Tanzania tumefaidika na UN- Balozi Mahiga

Uhuru - - Habari - NA RACHEL KYALA

SERIKALI imesema Umoja wa Mataifa (UN), ni jukwaa pekee linalotumika bila woga kuwasilisha hoja mbalimbali, hivyo italitumia ipasavyo kutatua changamoto zinazojitokeza na kujiletea maendeleo.

Aidha, imesema Tanzania imekuwa ikiwakilishwa ipasavyo na mashirika yote ya umoja huo, hususan Shirika la Maendeleo (UNDP), jambo ambalo limeleta manufaa mbalimbali, ikiwemo ajira kwa watu wake.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Augustine Mahiga, alisema hayo jijini Dar es Salaam, jana, wakati akizungumzia maadhimisho ya Siku ya Umoja wa Mataifa, ambayo huadhimishwa Oktoba 24, kila mwaka.

“UN ni mahali pekee ambapo tumekuwa tukipatumia bila woga kuwasilisha kero zote na masuala mengine muhimu katika kujiletea maendeleo, hivyo tunaendelea kuwatunza ipasavyo kwa ujasiri ili tusonge mbele,”alisema.

Pamoja na Watanzania kupata ajira katika umoja huo, Waziri Mahiga, alitaja manufaa mbalimbali, ambayo Tanzania imeyapata kutokana na uanachama wake kwenye mashirika mbalimbali ya UN kuwa ni pamoja na kushiriki kikamilifu katika suala la ukombozi wa bara la Afrika.

Alisema ushindani katika soko la ajira ndani ya UN ni mkubwa, hivyo aliwataka Watanzania, hususan wanafunzi kujifunza lugha mbalimbali ili kukidhi vigezo.

Balozi Mahiga alisema suala lingine ni kusimamia amani na ulinzi, ambapo Tanzania imekuwa ikifanya hivyo kwenye nchi mbalimbali kwa bendera ya UN, ikiwemo Lebanon, Sudan Kusini, Sudan (Darfur) na Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC).

“Kutokana na uanachama wetu UN, tumefaidika kwa kujengwa kwa Mahakama ya Kimataifa ya Mauaji ya Kimbari iliyoko jijini Arusha, ambapo Tanzania ilitengeneza ajira na baada ya kukamilika kwa mashauri hayo, jengo lake litatumika kwa shughuli nyingine,”alisema.

Alisema manufaa mengine yaliyopatikana hivi karibuni ni kukwamuliwa kwa ndege mbili aina ya Bombardier, zilizonunuliwa na serikali, ambapo zilikwamishwa njiani wakati zikija nchini, lakini tatizo hilo lilitatuliwa kupitia Shirika la Umoja wa Mataifa, linaloshughulikia Masuala ya Anga (ICAO).

Waziri Mahiga alisema katika mkutano ujao wa Umoja wa Afrika (AU) utakaofanyika Januari, mwakani, Afrika imekusudia kuomba uanachama wa kudumu UN na kuwa na kura ya turufu kwa nchi za Afrika Kusini na Nigeria. Pia, imepanga kuomba kuongeza wanachama wa mzunguko badala ya Ethiopia na Liberia pekee.

Mwakilishi wa UN hapa nchini, Chansa Kapaya, alisema maadhimisho ya mwaka huu, yamelenga kuelezea kwa undani shughuli zinazofanywa kwa pamoja baina ya wizara hiyo na umoja huo ili kuwezesha maendeleo endelevu.

Alisema upo mpango mpya wa miaka mitano wa maendeleo endelevu (SDG), chini ya ufadhili wa UN kwa serikali ya Tanzania, ujulikanao kama UNDP II 2016 hadi 2021, ambao umesanifiwa na kukubalika na umoja huo.

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa akikagua majengo ya Hospitali ya Wilaya ya Ruangwa mkoani Lindi.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.