Wazazi waungane na serikali katika elimu

Uhuru - - Maoni - NA ATHNATH MKIRAMWENI

IMEFIKA wakati kila mwananchi kuwa na uchungu na nchi yake katika suala zima la maendeleo, hususan katika sekta ya elimu nchini.

Pia, kuungana na walimu katika kuhakikisha wanafunzi wanakuwa na nidhamu kwenye masomo yao kwa ajili ya kutengeneza taifa la baadae lenye nidhamu na mafanikio.

Hilo kwa sasa limekuwa halipewi nafasi kubwa na wazazi wengi hasa kwa kipindi hiki ambacho serikali inatimiza ahadi yake ya elimu bure kwa wanafunzi ikiwa na lengo la kutengeneza kizazi bora kilichosoma na kitakachokuwa na wataalamu wa kutosha.

Aidha, inatatakiwa kila mwananchi kutambua nyakati na majira yanavyokwenenda ndipo tutakapoweza kufikia mapinduzi ya kimaendeleo katika suala la elimu.

Inasikitisha kuona wakati serikali ikijititahidi kuwatimizia wananchi wanachokihitaji lakini baadhi ya wananchi wanashindwa kwenda na kasi hiyo kwa angalau kuwahimiza wanafunzi kwenda shule na kuweka jitihada katika masomo.

Hali hiyo inasababishwa na baadhi ya wazazi kuwa na tabia isiyo nzuri ya kutowawekea mkazo watoto wao kuhusu mahudhurio ya shuleni.

Baadhi ya wazazi wanashindwa kutazama mbali na kutambua kuwa jukumu la ‘kumkaba’ mtoto na kuhakikisha anahudhuria kikamilifu shuleni liko mikononi mwao lakini wakati mwingine utashangaa kusikia wakiwaambia watoto wao waliotega shule “Utajijua wewe kwani serikali si inatoa elimu bure usome, usisome ni shauri yako” hii ni kauli ya aabu na haiaswi kuungwa kuendekezwa.

Ukweli ni kwamba kauli hiyo sio nzuri kwa mzazi mwenye nia ya taifa lake kuwa na maendeleo kwa sababu anakuwa hajengi msingi mzuri kwa mtoto na nchi kwa ujumla bali anabomoa.

Taifa lolote haliwezi kuendelea kama halitakuwa na wasomi wa kutosha ikiwa na maana kuwa hakutaweza kuwa na madaktari, viongozi wazuri, walimu, wauguzi, wachumi na wataalamu wote wanaohitajika kwenye sekta mbalimbali.

Tabia hiyo, pia inasababisha na kuchochea taifa kuwa tegemezi kwa kutokuwa na uchumi imara kwa kutokuwepo na wasomi watakaosaidia maendeleo nchini.

Tukumbuke maadui watatu wa maendeleo ni ujinga, maradhi na umaskini kwa hiyo tusipokuwa mstari wa mbele kumhimiza mtoto kusoma hatuwezi kuwakabili wala kuwadhibiti maadui hao.

Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere aligiza vita kali dhidi ya maadui hao baada ya kutazama mbali kuwa endapo wataedelea kuizunguuka jamii ya Watanzania watasababisha athari kubwa na kusababisha udumavu wa maendeleo.

Hivyo basi tusipozingatia umuhimu wa elimu hatutaweza kufika mbali na kusababisha tuwe na watu wa kuhangaika, kuombaomba na hatimaye hatutaweza kufikia mafanikio.

Ni vyema kila mmoja katika jamii kuwa mlinzi kwa mwenzake na kuhakikisha kila mtoto aliyefikia umri stahili anapata elimu ya uhakika itakayomsaidia katika maisha yake binafsi na taifa kwa ujumla siku za usoni.

Tuwe mstari wa mbele kuunga mkono juhudi za serikali za katika elimu kuanzia elimu ya msingi hadi sekondari na kuhakikisha inaleta mafanikio kwa taifa.

Endapo tutashirikiana katika mapinduzi haya, walimu, wazazi, wanafunzi na serikali tunaweza kufika mahala pazuri kimaendeleo na taifa kuwa na vijana waliosoma na kuwa chachu ya maendeleo ya uchumi hapa nchini.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.