Mtuhumiwa aiomba mahakama imwachie huru

Uhuru - - Habari - NA LILIAN JOEL, ARUSHA

SHAHIDI wa pili, ambaye pia ni mtuhumiwa wa pili katika kesi inayomkabili aliyekuwa Mkurugenzi wa Mamlaka ya Ngorongoro, Bernad Murunya, ameieleza Mahakama ya Wilaya ya Arusha kuwa, Dola za Marekani 66,227, zilizolipwa kwa Kampuni ya Cosmos Travel, wahusika hawakusafiri.

Aidha, shahidi huyo, Veronica Ufunguo, alisema waliotakiwa kusafiri katika safari hiyo, alikuwa Murunya, Waziri wa Maliasili na Utalii wakati huo, Ezekiel Maige na aliyekuwa msaidizi wa waziri, Elgius Muyungi.

Katika kesi hiyo iliyokuwa inasikilizwa na Hakimu wa mahakama hiyo, Paricia Kisinda, shahidi Veronica, ambaye alikuwa mtumishi wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro tangu mwaka 2010-2013, kama meneja wa huduma za utalii, akiongozwa na wakili Boniface Joseph, alisema fedha hizo zilitumika kufidia safari nyingine mbili tofauti, ambazo zilihusisha watu watano.

Veronica alidai mahakamani kuwa, waliosafiri kufidia safari hiyo kwenda kwenye maonyesho ya utalii Canada ni pamoja na aliyekuwa Naibu Spika wa Bunge, Job Ndugai, Peter Makutiani, Yusuph Maimu ma Doantus Kamamba.

Aidha, alidai safari nyingine ilikuwa ya aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa mamlaka hiyo, Murunya, ambaye alisafiri kwenda Korea

Kwa mujibu wa Veronica, aliandaa safari hiyo baada ya kupata maelekezo ya maandishi kutoka kwa Mkurugenzi wa Fedha na Utawala, Shad Kyambile ya kuandaa tiketi tatu za ndege, posho na masurufu ya safari.

Baada ya maelezo hayo, wakili wake alimweleza Veronica kuwa, anatuhumiwa kukiuka taratibu za manunuzi na kusababishia mamlaka hasara, jambo ambalo Veronica alisema sio kweli kwani baada ya mchakato wa kupata kampuni ya kutoa huduma za usafiri, aliangalia kwa kina kampuni iliyokuwa na gharama nafuu za tiketi, ambayo ilikuwa Cosmos.

Alidai kampuni huyo ilikuwa na gharama ya dola 66,890, huku Kampuni ya Antelope ikiwa na gharama ya dola 69,227.

Veronica aliendelea kudai kuwa, kesi hiyo inatokana na ukaguzi maalumu uliofanyika kutokana na safari hiyo, ambapo wakaguzi hao walimkuta ofisini, lakini hawakumtendea haki kwa kuwa hawakumuuliza chochote.

Aidha, aliendelea kudai kuwa, wakati anahojiwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKUKURU) mkoa wa Arusha, kuna taarifa ya ufafanuzi aliomba itumike, lakini walimkatalia

Baada ya maelezo hayo, Veronica aliiomba mahakama kumwachia huru na kwamba, alitakiwa kupongezwa kwa kazi nzuri aliyoifanya ya kuchagua kampuni, ambayo ilikuwa na gharama nafuu za usafiri na kwamba, hakulisababishia shirika hasara.

Hakimu aliahirisha keshi hiyo mpaka leo, ambapo mashahidi wengine wawili wa upande wa utetezi watatoa ushahidi wao.

Licha ya Murunya, Veronica, ambaye ni Meneja Utalii wa mamlaka hiyo, washtakiwa wengine ni Salha Issa, aliyekuwa Mkurugenzi wa Kampuni ya Uwakala wa Usafirishaji ya Cosmas (Cosmas Travelling Agent) na Mkurugenzi wa Fedha na Utawala wa mamlaka hiyo, Shad Kyambile.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.