Wauguzi watumia tochi kuzalisha

Uhuru - - Habari - NA WILIUM PAUL, MOSHI

WAUGUZI wa Kituo cha Afya cha Pasua kilichopo wilayani Moshi mkoani Kilimanjaro, wanatumia tochi za simu za mkononi kumulika nyakati za usiku ili kuwazalisha kinamama wajawazito pindi umeme unapokatika nyakati za usiku.

Hayo yalibainishwa na Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) Mkoa wa Kilimanjaro, Juma Rahibu, wakati vijana wa umoja huo, walipokwenda kufanya usafi katika hospitali hiyo na kuwatembelea wagonjwa.

Rahibu aliiomba serikali kutatua tatizo hilo kwa kuwaletea umeme wa jua au jenereta ili wapate umeme wa uhakika.

Aidha, hospitali hiyo inakabiliwa na tatizo la uhaba wa wodi za kulaza wagonjwa, hali inayosababisha watoto wachanga wanaolazwa katika hospitali hiyo, kuchanganywa na kinamama katika wodi moja.

Mwenyekiti huyo pia alipokea kero ya wagonjwa wanaotegemea hospitali hiyo kukosa dawa, hali inayosababisha kununua dawa nje ya hospitali hiyo.

Kwa upande wake, Katibu wa UVCCM mkoa, Yasin Lema, alisema umoja huo umejijengea utaratibu wa kuwa karibu na jamii kwa kuwatembelea wagonjwa, kufanya usafi, kujitolea damu na shughuli mbalimbali za kimaendeleo.

Kaimu Mganga Mfawidhi wa hospitali hiyo, Dk. Michael Ndaishao, alisema hospitali hiyo inakabiliwa na changamoto mbalimbali, ikiwemo upatikanaji hafifu wa dawa zinazotoka katika Bohari Kuu ya Dawa (MSD)

Ndaishao alisema dawa zinazotoka MSD, zimekuwa hazifiki kwa wakati huku zile zinazofika huwa ni zile ambazo hawajaziagiza.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.