DC Bunda awasweka ndani watendaji Mamlaka ya Maji

Uhuru - - Habari - Na Mwandishi Wetu, Bunda

MKUU wa Wilaya ya Bunda, Lydia Bupilipili, ameamru kukamatwa kwa Meneja wa Maji wa Mamlaka ya Mji wa Bunda na msaidizi wake kwa tuhuma za usimamizi mbaya wa mradi wa maji uliosababisha kukosekana kwa huduma hiyo katika mji huo na vitongoji vyake.

Bupilipili, alichukua hatua hiyo jana, ofisini kwake baada ya kutoridhishwa na utendaji kazi wa meneja huyo, Mansour Mawilid na msaidizi wake, Malecela Maisha, hususan baada ya kushindwa kutekeleza majukumu yao.

Mkuu huyo wa wilaya alizitaja tuhuma za viongozi hao kuwa ni wananchi kuendelea kulipa bili za maji dirishani, badala ya benki, kushindwa kuwafikisha mahakamani wanaohujumu miundombinu ya maji, kukaidi kutoa taarifa za maji kwake na kutoza faini chini ya kiwango.

Alifafanua kuwa kutokana na udhaifu huo, huenda kuna mazingira ya rushwa, ambayo yanazorotesha huduma ya mradi wa maji wa Nyabehu/Bunda na kuusababishia kukwama, hivyo kuwaathiri wananchi kwa kukosa maji.

Aliwaagiza polisi kuwaweka ndani kwa amri yake kwa muda wa siku mbili kisha wakitoka wajadiliane naye, wakiwa na majibu sahihi ya kuboresha huduma za maji katika mji wa Bunda.

Mkazi wa mji huo, Jonh Kitangosa, aliunga mkono kuwa huduma za maji Bunda ni hafifu kutokana na usimamizi mbovu wa watendaji wa idara ya maji.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.