Wanafunzi vyuo vikuu waruhusiwa kulipa nusu ada

Uhuru - - Habari - NA EMMANUEL MOHAMED

VYUO vikuu nchini vimewaruhusu wanafunzi kuingia madarasani kuendelea na masomo huku wakipewa masharti ya kulipa nusu ya ada ndipo waweze kujisajili, wakati wakisubiria taarifa ya uhakiki ya Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu (HESLB).

Hali hiyo inatokana na HESLB, kutoa orodha ya wanafunzi 3,966, wanaotarajiwa kunufaika na mikopo hiyo, kati ya 58,000, wanaojiunga na elimu ya juu mwaka huu.

Oktoba 14, mwaka huu, serikali ilitangaza uamuzi wa kubadilisha vipaumbele kwa wanufaika wa mikopo, ikiwemo fani za masomo ya sayansi za tiba na afya, ualimu wa sayansi na hisabati, uhandisi wa viwanda, kilimo, mifugo, mafuta na gesi asilia.

Vipaumbele vingine ni kwa masomo ya sayansi asilia na mabadiliko ya tabianchi, sayansi za ardhi, usanifu majengo na miundombinu na kwa wahitaji wenye mahitaji maalumu kama vile walemavu na yatima na ufaulu wa waombaji katika maeneo ya vipaumbele na umahiri.

Gazeti hili lilitembelea Chuo Kikuu cha Dar es Saalam (UDSM) na Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu Dar es Saalam (DUCE), ambapo lilishuhudia kusitishwa kwa usajili wa masomo ya mwaka huu, kutokana na HESLB kusitisha mikopo kwa wanafunzi hao kwa ajili ya kupitia upya vigezo vya utoaji wa mikopo.

Akithibitisha kutokea kwa hali hiyo, Juma Hamisi, ambaye ni mwanafunzi wa mwaka wa tatu, anayesomea shahada ya uhandisi wa viwanda, alisema alikataliwa kusajiliwa na kusubiri orodha ya majina mapya ya wanufaika wa mikopo yatakayotolewa na HESLB.

“Usajili wa masomo yangu ya mwaka wa mwisho yamesitishwa hadi bodi itakapotoa majina mapya, yaani kutokana na hivi karibuni serikali imebadilisha vipaumbele vya utoaji wa mikopo, hivyo nasubiria kuhakikiwa upya jina langu ndipo nijue napata kwa asilimia ngapi,” alidai.

Kwa upande wake, Ofisa Mikopo wa wanafunzi wa DUCE, Salmon Daudi alieleza kuwa chuo hicho kimesitisha usajili wa masomo ya mwaka huu kwa wanufaika hadi HESLB itakapowasilisha majina mapya, lakini wanaruhusiwa kulipa nusu ada ndipo wasajiliwe.

“Chuo kimeruhusu wanafunzi kuendelea na masomo bila tatizo na kwamba wanafunzi wameanza masomo Oktoba 17, mwaka huu.

Hata hivyo, wapo wanafunzi ambao wamekwishalipa nusu ada yaani ada ya masomo ya sayansi ni shilingi milioni tatu na ya sanaa ni sh. milioni moja,” alifafanua.

Daudi alisema wanafunzi ambao wamekwishalipa nusu ada, wameruhusiwa kujisajili na kwamba, kwa upande wa chuo hakina shida ya kuwaruhusu wanafunzi kuendelea na masomo na wanafunzi wa mwaka wa kwanza tayari wameanza masomo.

Mwanahamisi Shaaban, mwanafunzi wa mwaka wa kwanza, ambaye anasomea masomo ya sayansi kutoka DUCE, alidai ameshindwa kujisajili kutokana na HESLB kushindwa kutoa orodha ya majina ya wanufaika na kwamba, amelipa nusu ada ya sh.milioni tatu.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.