Kakaye Obama amuunga mkono Donald Trump

N Obama asema Trump akishinda atamkabidhi madaraka bila nongwa

Uhuru - - Maoni - NEWYORK, Marekani

VITA ya urais wa Marekani, imeanza kuipasua familia ya rais wa nchi hiyo, Barack Obama, baada ya kaka wa rais huyo, Malik anayeishi Kenya, kualikwa nchini humo, kumuunga mkono mgombea wa Republican, Donald Trump.

Maliki, (pichani) ambaye kwa muda mrefu amekuwa katika uhusiano mbovu baina yake na Obama, jina lake limetangazwa kuwemo kwenye orodha ya wageni waalikwa watakaotambulishwa na Trump kwenye mdahalo wa mwisho wa wagombe wa urais nchini humo.

Taarifa iliyotolewa jana na maofisa wa kampeni wa Trump, walieleza wana mpango wa kumwalika Maliki kuhudhuria mdahalo wa mwisho wa urais nchini Marekani kwa kuwa ni mtu makini na mwenye uwezo mkubwa.

Tayari, Malik, amepokea mwaliko huo na kueleza kuwa ana furaha isiyo na kifani kwamba atahudhuria mdahalo huo, ambao kwa namna moja au nyingine ataweza kukutana na mgombea bora wa urais nchini Marekani.

“Trump anaweza kuirejeshea Marekani fahari yake tena,” alisema Maliki, ambaye wafuasi wa Obama wanaeleza uhasama wake na ndugu yake, unachochewa na njaa kwa kuwa amekuwa hapokei msaada wowote kutoka kwa rais wa Marekani.

Wagombea wa urais nchini humo, wamekuwa wakitumia wageni kwenye midahalo kama njia ya kuwakabili wapinzani wao, ambapo Hillary Clinton, ambaye ni mgombea wa urais wa Democratic, yeye aliwaalika bilionea Mark Cuban na Ofisa mtendaji mkuu wa kampuni ya Hewlett Packard Enterprise, Meg Whitman.

Katika hatua nyingine, Rais Obama amemshutumu Trump kwa madai anayotoa kwamba kuna hila dhidi yake zinazofanywa katika uchaguzi nchini humo, kwa kumtaka kuacha kulalama.

Alisema malalamiko ya mgombea huyo kuwa anataka kuibiwa kura ni jambo ambalo halijawahi kutokea kwa mgombea yeyote nchini Marekani kujaribu kutilia shaka uchaguzi hata kabla haujafanyika.

“Sijawahi kuona katika maisha yangu ama katika historia za siasa za sasa kwa mgombea yoyote wa kiti cha Urais kujaribu kutilia shaka uchaguzi kabla ya zoezi la upigaji kura kufanyika.”alisema Rais Obama.

Aidha, Rais Obama amempa ushauri mgombea huyo wa Republican kuendelea na kile anachokitafuta kuwa Rais ajaye wa Marekani.

“Namshauri Trump kuacha kulalamika na kujaribu kuchukulia suala lake hilo kujaribu kupata kura. Na kama atapata kura nyingi hivyo itakuwa matarajio yake, ambayo sina uhakika huo,’’alisema.

Aliongeza kusema “Endapo akichaguliwa kuwa rais nitamkaribisha Trump bila kujali alichosema kuhusu mimi ama tofauti yangu dhidi yake juu ya mawazo yangu na pia kumsindikiza kuweza kukabidhiana madaraka kwa amani. Hivyo ndivyo Wamarekani wanavyofanya...’’

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.