Kwa hili la machinjio ya Ruvu wanaokwamisha wamulikwe

Uhuru - - Maoni -

MOJA ya habari kubwa zilizokuwa kwenye gazeti hili toleo la jana ilikuwa ni ile inayohusu kupigwa danadana kwa ujenzi wa machinjo ya kisasa yaliyopangwa kujengwa Ruvu mkoani Pwani.

Katika habari hiyo ilibainika kwamba licha ya mchakato wa ujenzi wa machinjio hayo kutekelezwa kwa hatua mbalimbali, lakini hadi sasa suala hilo linaonekana kuwa katika giza nene.

Inadaiwa kwamba licha ya mchakato wa Zabuni Namba PA/110/2014-2015/HQ/W/01, kuanza tangu Aprili 10, 2015 hadi sasa hakuna jambo linaloendelea kuhusiana na kuanzishwa kwa machinjio hayo.

Uchunguzi zaidi ndani ya Mamlaka ya Ranchi za Taifa (NARCO) ulibaini kuwa baada ya kipindi cha zaidi ya mwaka mmoja na nusu kupita, mamlaka hiyo sasa inadai haina fedha kwa ajili ya mradi huo.

Wakati kukiwa na madai ya kutokuwa na fedha, uchunguzi ulibaini kwamba NARCO inataka kutangaza upya zabuni hiyo.

Kwa lugha nyepesi tunaweza kusema kwamba ujenzi wa machinjio hayo ambayo pamoja na kuwa moja ya njia za kutatua tatizo la usalama wa nyama na kutengeneza fursa za ajira, wapo baadhi ya watendaji wanaotaka kuendeleza utamaduni wa kutengeneza mazingira ya kupoteza fedha za serikali na kuwanyima huduma stahili wananchi.

Kila mmoja anatambua moja ya ahadi na azma ya Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais Dk. John Magufuli ni kuifanya Tanzania kuwa nchi ya viwanda.

Lengo hilo ni sehemu ya utekelezaji wa mkakati wa kuipandisha nchi kuwa ya uchumi wa kati mwaka 2025 sambamba na kupunguza hali ya umasikini kwa watu wake.

Lakini inaonekana wapo baadhi ya watumishi ndani ya serikali ambao bado wana dhana ya ‘kupiga’ fedha za umma ikiwa na maana ya kutengeneza mazingira ikiwa ni pamoja na kupanga kufungua upya tenda za zabuni ili kutengeneza mazingira ya kushirikiana na mwombaji ambaye ama wameshamuandaa au wanapanga kumsaka ili kujipatia fedha kwa njia za ujanjaujanja.

Jambo hili linapaswa kutazamwa kwani moja ya sifa ya serikali ya awamu ya tano ni pamoja na kutoa uamuzi na utekelezaji kwa haraka. Mambo ya mchakato, njoo kesho, mikakati inafanyika hayo yamepitwa na wakati na hayapaswi kupewa nafasi.

Kwa hili linaloendelea katika ujenzi wa machinjio hayo ni dhahiri inaonekana wapo wajanja wachache wanaotaka kuturudisha huko, hatupaswi kuwafumbia macho.

Ikumbukwe kwamba kukamilika kwa machinjio hayo, pia kutasaidia kutatua changamoto ya migogoro ya wakulima na wafugaji mkoani Pwani ambayo kwa sasa imekuwa ikiumiza vichwa vya wananchi na viongozi kwenye maeneo mbalimbali nchini.

Kwa kujengwa machinjio hayo kutatoa fursa ya mifugo kuuzwa kwa bei nzuri, hivyo kutoa hamasa kwa wafugaji kuondokana na ufugaji wa kizamani wa kuwa na makundi makubwa ya mifugo badala yake kufuga kisasa huku wakiyatumia machinjio hayo kuuza mifugo yao na kujiendeleza kwenye shughuli nyingine za maendeleo.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.