Wanajeshi wapelekwa Kinshasa

Uhuru - - Maoni - KINSHASA, DRC

UMOJA wa Mataifa(UN), umewaondoa wanajeshi 300, waliokuwa wakilinda amani mashariki mwa Jamhuri ya kidemokrasi ya Congo na kuwapeleka Kinshasa kusaidia kukabiliana na uwezekano wa ghasia kufuatia kuahirishwa kwa uchaguzi wa urais.

Wanajeshi hao ni wale wanaotoka kwenye vikosi vya jeshi, vinavyounda muungano wa wanajeshi wa MONUSCO, ambapo sasa wanapelekwa Kinshasa, ambako kuna ghasia za wananchi wanaotaka kufanyika kwa uchaguzi nchini humo.

“Tunapanga kwa hali yoyote na tumechukua hatua kuimarisha uwepo wetu Kinshasa,” alisema mkuu wa kikosi hicho, Herve Ladsous wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusiana na uamuzi wao wa kuamia katika mji mkuu wa DRC.

Hata hivyo, alisema huenda wanajeshi hao wanaotumwa wasitoshe iwapo mji mkuu huo utazuka ghasia ambapo alidai Kinshasa ni mji wenye watu zaidi ya milioni 11 na MONUSCO haina idadi ya kutosha ya wanajeshi na pia jukumu lao ni kutoa usalama.

Katika hatua nyingine, makubaliano mengine zaidi yamefikiwa wiki hii kuusogeza mbele uchaguzi huo, hadi Aprili 2018, ambapo upinzani umesusia makubaliano hayo na umeitisha maandamano makubwa ndani ya wiki hii.

Mjumbe wa Umoja wa mataifa kwa Congo, Maman Sambo Sidikou, wiki iliopita ameonya kuwa huenda nchi hiyo ikaingia katika hatari ya kukumbwa na ghasia iwapo hakuna jambo litakalofanyika kukabiliana na mzozo huo.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.