Wanamsumbiji waadhimisha miaka 30 ya kifo cha Samora Bagamoyo

Uhuru - - Mbele - NA CHRISTOPHER LISSA

JUMUIYA ya wananchi wa Msumbiji waishio nchini, (COMORETA), jana waliungana na Watanzania katika kuadhimisha miaka 30 ya kifo cha Rais wa kwanza wa taifa hilo, Hayati Samora Machel.

Katika maadhimisho hayo, COMORETA, walizuru eneo la Kaole, wilayani Bagamoyo, mkoani Pwani, ambapo kulikuwa na kambi maalumu ya wapigania uhuru wa taifa hilo, chini ya chama cha ukombozi cha FRELIMO, ambapo katika kambi hiyo Hayati Machel, aliwahi kuishi na kupata mafunzo.

COMORETA iliungana na Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuadhimisha siku hiyo, kupitia Jumuiya ya Wazazi, ambapo kwa pamoja walitembelea eneo hilo ambalo hivi sasa kuna Chuo cha Kilimo na Mifugo kinachomilikiwa na Jumuiya ya Wazazi ya CCM.

Wakiwa katika eneo hilo, walitembelea majengo ya kihistoria, ikiwemo nyumba aliyokuwa akiishi Hayati Machel, ambayo ina pango la ndani kwa ndani, sehemu ambayo mashujaa wa FRELIMO walikuwa wakisafishia bunduki, uwanja ambao walikuwa wakifanya mazoezi ya kijeshi na sehemu zingine muhimu.

Kiongozi wa msafara huo, ambaye pia ni mmoja wa wapigania uhuru wa FRELIMO, Paul Matete Lekanone, alisema wanatambua mchango mkubwa wa taifa la Tanzania katika ukombozi wa Msumbiji na bara la Afrika.

“Maadhimisho ya miaka 30 ya Hayati Machel ni muhimu katika historia ya ukombozi wa taifa letu la Msumbiji na bara la Afrika. Tanzania ilitupa hili eneo la Kaole Bagamoyo ili tufanye kambi kubwa ya mashujaa wa FRELIMO waliokuwa wanaendesha harakati za ukombozi. Hapa aliishi Machel na kupata mafunzo, kisha kuwaongoza wanamsumbiji kulikomboa taifa letu,” alisema Lekanone.

Alisema, yapo maeneo mengi hapa nchini ambayo Tanzania chini ya Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere, waliyatoa kwa ajili ya harakati za ukombozi wa Msumbiji, hali inayodhihirisha undugu uliopo baina ya mataifa hayo mawili.

Kwa upande wa Katibu wa FRELIMO Ukanda wa Tanzania Bara, Bosco Fereji, aliiomba CCM kubadili jina la Chuo cha Wazazi cha Kilimo na Mifugo Kaole, ili kiitwe Samora Machel ikiwa ni kuenzi historia ya eneo hilo.

“Tubadilishe jina ili historia hii isije kupotea na iweze kurithishwa kwa vizazi vingine,” alisema Fereji.

Naye Naibu Katibu Mkuu Jumuiya Wazazi Bara, Edwin Millinga, alisema CCM itaendelea kuenzi ushirikiano baina yake na FRELIMO na kuhakikisha maeneo yote ya kihistoria ambayo wapigania uhuru wa taifa hilo yaliyopo nchini yanasimamiwa kikamilifu.

“Lakini pia tutafikiria ombi lenu la kutaka chuo hiki kiitwe Samora Machel. Tutalifikisha katika ngazi husika na tunaamini litafanyiwa kazi,” alisema Milinga.

Katibu wa Wazazi Wilaya ya Bagamoyo, Aeshi Khatibu, alipongeza ziara hiyo ya COMORETA katika eneo la kihistoria la Bagamoyo na kwamba imeongeza ari ya kuyalinda na kuyaenzi maeneo hayo ya kihistoria.

Machel alifariki dunia katika eneo la Mbuzini, nchini Afrika Kusini, kwa ajali ya ndege Oktoba 19, mwaka 1986.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.