Majaliwa aagiza kukamatwa waharibifu wa mazingira

Uhuru - - Habari - NA MWANDISHI MAALUMU

WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa ameuagiza uongozi wa mkoa wa Lindi, kuhakikisha wanawakamata na kuwachukulia hatua watu wote wanaoharibu mazingira kwa kufyeka na kuchoma moto misitu kwa kuwa wanaharibu mazingira na kusababisha ukame.

Amesema mkoa huo upo hatarini kugeuka jangwa na tayari vyanzo vingi vya maji vimeanza kukauka, kwa sababu ya uharibifu wa mazingira unaotokana na watu kufanya shughuli za kijamii kwenye vyanzo vya maji.

Waziri Mkuu alitoa agizo hilo juzi, wakati akizungumza kwa nyakati tofauti na wananchi wa wilaya ya Ruangwa, katika mikutano iliyofanyika kwenye vijiji vya Nanjaru, Nachinyimba, Nambiranje, Mkaranga, Nandenje, Nachinyimba na Mandarawe.

Alisema wakulima wa ufuta wanatakiwa kuendelea kutumia mashamba yao ya zamani na kuacha tabia ya kufyeka misitu kila mwaka, badala yake waanzishe mpango wa upandaji miti ili kuepusha taifa kugeuka jangwa.

ìVyanzo vya maji vimekauka kwa sababu tumekata miti mingi. Mito yote iliyokuwa inatiririsha maji imekauka. Viongozi wa mkoa hakikisheni misitu inalindwa na atakayekutwa analima kwenye vyanzo vya maji akamatwe,îalisema.

Waziri Mkuu aliongeza: ìUkataji miti huu unaoendelea kwenye maeneo yetu hakutasababisha kukosekana kwa maji tu, bali hata mazao yatapungua. Jambo hili litasababisha njaa kwenye vijiji vyetu, tuache kukata miti.”

Alisema serikari inatumia gharama kubwa kuchimba visima virefu kutafuta maji.

Majaliwa alisema huko nyuma, maji yalikuwa yakipatikana urefu usiozidi mita 20 hadi 30, ardhini huku gharama yake ikiwa sh.milioni 35, lakini hivi sasa wanalazimika kuchimba mita zaidi ya 150, kwa gharama ya sh. milioni 75, kwa kisima kimoja.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Godfrey Zambi, aliwataka watendaji wa kata na vijiji kuimarisha ulinzi wa maeneo ya misitu na vyanzo vya maji na atakayeshindwa kufanya hivyo achukuliwe hatua kali za kisheria.

“Hatuko tayari kutengeneza jangwa, hivyo tutapamba na wote wenye tabia ya kuchoma misitu au kulima kwenye vyanzo vya maji,”alisema.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.