Wanafunzi 171 wasoma darasa moja Iduda

Uhuru - - Habari - NA SOLOMON MWANSELE, MBEYA

SHULE ya msingi Iduda iliyoko katika Halmashauri ya Jiji la Mbeya mkoani hapa, inakabiliwa na upungufu wa vyumba vya madarasa, hali inayosababisha wanafunzi 171 kusoma katika darasa moja.

Imeelezwa kuwa hata wanafunzi waliohitimu darasa la saba hivi karibuni, walikuwa 164 na walikuwa wakikaa darasa moja, hali iliyosababisha kuwepo kwa ugumu wa ufundishaji.

Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Leonard Siwavula, aliyasema hayo jana, mbele ya Katibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Wilaya ya Mbeya Mjini, Robert Kerenge, ambaye aliwaongoza wanaCCM wa Kata ya Iduda, tawi la NADO, kukabidhi msaada wa madawati 10, ambayo walichangishwa katika tawi hilo.

Matawi mengine ya CCM ya MECCO na Iduda, yanayounda kata hiyo, nayo yanatengeneza madawati 10 kila moja, hivyo matawi hayo matatu yanatarajia kutoa msaada wa madawati 30, kwa shule hiyo ili kupunguza uhaba wa madawati.

“Darasa la sita wapo wanafunzi 171 na wanasomea chumba kimoja.

Hali hii ni changamoto kwani tuna uhaba wa vyumba vya madarasa na tunategemea zaidi nguvu ya wananchi katika ujenzi wa madarasa,” alisema.

Aliongeza kuwa hivi sasa shule hiyo ina madawati 348, yakiwemo mapya 120, waliyokabidhiwa hivi karibuni, ambayo yaliyotolewa na Ofisi ya Bunge.

Mwalimu mkuu huyo alisema hadi sasa ujenzi wa vyumba vinne vya madarasa unaendelea, ambapo viwili tayari vimefikia hatua ya kupauliwa na vilivyosalia vipo usawa wa renta.

Hata hivyo, alisema mashimo ya choo nayo ni changamoto nyingine iliyopo shuleni hapo, kwani shule hiyo yenye wanafunzi 902, wakiwemo wasichana 469, wanatumia matundu manne ya vyoo yaliyopo shuleni hapo huku wanaume 433, wakitumia matundu tisa.

“Hivi sasa tupo katika ujenzi wa choo, ambacho kinajengwa na wananchi na hadi sasa wametumia gharama ya sh. milioni 7.2. Changamoto ya vyoo nayo imekuwa inatuumiza kwani idadi ya wanafunzi waliopo ni kubwa,” alisema.

Aliwashukuru wana-CCM wa tawi hilo kwa msaada huo wa madawati 10, waliyoyatoa huku mengine 20, yakitarajiwa kukabidhiwa hivi karibuni na matawi mawili yaliyobaki, hivyo hakuna mwanafunzi atakayekaa chini.

Naye Katibu wa CCM wilaya ya Mbeya Mjini, Kerenge, alisema walitembelea shule hiyo na kujionea hali halisi iliyopo, hivyo waliahidi kufikisha kilio hicho kwa mamlaka zinazohusika ili kiweze kufanyiwa kazi haraka iwezekanavyo.

Kerenge aliwaomba walimu waendelee kuvuta subira wakati hatua za kuzitafutia changamoto zinaendelea kuchukuliwa na kwamba, ofisi yake inachangia sh.500,000 katika ujenzi wa choo unaoendelea.

“Ni kweli walimu kufundisha kwenye darasa lenye wanafunzi zaidi ya 170, kunawakatisha tamaa, hivyo tunalichukua hili na tutalifikisha mbele ya mamlaka husika ili kulitafutia ufumbuzi wa kudumu,”alisema.

Diwani wa kata hiyo , Josephat Nyembele (CCM), alikiri kuwepo kwa changamoto hiyo na alifurahishwa jinsi CCM inavyotekeleza ilani ya uchaguzi kwa vitendo kwa kuchangia madawati hayo.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.