Jiji la Mbeya latakiwa kurudisha fedha

Uhuru - - Habari -

HALMASHAURI ya Jiji la Mbeya imegizwa na Kamati ya Bunge na Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC), kuhakikisha inazirejesha fedha zilizotumika kinyume cha utaratibu, zikiwemo sh. milioni 45, za mfuko wa jimbo, ambazo zimetumika bila kumshirikisha mbunge.

Pia, imeagizwa kutolewa kwa sh. milioni 118, ambazo zilitengwa kwa ajili ya mradi wa maji na zingine zilizotolewa kwenye akaunti ya maji, zirejeshwe kabla ya Aprili 30, mwakani.

Halmashauri hiyo ilinusurika kutimuliwa na kamati hiyo baada ya baadhi ya wajumbe kumshauri mwenyekiti kuirudisha kutokana na majibu yao kutoridhisha wajumbe.

Akisoma maagizo ya kamati hiyo juzi, Makamu Mwenyekiti wa LAAC, Abdallah Chikota, alisema halmashauri hiyo ina matumizi mabaya ya fedha za miradi na imekuwa ikibadili matumizi kinyume na utaratibu.

“Mmekuwa mkikopa fedha nyingi na kuzipeleka kwenye matumizi mengine na hazirudi. Tunaomba kujua ni kwa sababu gani kwani ni kinyume na sheria,”alisema Chikota.

Alisema tabia ya kuhamisha fedha za miradi na mafungu mengine, ikiwemo za Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF), haitakiwi na kuagiza fedha hizo zirejeshwe na kutumika kwa malengo yaliyokusudiwa.

Kuhusu fedha za mfuko wa jimbo, Chikota alisema halmashauri hiyo imekuwa ikitumia fedha bila kumshirikisha mbunge wa jimbo husika, ambaye ni mbunge wa jimbo la Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi.

Alisema hatua hiyo inakiuka muongozo wa matumizi ya fedha za mfuko wa jimbo na kuagizwa kutotumia fedha hizo bila kumshirikisha mbunge na fedha zilizotumika mwaka huu, zirejeshwe ili zitumike kwa shughuli zilizoainishwa.

Aliyataja maagizo mengine kuwa ni pamoja na kuandaa kitabu kipya cha utekelezaji wa maagizo ya hoja za ukaguzi 118 na kikamilike kabla Desemba 30, mwaka huu, na kuwasilishwa ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).

Alisema kwa kuwa halmashauri hiyo itaitwa tena Januari, mwakani na kuna gharama, ambazo zimetumika, halmashauri ikapige hesabu ya fedha zilizotumika kuja Dodoma, jana, za kujikimu na kwamba, itafutwe orodha ya watumishi wote waliohusika na uzembe huo ili zirudishwe na taarifa iende kwa CAG.

Awali, akichangia hoja hiyo, mjumbe wa kamati hiyo, mbunge wa Rombo, Joseph Selasini (CHADEMA), alisema haiwezekani fedha hizo zihamishwe wakati ni makosa kuchukua fedha hovyo.

Alisema fedha za mfuko wa jimbo zimechukuliwa kibabe wakati zina utaratibu wake kisheria.

Naye Mbunge wa Mbeya Mjini, Mbilinyi, alisema anashukuru kamati hiyo kwa kupigania fedha za jimbo zirejeshwe, sambamba na fedha za mafungu mengine.

Kwa upande wake, Mbunge wa Njombe Kusini, Edward Mwalongo (CCM), alimshauri mwenyekiti kuwa ni vyema akaiita halmashauri hiyo kwenye kikao ili iende kujibu hoja kikamilifu.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.