Wadau wa habari wapewa wiki moja kuupitia muswada

Uhuru - - Habari - NA HAPPINESS MTWEVE, DODOMA

WADAU wa sekta ya habari nchini, likiwemo Baraza la Habari Tanzania (MCT), wamepewa wiki moja na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma za Jamii, kuhakikisha wanawasilisha maoni yao kwa ajili ya kuboresha Muswada wa Sheria ya Huduma za Habari wa mwaka 2016, unaotarajiwa kuwasilishwa bungeni hivi karibuni.

Kauli hiyo imekuja baada ya wadau hao, kugomea kutoa maoni yao mbele ya kamati hiyo, ambayo jana ilianza kupokea maoni ya wadau.

Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kuahirisha kikao hicho katika ukumbi wa Ofisi ya Mkaguzi Mkuu na Mdhibiti wa Hesabu za Serikali mjini hapa, Mwenyekiti wa kamati hiyo, Peter Serukamba, alisema bunge haliwezi kuahirisha shughuli zake kwa sababu ya kusubiri maoni ya wadau.

Serukamba alisema maoni ya wadau ni muhimu kwa sababu yatasaidia kuboresha zaidi muswada huo, utakaotumika kwa faida ya Watanzania.

“Ndio maana tunawapa muda wa wiki moja wadau hawa wajikusanye na kupitia muswada huu na kisha watuwasilishie maoni yao kwa maandishi au maneno,” alieleza.

Aidha, katika kikao hicho, kuliibuka mzozo na mvutano mkubwa, ambao ulitawaliwa na mabishano miongoni mwa wabunge na wadau hao, kuhusu ushirikishwaji wa wadau wa habari katika mchakato wa kuandaa muswada huo.

Awali, kabla ya kukaribishwa kwa wadau hao kutoa maoni yao, mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe, aliomba kutoa hoja kwa kamati hiyo, akimtaka Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye, aithibitishie kamati hiyo kuhusu kushirikishwa kwa wadau hao katika mchakato huo.

Hoja ya Zitto, ilizua mtafaruku baina ya wabunge hao huku wengine wakidai haina mashiko kwa kuwa, wadau walishirikishwa tangu mwanzo kwenye mchakato huo na wengine wakitaka Waziri Nape ajibu hoja ya Zitto, hali iliyomlazimu Serukamba kuwatoa nje wadau hao ili wabunge wafikie muafaka.

“Baada ya wadau hao na waandishi wa habari kurejea tena kwenye kikao hicho, ndipo mwenyekiti wa kamati hiyo aliwataka wadau hao kuwasilisha maoni yao,”alisema.

Wadau waliohudhuria na kugoma kutoa maoni ni Chama cha Wamiliki wa Vyombo ya Habari (MOAT), Jukwaa laWahariri (TEF), Baraza la Habari Tanzania (MCT), MISA-Tanzania, Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Umoja wa Klabu za Waandishi wa Habari Tanzania (UTPC) na Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS).

Katibu Mtendaji wa MOAT, Henry Mhanika, akiwasilisha maoni kwa niaba ya chama hicho, alisema bado wanaendelea kukusanya maoni kwa wadau, hivyo muda waliopatiwa kwa ajili ya kuupitia muswada huo hautoshi.

Alisema hivi sasa, baadhi ya wamiliki bado wanaendelea kuupitia muswada huo, ndio maana wanaomba wapatiwe muda angalau hadi Februari, mwakani, ili waweze kuwafikia wadau wengi zaidi na kupata maoni yenye tija.

Mhanika aliieleza kamati hiyo kuwa, MOAT haijawahi kushirikishwa kwenye mchakato huo na kwamba hiyo ni mara yao ya kwanza.

Mwakilishi wa MCT, Pili Mtambalike, alisema pamoja na kwamba mchakato wa kuanzishwa kwa sheria hiyo una takribani miaka 10, muswada uliosomwa hivi karibuni bungeni umebainika kuwepo na baadhi ya vifungu vinavyohitaji umakini katika kuvipitia na kuvitolea mapendekezo.

Alitaja baadhi ya vifungu hivyo kuwa ni pamoja na kifungu kinachompa mamlaka Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), kung’oa mitambo ya uchapishaji katika chombo chochote cha habari endapo atahisi au kubaini kuwa kinachapisha taarifa yeyoye yenye kashfa.

“Pia tumebaini kuwepo katika muswada huu, sheria ya habari ya mwaka 1970, inayompa mamlaka waziri kulifungia gazeti wakati wowote, imerejeshwa bila kubadilishwa. Sisi kama MCT wadau wetu ni vyombo na taasisi za habari, tunahitaji muda kuupitia muswada huu ili tuje na kauli moja,”alisisitiza.

Katibu wa TEF, Neville Meena, alisema wadau wa habari hawajaupinga muswada huo, ila wameomba kuongezewa muda wa kuupitia vizuri, ikiwa ni pamoja na kuwashirikisha wadau wengi zaidi na kutoka na tamko moja litakaloboresha muswada huo.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.