Mfalme Kigeli V atajwa mmoja wa wafalme maskini

N Alikuwa akidai yeye ni mfalme wa Afrika n Aliwahi kuishi Tanzania, Kenya na Uganda

Uhuru - - Maoni - KIGALI, Rwanda

RWANDA ni nchi ambayo watu wengi, walikuwa hawajui kuwa ilikuwa ni ya kifalme, ambapo mfalme wa mwisho kuitawala nchi hiyo ilikuwa mwaka 1961.

Mwaka huo, ndio utawala wa kifalme nchini humo uliondolewa, ambapo wafalme wengi nchini humo walikuwa wanatambuliwa kwa jina la Mwami au Umwami, huku wengine wakiitwa Abami.

Mwami wa mwisho kutawala Rwanda alikuwa Mfalme Kigeli V (Kigeli wa Tano) ambaye aliondolewa madarakani 1961 na kuamua kwenda kuishi uhamishoni nchini Marekani.

Mfalme Kigeli V alizaliwa Juni 29, 1936 eneo la Kamembe Kusini magharibi mwa Rwanda akiwa mwana wa Mfalme Yuhi V Musinga, na Malkia Mukashema. Alitoka jamii ya Watutsi.

Wakati wa kuzaliwa kwake, baba yake alikuwa ameondolewa madarakani na Wabelgiji kwa kushukiwa kupendelea sana wakoloni wa awali Ujerumani.

Alikuwa amewekwa eneo lililotengwa kusini magharibi mwa Rwanda lakini miaka minne baadaye, familia yao yote ilihamishiwa Jamhuri ya Kidemokrasia Congo(DRC).

Baba yake alifariki kutokana na kichomi (nimonia) mwaka 1944.

Jina lake la kuzaliwa ni Ndahindurwa.Alibatizwa katika kanisa Katoliki la Kirumi na akaongezewa jina Jean-Baptiste.

Alipata masomo ya msingi katika shule za Groupe Scolaire d’Astrida kisha akapata elimu ya juu katika chuo cha Nyangezi katika nchi ya Zaire(sasa inaitwa DRC).

Baada ya kuondolewa madarakani kwa baba yake Mfalme Yuhi V Musinga, kaka yake wa kambo alitawazwa Mfalme Mutara III Rudahigwa. Alisaidia kutetea familia ya Musinga kukubaliwa kurejea nyumbani Rwanda.

Mfalme Kigeli baada ya kumaliza masomo yake alifanyia kazi utawala wa wakoloni wa Ubelgiji katika jimbo la Astrida kusini mwa Rwanda kati ya 1956 na 1958.

Aliteuliwa naibu chifu wa eneo la Bufundu mwaka 1959, na baadaye akateuliwa kuwa chifu kamili.

Mfalme Mutara aliugua baada ya kudungwa sindano na daktari Mbelgiji na akafariki dunia Julai 25, 1959.

Mutara alikuwa ameoa lakini hakuwa amejaliwa watoto. Wakati wa mazishi yake, wasimamizi wa urithi walimtangaza Ndahindurwa kuwa mfalme mpya na akachukua jina Mfalme Kigeli V, wakati huo akiwa na miaka 23 pekee.

Novemba mwaka huo, chini ya mwezi mmoja baada yake kuapishwa, Wahutu walio wengi waliasi na kuwaua mamia ya Watutsi huku wengine wakilazimika kukimbilia nchi jirani.

Wahutu walimtazama Mfalme Kigeli kama mwakilishi wa “mfumo dhalimu wa wakoloni na Watutsi”.

Mfalme Kigeli V alikimbilia Congo, ambayo ilikuwa imejipatia uhuru siku chache awali.

Alirejea kwa muda mfupi Septemba mwaka uliofuata wakati kura ilikuwa inapigwa kuamua hatima ya taifa hilo. Zaidi ya asilimia 80 walipiga kura kupinga utawala wa kifalme na kumpinga Mfalme Kigeli, wakati huo akiwa chini ya kizuizi cha nyumbani.

Oktoba 2, 1961, siku chache kabla ya uchaguzi mkuu na miezi michache kabla ya Rwanda kujipatia uhuru wake, Mfalme Kigeli alisafirishwa hadi Tanzania kuishi uhamishoni.

Hakuwahi kurejea tena nchini Rwanda tangu siku hiyo. Rwanda ilijipatia uhuru kama Jamhuri, Mhutu Dominique Mbonyumutwa akiwa rais.

Kwa miaka iliyofuata, aliishi katika nchi kadhaa uhamishoni.

Alikuwa amepewa nyumba na Idi Amin nchini Uganda mwaka 1973 lakini mtawala huyo wa kiimla alipoondolewa madarakani miaka sita baadaye, akalazimika kuikimbia nchi hiyo na kuingia Kenya.

Miaka ya 1980, hali ya kisiasa nchini Rwanda ilianza kuwa mbaya na Rais Juvenal Habyarimana aliyekuwa ametawala kwa mabavu kwa miongo miwili alilazimishwa kugawana madaraka na vyama vingine. Makundi ya Watutsi yaliyokuwa uhamishoni yalianza uvamizi na hapo uhasama baina ya Wahutu na Watutsi ukafufuliwa.

Rais Habyarimana alikuwa rafiki wa Rais wa Kenya, Daniel arap Moi na Mfalme Kigeli hakujihisi salama na ndipo akatumia urafiki aliokuwa ameunda na Mmarekani Bill Fisher kuhamia Marekani.

Alitua Oklahoma mwaka 1992, ambapo katika mahojiano na vyombo vya habari vya Marekani, mwaka 2007, Mfalme Kigeli alisema alitaka kurejea nchini mwake na kutawala tena.

Hata hivyo, alisema angerejea tu iwapo Wanyarwanda walimtaka arejee na iwapo wangekuwa tayari kumtambua kama mfalme wa kikatiba na tayari alikutana na Rais Paul Kagame.

Alikuwa bado anajichukulia kama mfalme kwa sababu alisema aliondolewa uongozini kwa njia isiyo halali huku akiwa hajafanya chochote kibaya ikiwa kujilimbikizia mali.

“Raia wa Rwanda wanaweza kunitaka au huenda wasinitake. Lakini ndipo nirejee nyumbani, nahitaji kufahamu iwapo bado wanataka niwe mfalme wao,” aliwahi kunukuliwa na waandishi wa habari huku akidai anapendwa aitwa mfalme wa Afrika.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.