Prof. Maghembe ashangazwa na uchafu Chuo cha Utalii Dar

Uhuru - - Habari - NA JESSICA KILEO

WAZIRI wa Maliasili na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe, amesema hajaridhishwa na hali ya usafi katika Wakala wa Chuo cha Taifa cha Utalii.

Ametaka chuo hicho kijulikane kama Chuo Cha Utalii Cha Taifa, badala ya kutumika kwa neno wakala.

Profesa Maghembe alisema hayo jana, jijini Dar es Salaam, alipotembelea chuo hicho Kampasi ya Bustani na kuzungumza na watendaji wake.

Alisema hali aliyoiona katika maeneo mbalimbali ya chuo hicho, ikiwemo eneo la kuhifadhia chakula na jikoni, hayaridhishi na inaondoa hadhi ya chuo.

“Haiwezekani unakuta sehemu inahifadhi vyakula kuna uchafu, watu wamepita na viatu na kuacha uchafu, mazingira machafu, leo nawaonya lakini nikirudi siku nyingine nitabadilika na tutaonana wabaya,”alisema Profesa Maghembe.

Aidha, Waziri Maghembe aliuagiza uongozi wa chuo hicho kubadili jina la chuo hicho na kitambulike kama Chuo cha Taifa cha Utalii, badala ya kuitwa wakala.

“Hatutaki jina la wakala, nini maana ya wakala? Tutakuwa na mkuu wa chuo na wasomi wenye taaluma na bodi ya wanataaluma, tunataka tuzalishe wafanyakazi wanaoweza kufanya kazi katika hoteli kubwa hapa nchini,”aliongeza.

Aliwataka wakufunzi wa chuo hicho kuwafundisha nidhamu wanafunzi wao ili kuepuka aibu wanazokutana nazo katika maeneo yao ya kazi.

Waziri Maghembe alisema ni aibu hoteli nyingi za hapa nchini kuwatumia wafanyakazi kutoka nje ya nchi wakati Tanzania inao wataalamu wanaoweza kufanya kazi hizo.

Alisema tatizo hilo linatokana na wamiliki wengi kuhofu kuajiri wazawa kwa sababu wengi wao ni wezi, hivyo kuchafua sifa za maeneo wanayopewa dhamana ya kuhudumia wageni.

Kwa mujibu wa Profesa Maghembe, matukio hayo yanaweza kuwakatisha tamaa wawekezaji na wale walio tayari kuwekeza kwenye sekta hiyo kushinikiza waje na wataalamu wao.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.