Itakuwa ngumu Conte kwenda Real Madrid

Rai - - MBELE -

HIVI sasa kikosi cha Real Madrid kiko chini ya kocha wa muda, Santiago Solari, ambaye kabla ya kupewa nafasi hiyo alikuwa akiinoa timu ya vijana. Baada ya kumtimua Julen Lopetegui, bado Madrid wanaendelea na harakati za kusaka atakayekikalia kiti chake

Lakini sasa, wachambuzi wa soka barani Ulaya wanaamini huenda Conte akaikataa ofa yoyote atakayowekewa mezani na mabosi wa Madrid. Kwanini?

Kwanza, mkufunzi huyo haonekani kuwa tayari kurejea haraka katika soka, hasa baada ya changamoto aliyokutana nayo msimu uliopita akiwa na Chelsea.

Kuinoa Madrid ni moja kati ya vibarua vigumu katika soka kutokana na klabu hiyo kuwa na utamaduni wa kutimua makocha mara kwa mara.

Kuingia katika kazi iliyowahi kuwashinda makocha wenye CV kubwa katika ulimwengu wa kandanda, Vicente del Bosque, Fabio Capello na Jose Mourinho, inahitaji ujasiri, jambo ambalo kwa sasa Conte anaweza asiwe nalo baada ya kutimuliwa Chelsea.

Conte mwenye umri wa miaka 49, hajapumzika tangu alipoanza kazi ya ukocha mwala 2007, hivyo kile kilichomkuta pale Chelsea, ikiwamo kukorofishana mara kwa mara na wachezaji, inaweza kuwa sababu nzuri ya kutaka kukaa mbali na soka, walau kwa muda kidogo.

Hata katika moja ya mazungumzo yake na waandishi wa habari, aliwahi kuweka wazi kuwa haoni kama atakuwa mkuu wa benchi la ufundi hivi karibuni.

Pili, kuna hili la kibarua pale Manchester United. Ikizingatiwa kuwa Ligi Kuu ya England (EPL) imekuwa ikiwavutia wanasoka, makocha na mashabiki wengi, si ajabu hata Conte anatamani kubaki. Akiwa anajua kabisa kwamba mwenzake, Jose Mourinho, ana wakati mgumu katika kibarua chake cha kuinoa Man United, Conte anaamini anaweza kuitwa Old Trafford.

Ni kweli mkataba wake na Chelsea haumruhusu kufanya kazi England hadi pale msimu huu utakapomalizika lakini kama ni Man United atakuwa tayari kusubiri hata mwakani.

Kuna taarifa kuwa amekuwa akiamini kuwa ndiye atakayepewa kazi ya kuliongoza benchi la ufundi la Mashetani Wekundu, ingawa hilo litategemea na mwenendo wao chini ya Mourinho.

Bado Mourinho ana mkataba na kama timu itakuwa kwenye kiwango kizuri kwa miezi sita ijayo, hakuna ubishi kuwa mabosi wa Man United hawataona umuhimu wa kumfukuza kocha huyo wa kimataifa wa Ureno.

Tatu, inaonekana ni ngumu kwa Conte kwenda Madrid kutokana na ukweli kwamba baadhi ya mastaa wa Santiago Bernabeu hawamtaki.

Pindi tu zilizoibuka taarifa zilizomtaja Conte kuwa ndiye atakayekuwa kocha wao, walionesha wazi kutokubaliana na suala hilo.

Orodha ya wachezaji wanaopinga kuwa chini ya Conte haijawekwa hadharani lakini inafahamika kuwa Madrid ina Sergio Ramos, Marcelo Toni Kroos ambao wanatajwa kuwa na ushawishi mkubwa kikosini na hata kwa mabosi.

Inaelezwa pia sehemu ya wasiomtaka kocha huyo ni wale wanaoamini kuwa ujio wake utawanyima nafasi ya kucheza mara kwa mara. Mfano; hakuna ubishi kuwa Keylor Navas hatakaa langoni kwa kuwa Thibaut Courtois na Conte wanajuana vizuri tangu walipokuwa Chelsea.

Katika hilo, hata Gareth Bale anaweza asifurahishwe na ujio wa Conte, akijua wazi kwamba kocha huyo atataka Eden Hazard asajiliwe, jambo linaloweza ‘kuuzika’ ufalme wake Bernabeu.

Kama si Hazard aliyewahi kufanya naye kazi Stamford Bridge, Conte anaweza kuwashawishi Madrid wamuuze Bale ili kiasi cha fedha kitakachopatikane kiongezewe kumvuta Neymar.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.