JET, Marekani waungana kulinda hifadhi

Rai - - HABARI - NA MWANDISHI WETU

CHAMA cha Waandishi wa Habari za Mazingira Tanzania (JET), kwa kushirikiana na Shirika la Misaada la Marekani (USAID), wameamua kushiriki kikamilifu kwenye vita ya kuendeleza na kulinda mazingira.

USAID inashiriki kwenye vita hiyo kupitia mradi wake wa kuendeleza Mazingira, Uhifadhi na Utalii Tanzania (PROTECT).

Katika kuhakikisha vita hiyo inafanikiwa JET na USAID PROTECT wametoa mafunzo maalum kwa waandishi wa habari 30 wa Tanzania, lengo likiwa ni kuwaongezea uwezo katika kuripoti kwa kina habari zote zinazohusu masuala ya mazingira, uhifadhi, ujangili na usafirishaji haramu wa wanyamapori.

Mafunzo hayo yaliendeshwa kwa siku tatu na wakufunzi mbalimbali waliobobea kwenye masuala ya uandishi hasa wa mazingira na uhifadhi, akiwemo mwanahabari nguli Atilio Tagalile, Radhia Mwawanga na Katunzi.

Mafunzo hayo yaliyofanyika Bagamoyo mkoani Pwani, yametajwa na baadhi ya washiriki kuwa na umuhimu mkubwa kwa sekta ya uhifadhi wa mazingira na wanyama nchini, kwangu Watanzania walio wengi wanaamini masuala hayo hayawahusu.

Said Mwishehe, kutoka Michuzi Blog alieleza kuwa, kwa kiasi kikubwa mafunzo hayo yamemwongezea uwezo wa kuujua umuhimu way eye kushiriki moja kwa moja katika kuandika habari za sekta hiyo kwa weledi.

“Tunapaswa kuyajua haya masuala kwa kina, nimegundua kuwa kila Mtanzania nikiwemo mimi tunapaswa kushiriki kikamilifu katika kulinda na kuhifadhi mazingira na wanyamapori,”alisema.

Lucy Lyatuu kutoka Habari Leo (TSN), alisema kwake amepata faida kubwa ambayo anaamini itamsaidia kuripoti kwa weledi masuala yanayohusu mazingira na wanyamapori.

Akizungumza na RAI, Mkurugenzi Mtendaji wa JET, John Chikomo, alisema kuwa chama hicho kimejipanga kuhakikisha kinakuwa sauti ya kweli ya Mazingira. Alisema kwa kuanzia wameiona haja ya kuwapa mafunzo waandishi wa habari kisha watayaelekeza mafunzo hayo kwa Wahariri, lengo likiwa ni kupata sauti ya pamoja katika kuripoti habari za mazingira na uhifadhi.

Alisema katika kufikia malengo hayo wameuona umuhimu wa kushirikiana na USAID PROTECT ili kuwajengea uwezo wanahabari kutoka mikoa mbalimbali nchini.

Alibainisha kuwa kiu ya JET kwa sasa ni kuona Tanzania inakuwa kimbilio kubwa la watalii kutoka maeneo mbalimbali duniani, hatua itakayosaidiua kuingiza fedha nyingi za kigeni, pamoja na kuunga mkono jitihada za Rais John Magufuli za kutaka nchi ifike hmahali ijitegemee.

“Jukumu letu ni kupaza sauti ya juu ya ulinzi na uhifadhi wa mazingira, kwa kiasi kikubwa tumefanikiwa kupaza sauti yetu kwenye maeneo mbalimbali, lakini tumeona haitoshi ni vema kama tutatanua wigo kwa kuangalia ni namna gani tutakuwa na sauti ya pamoja katika kukemea uwindaji, usafirishaji haramu na hifadhi za wanyama,”alisema Chikomo.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.