Manispaa Dodoma, CDA wapanga mikakati

Uhuru - - Habari -

MENEJIMENTI ya Manispaa ya Dodoma na Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu (CDA), zimetakiwa kufanya kazi pamoja ili kuhakikisha serikali inapohamia Dodoma, hakutakuwa na matatizo yoyote.

Hayo yalisemwa juzi, mjini hapa, katika kikao kilichofanyika chini ya Mwenyekiti wake, ambaye ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Uratibu, Bunge, Ajira, Vijana na Walemavu, Jenista Mhagama, ambacho kilijumuisha wakurugenzi wa taasisi hizo na menejimenti zake, wakiwemo madiwani.

Akizungumza baada ya kumalizika kwa kikao hicho, Jenista alisema ipo haja ya kujitafakari kuona kwa kiasi gani taasisi hizo mbili zitaweza kutekeleza yale, ambayo viongozi wa juu wamekuwa wakiyasema hususan serikali inapohamia Dodoma.

Jenister alisema wanataka serikali inapohamia Dodoma, isikutane na vikwazo, ambavyo viongozi wakubwa wanaviona vitaweza kuwa sababu ya kutohamia Dodoma.

Alisema katika kikao hicho, wamejaribu kutazama mfumo wa utendaji katika taasisi hizo ili kukamilisha zoezi la serikali kuhamia Dodoma.

Pamoja na kuangalia mfumo huo, pia alisema wameangalia mfumo wa kisheria ulivyo katika kuruhusu taasisi zifanye kazi kwa pamoja.

Alisema kikao kimejaribu kuangalia mfumo wa mawasiliano wa taasisi hizo ili kurahisisha mchakato wa serikali kuhamia Dodoma.

Meya wa Manispaa ya Dodoma, Jaffary Mwanyemba, alisema kikao hicho ni cha kuweka mahusiano mazuri kati ya CDA na manispaa hiyo ili wananchi waweze kunufaika na huduma zinazotolewa na mamlaka hizo mbili.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.