ACT-Wazalendo kuwasilisha muswada bungeni

Uhuru - - Habari -

KAMATI ya Katiba na Sheria ya Chama cha ACT Wazalendo, inatarajia kuwasilisha bungeni Muswada wa Sheria ya Mabadiliko ya 15 ya Katiba ya Tanzania ya mwaka 2016, kuhusu masuala ya mafuta na gesi asilia Zanzibar ili kuipa mamlaka kamili.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini hapa, juzi, Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe, alisema muswada huo utawasilishwa kupitia yeye, ambaye ni mbunge wa chama hicho.

Zitto alisema, tayari amewasilisha barua kwa Katibu wa Bunge, Thomas Kashilila, kuhusiana na azima hiyo.

Alisema Oktoba 8, mwaka huu, ACT -Wazalendo ilifanya mkutano mkuu wa kidemokrasia (MMK), uliolenga masuala mbalimbali yahusuyo nchi, ambapo pamoja na mambo mengine, walitoka na maazimio kadhaa, ikiwemo suala la kuibua upya mchakato wa katiba mpya.

Alilitaja jambo lingine kuwa ni Sheria Mpya ya Usimamizi, Utafutaji na Uchimbaji wa Mafuta na Gesi Asilia, iliyotungwa na Baraza la Wawakilishi la Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, ili kuanzisha kampuni ya maendeleo ya mafuta na gesi asilia Zanzibar (ZPDC), ambayo itashiriki shughuli za utafutaji na uendelazaji wa mafuta na kesi asilia kwa niaba ya serikali ya Zanzibar.

“Sheria husika ilitungwa na kupitishwa mwezi huu na baraza hilo la kutunga sheria Zanzibar, katika vikao vyake vilivyomalizika hivi karibuni,”alisema.

Alisema mabadiliko hayo yatawezesha kuanzishwa kwa kampuni hiyo, ambayo itashiriki katika shughuli za utafutaji na uendelazaji wa mafuta na kesi asilia kwa niaba ya serikali ya Zanzibar.

Alisema wanasheria mbalimbali walieleza kuwa, vikwazo vya kisheria na kikatiba vitawasababisha wawekezaji wa sekta ya mafuta na gesi asilia, kutothubutu kufanya uwekezaji Zanzibar, na hivyo kuwanyima fursa Wazanzibari ya kufaidika na rasilimali za Taifa.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.