayari umeandaliwa mkakati wa kuwashughulikia katika mikutano ijayo ya Bunge.

Wabunge hao wa CCM salama yao kwa sasa itakuwa ni kusalia kwenye mikutano na vikao vyote vya Bunge pamoja na kusikiliza na kutatua kero za wapiga kura wao.

Wale watakaoendeleza utaratibu wa mazoea wa kutokaa bungeni watachukuliwa hatua stahiki, zitakazowalazimisha kujitafakari mara mbili kama wanatosha kuwamo ndani ya chama hicho.

Imeelezwa kuwa taarifa za utoro wa baadhi ya wabunge wa chama hicho, tayari ziko mezani kwa Katibu Mkuu huyo, lakini chama hakitamshughulikia mtu bila kuwa na vielelezo vya kutosha, ambavyo vinaendelea kukusanywa.

“Kila mbunge wa CCM ana ukurasa wake kwangu wa jinsi anavyochangia bungeni, kuhudhuria vikao, kujenga chama, anafanya mikutano ya hadhara nakadhalika, 2020 tutampa ukurasa wake,”alinukuliwa Dk. Bashiru.

Wafuatiliaji na wachambuzi wa siasa nchini wanaamini kuwa hatua ya CCM kuondoa mfumo wa baadhi ya watu kujiona wao ni zaidi utasaidia kuleta heshima ndani ya chama hicho.

James Ole Milya Dk. Bashiru Ally

Dk. Bashiru Ally

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.