Ukurasa wa facebook wa Profesa Tibaijuka waingiliwa na matapeli

Uhuru - - Habari - NA MWANDISHI WETU

MBUNGE wa Jimbo la Muleba Kusini (CCM), Profesa Anna Tibaijuka, ametoa tahadhari kwa wananchi kwamba, ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Facebook, umeingiliwa na matapeli ambao wanatoa taarifa za uongo.

Profesa Tibaijuka alitoa tahadhari hiyo jana, alipozungumza na Uhuru, kuhusu kuwepo kwa matapeli hao, ambao wanawadanganya wananchi kwamba, anatangaza nafasi ya kazi ya kujiunga na taasisi isiyo ya kiserikali, inayosaidia watu waliopo kwenye wimbi la umasikini Afrika.

Alisema ukurasa huo wa Facebook siyo wa kwake na haufahamu na kwamba, taarifa zote zinazoandikwa ni za uongo na hazitoki kwake.

“Waliotengeneza ukurasa huu ni matapeli na wanatafuta kuchafua jina langu na kuwatapeli watu,” alisema.

Mbunge huyo aliyewahi kuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, aliwaomba Watanzania kupuuza taarifa hizo na wasitume taarifa zao kupitia barua pepe kama inavyoelekeza.

Profesa Tibaijuka aliwaomba wawe makini wakati huu, ambapo taarifa zimekwishafika kwenye vyombo vya usalama na wanaendelea na uchunguzi ili kuwabaini wahusika na kuwatia mbaroni.

Katika mtandao huo, unaotumiwa na matapeli hao, wanadai watu watume wasifu wao kutumia annatibaijuka200@ gmail.com au kutembelea website isemayo https://www.one.org/africa.

Mbunge huyo kwa sasa yupo nchini Ecuador, akihudhuria mkutano wa Umoja wa Mataifa, unaohusu makazi na maendeleo endelevu, ambao ulianza Jumatatu iliyopita na unatarajia kumalizika leo.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.